Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha bajeti ya shilingi Billioni 74.2 ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu itakayosaidia kuratibu afua za kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi na kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima amesema vipaumbele vya Wizara hiyo ni pamoja na kutekeleza Mpango wa Taifa wa kuhamasisha na kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi, kukuza ari ya jamii kushiriki katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo .

Akieleza hayo leo Mei 18,2023 Bungeni Dodoma, amesema kwa mwaka wa fedha Wizara itaboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, kuratibu utoaji wa huduma za msingi kwa watu wenye mahitaji maalum ikiwemo huduma za msaada wa kisaikolojia kwa manusura wa majanga mbalimbali na makundi mengine yenye uhitaji katika jamii.

Amevitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuratibu na kuwezesha upatikanaji wa haki za watoto na huduma za ustawi wa jamii kwa wazee, kuimarisha mifumo ya malezi, ulinzi na maendeleo ya watoto na familia na kuimarisha utendaji kazi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

“Mchango na ushiriki wa Mashirika hayo katika maendeleo ya Taifa utasaidia kutambulika na kuwa na tija kwa jamii, ” mesisitiza.

Akizungumzia shughuli za maendeleo,Dkt.Gwajima amesema Wizara inakadiria kutumia Shilingi Billioni 30.5 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na kwamba Kati ya fedha hizo, Shilingi Billioni 26.8 ni Fedha za Ndani na Shilingi Billioni 3.7 ni Fedha za Nje.

“Kwa mwaka 2023/24, Wizara inaomba jumla ya Shilingi Billioni 74.2 ili kutekeleza majukumu yake kwa maendeleo na ustawi wa jamii kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi, kukuza ari ya jamii kushiriki katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo,”amefafanua.

By Jamhuri