NA ALEX KAZENGA

Kitendo cha Rais John Magufuli kuagiza kuchukuliwa hatua kwa watendaji na viongozi katika maeneo ambayo shule za msingi na sekondari bado zinaendeleza tabia ya kutoza michango kwa wazazi, hata baada ya Serikali kutangaza kutoa elimu bila malipo, ni cha kuungwa mkono.

Hiyo inaonesha ni kwa kiasi gani Serikali hii ya Awamu ya Tano inavyotekeleza kwa vitendo ahadi na sera zake ilizoziahidi kipindi cha kuomba ridhaa ya kuwaongoza Watanzania.

Mbali na kuwa ni utekelezaji wa ahadi za Serikali zilizoahidiwa wakati wa kampeni zake, hatua hii inampa unafuu mzazi kumsomesha mtoto wake bila bughudha ya walimu na viongozi wengine kuomba michango kutoka kwa wazazi.

Ikumbukwe kwamba wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, moja ya ahadi za Rais Magufuli katika Ilani ya Chama anachokiongoza kwa sasa ni kutoa elimu bure kuanzia shule za awali hadi kidato cha nne.

Suala hili la elimu bure kwa miaka miwili ambayo Rais Magufuli amekaa madarakani, kabla ya kutoa kauli yake hivi karibuni lilikuwa na ukakasi kwa wazazi wengi hasa wanaosomesha watoto wao katika shule za kata.

Ilikuwapo minong’ono kwa baadhi ya wazazi wakihoji inawezekana vipi Serikali kujinasibisha kwamba inatoa elimu bure ilhali kuna michango lukuki – ya kujenga maabara, chakula, madawati na michango ya ulinzi wa shule – inayodaiwa kwa nguvu na viongozi wa shule.

Wengi kabla ya katazo la Rais walihoji Serikali inawezaje kusema inatekeleza sera ya elimu bure kwa watoto kuanzia shule za awali hadi kidato cha nne ilhali hakuna tofauti iliyopo baina ya awamu iliyopita, ambayo wazazi walikuwa wanalipa ada na michango kama kawaida.

Wakati Rais Magufuli akitoa agizo hilo la kuwakamata wale wote wanaoendeleza tabia ya kukusanya ama kuwatoza michango wazazi, alishangaa kwa nini walimu wanaendelea kutoza michango hiyo wakati Serikali inatoa Sh bilioni 23.875 kila mwezi kwa ajili ya utekelezaji wa elimu bila malipo.

Kama alivyoshangazwa na hali hiyo Rais, kuna maswali mengi tunapaswa kujiuliza. Mosi, hizo fedha zinazotolewa na Serikali kila mwezi kwa ajili ya utekelezaji wa sera ya elimu bure zinakidhi mahitaji ya shule zilizopo kwa sasa hapa nchini? Je, fedha hizo zinawafikia walengwa? Je, zinafika kwa kiwango kinachotakiwa? Au zinakwama mikononi mwa watendaji wachache?

Na ikiwa fedha hizo zinazotolewa hazitoshi; kama wahusika kabla ya kuanzisha utaratibu wa kuchangisha wazazi wamefanya mawasiliano ya kutosha na mamlaka zote zilizoanzisha utaratibu huu wa elimu bure kama Serikali ilivyoagiza?

Vilevile kama sera hii ina upungufu ambao pengo lake kuzibika kwake ni lazima michango ya wazazi ihusike katika utekelezaji wake, katika katazo hili lililotolewa na Rais kwamba michango hiyo haitakiwi tena, je, wahusika wamejipanga vipi kukabiliana na vikwazo ama changamoto zinazoweza kuibuka katika kipindi cha utekelezaji wa agizo hilo?

Rais ameonesha nia ya dhati ya kutekeleza sera ya elimu bure kwa vitendo, ni dhahiri sasa viongozi wanaohusika katika utekelezaji wa sera hii wakae chini na kutafakari kwa kina, juu ya utaratibu unaotumika kutekeleza sera hiyo bila misigano yoyote inayoweza kuibuka wakati wa utekelezaji wake.

By Jamhuri