Home Kurasa za Ndani MIMBA ZA UTOTONI ZINAVYOATHIRI WANAFUNZI DODOMA

MIMBA ZA UTOTONI ZINAVYOATHIRI WANAFUNZI DODOMA

by Jamhuri

NA EDITHA MAJURA

Wanafunzi wa kike 710 mkoani Dodoma hawakufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka jana, kutokana na sababu mbalimbali, 67 kati ya hao wakitokana na ujauzito.

Taarifa ya sekta ya elimu inayowasilishwa na Afisa Elimu wa Mkoa, Maria Lyimo, kwa Kamati ya Ushauri ya Mkoa huo hivi karibuni, imeeleza kuwa Wilaya ya Chamwino imeongoza kwa kuwa na wanafunzi 24 ambao hawakuhitimu elimu ya msingi kutokana na ujauzito.

Wilaya zilizofuatia na idadi ya wanafunzi walioshindwa kuhitimu kwa sababu ya mimba kwenye mabano ni Mpwapwa (13) na Dodoma Mjini (12).

Hali hiyo inajitokeza huku Serikali ikiwa imeweka wazi msimamo wake dhidi ya wanafunzi wa kike katika shule za msingi au sekondari kutoendelea na masomo wanapopata ujauzito.

DC CHAMWINO AFUNGUKA

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamonga, amesema kukua kwa tatizo la ujauzito kwa wanafunzi kunachangiwa na sababu mbalimbali ikiwamo hali duni ya kiuchumi kwa wazazi ama walezi wa mwanafunzi msichana.

Baadhi ya wazazi wanaamini kuwa wasichana wanatakiwa kuendesha maisha ya familia badala ya kusoma, wazazi wa aina hii inapotokea mtoto akapata ujauzito, hawatoi ushirikiano kwa mamlaka zinazohusika,” amesema Nyamonga.

Pia amesema sababu nyingine zinachangia ni wanafunzi wa kike wanaojihusisha na vitendo vya kujamiiana hivyo kujikuta wakipata ujauzito.

HATUA ZA KUCHUKUA

Nyamonga amesema zipo hatua kadhaa zinazochukuliwa ili kukabiliana na tatizo hilo, ikiwamo kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa wanafunzi wa kike, ili kuwajengea uwezo wa kujitambua na kuepuka vyanzo vinavyoweza kuwasababishia kupata ujauzito.

DC KANGOYE

Aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne,  Kangoye, amesema Rais John Magufuli hana mzaha na wahalifu, hivyo ilitarajiwa wanaowapa ujauzito wanafunzi ‘wasifumbiwe macho’.

Wakati wetu, tatizo lilikuwa uwajibikaji kwa ujumla tofauti na hali ilivyo sasa ambapo Namba Moja (Rais Magufuli), anasisitiza  kuzingatia sheria tofauti, ilikuwa mtu akichukuliwa hatua, mwingine anatokea huko ikiwemo kwenye chama kumkingia kifua,” amesema Kangoye.

Ameshauri jamii ishiriki katika kuimarisha mawasiliano kati ya wanafunzi, walezi, wazazi na walimu ili kuyadhibiti mazingira na vyanzo vinavyosababisha ujauzito kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Fedha zinazotumiwa na Serikali kugharamia elimu ya wanafunzi hawa inatokana na kodi za wananchi, wanaume wanaofanya ngono na wanafunzi haitakiwi wafumbiwe macho,” amesema Kangoye.

Kangoye amesema ipo haja kwa kila mtu kutimiza wajibu wake unaohusisha ama kuchangia kumkinga mwanafunzi wa kike dhidi ya mimba za utotoni.

KATIBU WA CCM MPWAPWA ATOBOA SIRI

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Mpwapwa, Rukia Hassan, amesema mtindo wa maisha wa baadhi ya familia unachangia kuwapo tatizo hilo.

Amesema baadhi ya familia hasa za wafugaji na wakulima zinaishi kwa kuhamahama ili kufuata malisho ya mifugo na au mashamba.

Watoto wakiachwa nyumbani wanakosa usalama, na wanapoongozana na wazazi wao wanakuwa mbali na shule, hivyo kulazimika kutembea mwendo mrefu kufuata shule,” amesema Rukia.

Kutokana na hali hiyo, Rukia amesema baadhi ya watoto wa kike wanajikuta katika vishawishi kama msaada wa usafiri wanaopata kutoka kwa wanaume wasiokuwa waadilifu.

Pia amesema tatizo jingine ni malezi, kwani baadhi ya familia bado zinaamini katika mfumo dume, wakidhani kuwa mtoto wa kike hana haki ya kupata elimu.

Mzazi hasa wa kiume anatumia hila na kumuoza mtoto bila hata mtoto mwenyewe wala mama yake kujua, anachukua mahari ya fedha ama mifugo kwa siri kutoka kwa anayemtaka binti yake,” amesema.

Rukia amesema wazazi ama walezi wenye hulka hiyo wanajikuta mara kadhaa wakijenga mazingira ya kumkutanisha mwanafunzi wa kike na ‘mumewe’, hivyo kusababisha mimba za utotoni.

Ingawa ni hivyo, Rukia anasema wapo wanafunzi wasichana wasiokuwa na maadili mema, wanaoshindwa kufuata malezi bora kutoka kwa wazazi ama walezi wao, hivyo kuwa katika mahusiano ya kingono yanayowasababishia ujauzito.

NINI KIFANYIKE?

Amesema kwa upande wao (CCM) kwa sasa wanahimiza wazazi kupeleka watoto shuleni, huku wakihimiza uwekezaji katika   mazingira mazuri kwa watoto wa kike kuhitimu masomo katika ngazi zote.

Kwa mujibu wa Rukia, wazazi wanapaswa kuimarisha mawasiliano kati yao na shule wanakosomea watoto, ili kufahamu maendeleo ya kitaaluma na mwenendo wa tabia.

Mawasiliano ya karibu kwa pande hizo mbili, yameelezwa na Rukia kuwa yatasaidia kupunguza uwezekano wa mtoto wa kike kupata mwanya wa kuingia au kuingizwa kwenye vishawishi vinavyosababisha ujauzito.

UTAFITI WA TenMet

Mtandao wa Elimu Tanzania (TanMet), kupitia taarifa ya utafiti uliofanyika mwaka jana kwenye wilaya saba katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Mara, Morogoro na Pwani, umeeleza kuwapo tatizo hilo kama ilivyo mkoani Dodoma.

Akiwasilisha taarifa ya utafiti huo, Dk Rose Shayo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema kwa baadhi ya maeneo, wanafunzi wamebainika kuanza kujaamiana wakiwa darasa la kwanza.

Amesema lengo la utafiti huo lilikuwa kuibua masuala ya kijinsia na kuishauri Serikali juu ya hatua za kuchukua ili kupata suluhu.

Utafiti huo uliofanyika kwenye shule mbalimbali za msingi na sekondari zinazomilikiwa na Serikali, umebaini kuwa ingawa watoto wa kike wanaathiriwa na ukatili wa kijinsia na kukatishwa masomo kutokana na ujauzito, watoto wa kiume pia wapo hatarini zaidi kwa vitendo vya kulawitiwa.

Watoto hawapo salama nyumbani wala shuleni, wanafanyiwa vitendo vya ukatili kwa kiwango kisichoelezeka, ni vyema wazazi na walezi kujenga tabia ya kuzungumza nao kwa uwazi na ukweli, ili kuwajengea uwezo wa kujitambua na kujilinda,” ameeleza Dk Shayo.

 Ameshauri elimu kuhusu ukatili wa kijinsia itolewe kuanzia ngazi ya familia, kwa sababu mtoto anayefanyiwa ukatili, huishia kuwa katili.

Kwa mfano, kunapokuwa na mkutano wa kijiji au mtaa, awepo mtu wa kufundisha wazazi kuwa na ukaribu na watoto, kujihusisha na masuala yake ya shule na maisha kwa ujumla,” imeshauri sehemu ya taarifa hiyo ya utafiti huo.

You may also like