NA MICHAEL SARUNGI

Tatizo la rushwa kupenya katika mpira wa miguu limelitikisa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kiasi cha kuamua kufuta posho za waamuzi kulipwa na vyama na mashirikisho Afrika. Sasa posho zao zitalipwa moja kwa moja kutoka CAF kwa waamuzi watakaochezesha mechi.

Wakizungumzia hali hiyo, viongozi wa mchezo huo ndani na nje ya Tanzania, wamesema kuna haja ya waamuzi kuanza kujiuliza maswali magumu juu ya kwa nini hawaishiwi kunyooshewa vidole wanapokuwa katika majukumu yao.

Leslie Liunda, Mkufunzi wa Waamuzi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), amesema suala la waamuzi kuboronga limeendelea kuwa sugu kila kukicha, hali ambayo imeanza kukwamisha jitihada za kuhakikisha mchezo wa soka unakua.

Amesema licha ya kuwa malalamiko ya harufu ya rushwa dhidi ya waamuzi wanaosimamia mechi mbalimbali nchini umekithiri, lakini bado kuna haja ya viongozi kuhakikisha waamuzi hawa wanapewa semina za mara kwa mara ili kuendana na mpira wa kisasa.

Katibu huyo wa zamani wa Kamati ya Wamuuzi nchini, amesema hofu yake ni kuhusu uwezo wa waamuzi kuchezesha mechi na si kuzifahamu sheria 17 za mchezo huo, unaoongoza kupendwa na watu wengi nchini na duniani kote.

Amesema japo mpira wa miguu nchini unakabiliwa na matatizo mengi, lakini pia uamuzi mbovu wa baadhi ya waamuzi nchini umekuwa ukichangiwa na uelewa ndogo wa baadhi ya viongozi wa mchezo huo nchini wasiojua sheria.

Ni kweli kumekuwepo na tuhuma mbalimbali kwa baadhi ya waamuzi kuhusishwa na masuala ya rushwa michezoni, lakini kuna haja ya kwenda mbali zaidi ya hapo na viongozi wa klabu wanapaswa kuwa na uelewa wa kutosha wa mchezo wenyewe,” amesema Liunda.

Amesema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linatakiwa kuwa makini zaidi hasa katika kipindi hiki ambacho malalamiko juu ya waamuzi yamekuwa yakiendelea kutokea kila siku iendayo kwa Mungu.

Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT), Alhaj Muhidin Ndolanga, amesema tuhuma hizi zinapaswa kufanyiwa kazi ili kuondoa utata unaozidi kuongezeka na kuharibu taswira ya soka.

Jambo hili linaonekana kuvuka mipaka ya nchi wananchama hadi kufikia CAF kuamua kulivalia njuga huku kila kukicha waamuzi wamekuwa wakiingia lawamani katika michezo mbalimbali,” amesema Ndolanga.

Amesema kuna haja kwa wadau wote wa mchezo wa soka kuungana kwa pamoja kuhakikisha wanapiga vita suala zima la rushwa michezoni, ili kuuondoa mchezo huu kutokana na uchafu huu wa rushwa.

Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad Ahmad, akizungumza na wanahabari siku za karibuni, alitoa onyo kwa waamuzi wa Afrika wanaoendekeza vitendo vya rushwa wakati wa utoaji wa haki katika michuano inayosimamiwa na shirikisho hilo.

Amesema  suala la maendeleo ya soka linatokana na mambo mengi ikiwamo uamuzi sahihi ili timu dhaifu ipoteze na ile bora iweze kupata matokeo ingawa wakati mwingine inakuwa kinyume chake.

Suala la rushwa kwa baadhi ya waamuzi kwenye soka la Afrika linaonekana kama ni tatizo sugu, lakini niseme jambo moja kwamba CAF haijalala wala haijapuuzia taarifa inazozipata juu ya baadhi ya waamuzi kupewa rushwa,” amesema Ahmad.

Amesema umefika wakati kwa wadau wote wa mchezo wa mpira wa miguu kuhakikisha wanajiepusha na vitendo vyote vinavyokiuka maadili ya mchezo wa soka ndani ya nchi zote wanachama wa mchezo wa mpira wa miguu.

By Jamhuri