NA JAMES LANKA, MOSHI

Ukataji hovyo wa miti kwa ajili ya kuni na kuchoma mkaa unaotumika na wananchi wengi hasa wa kipato cha chini na cha kati kuwa nishati ya kupikia, unachochea uharibifu wa mazingira katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Ingawa ni hivyo, ukataji miti huo unatajwa kuwa chanzo cha mapato kwa wananchi wanaowekeza katika biashara ya nishati hiyo mkoani humo.

Lakini ukweli unabaki kuwa ukataji miti huo usiozingatia utaratibu maalumu hususani kwa ikolojia ya mimea ikiwamo miti ya asili, umegeuka kuwa mfano wa ‘mwiba kwa binadamu’ kutokana na mazingira husika kukabiliwa na hatari ya kuwa jangwa.

Serikali kupitia wadau mbalimbali wa mazingira zikiwamo asasi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, miongoni mwa hizo ni Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na asasi zisizo za kiserikali (NGOs)  zinazojihusisha na uhifadhi wa mazingira, wamekuwa mstari wa mbele katika kudhibiti uharibifu huo wa misitu na mazingira.

Muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali unaojulikana kama Tanzania Environmental Action Association (TEACA) na East Africa Economic Foundation (EACF) la nchini Poland, umedhamiria kupunguza ukataji wa miti kwa kubuni na kutekeleza mradi wa mkaa mbadala kutokea eneo la Old Moshi-Kidia.

TEACA na EACF wametumia zaidi ya shilingi milioni 300 katika kipindi cha mwaka 2016/17 kuzalisha nishati inayotokana na mkaa mbadala, ukiwa ni matokeo ya masalia ya mimea (biomass briquettes) na maranda ya mbao (saw dusts).

Makamu Mwenyekiti wa TEACA, Andoncome Mcharo, amesema mradi huo wenye lengo la kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika utunzaji wa mazingira na mkakati wa uchumi wa viwanda, utasaidia kurudisha mandhari ya kijani ya Mlima Kilimanjaro na mkoa huo kwa ujumla.

TAKATAKA

Mcharo anasema miongoni mwa malighafi zinazotumika katika utengenezaji wa mkaa mbadala ni takataka zinazozalishwa na binadamu kutoka kwenye makazi ama maeneo ya biashara.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa kubadili takataka kuwa mkaa, wameweza kuokoa uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti, na kupunguza kuzagaa kwa taka ambazo sasa zinatumika kwa uzalishaji wa mkaa mbadala.

Mcharo amesema TEACA imetanua wigo wa mradi huo kuzifikia shule 15 za msingi na tano za sekondari mkoani humo.

Mwanzilishi wa EACF, Robert Zdunczyk, amesema mradi huo utafanikisha jitihada za utunzaji mazingira na kutengeneza fursa pana za ajira hasa kwa vijana na wanawake.

Kwa mujibu wa Zdunczyk, eneo jingine la utekelezaji wa mkaa unaotokana na maranda ya mbao ni Tarakea mkoani humo, mahali palipoanzishwa kiwanda kidogo kwa ajili ya kufanikisha malengo ya mradi huo.

Amesema EACF inatekeleza miradi zaidi ya 30 katika nchi za Kenya, Burundi na Uganda kwa mwitikio mkubwa wa watu kushiriki katika utunzaji wa mazingira.

Mmoja wa wajumbe wa Bodi ya TEACA, Clemency Maro, amesema taasisi hiyo imefanikiwa kuanzisha viwanda vidogo vya kuzalisha mkaa mbadala katika maeneo tofauti ikiwamo Old Moshi, Uru Kaskazini hususani katika kijiji cha Ongoma na Tarakea.

Maro ambaye pia ni Mkurugenzi wa taasisi ya Living Centre, amewataka watumishi wa umma waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za misitu nchini, kujiweka kando dhidi ya vitendo vinavyochochea uharibifu wa mazingira.

Amesema TEACA haitegemei kuona baadhi ya viongozi wenye dhamana ya kusimamia rasilimali kama misitu, wakishindwa kutekeleza majukumu yao na badala yake wanakuwa kichocheo cha uharibifu huo.

Jamii imekuwa mstari wa mbele katika  kupanda miti na kuitunza, ingawa wapo baadhi ya viongozi wameshindwa kusimamia majukumu yao na misitu hiyo kuendelea kuteketea, na usimamizi madhubuti, jambo ambalo linawakatisha tamaa wananchi wengine, ” amesema Maro.

Mratibu wa TEACA, Elibariki Joshua Mcharo, aliwataka wananchi kuendelea kuzilinda rasilimali za misitu zilizopo na kuziendeleza kwa kuongeza upandaji wa miti kwa wingi.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa;

Baruapepe: [email protected]

Simu: +255 752 691 129.

Please follow and like us:
Pin Share