CanavaroMatumani ya kufanya maajabu ugenini kwa upande wa Klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, yamefufuka baada ya taarifa za kitabibu kusema Nahodha wa kikosi hicho, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, atakuwa fiti kuwakabili Waarabu.


Yanga wanaotarajiwa kuondoka nchini kesho Jumatano kwenda Tunisia kurudiana na Etoile du Sahel katika mechi ya Kombe la Shirikisho, ilimkosa mchezaji huyo katika kipindi cha pili cha mechi ya kwanza iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.
Katika mchezo huo wa 16 bora uliopigwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam, libero huyo aliifungia bao timu yake katika dakika ya pili kwa mkwaju wa penalti kabla ya kuumia.


Wanachama na mashabiki wa Yanga walikuwa na hofu kwa kuwa kwake majeruhi, kutokana na umuhimu wake kikosini ikizingatiwa kuwa ndiye mfungaji wa bao pekee lililorejesha heshima ya Yanga mbele ya Waarabu, alipoitungua Al Ahly ya Misri kwenye uwanja huo mwaka jana waliposhinda 1-0.


Taarifa za kurejea dimbani zimewakuna mashabiki wa Yanga na sasa wanaamini anaweza kusaidia kuandika historia kwa kuitoa Etoile Du Sahel.


Tabibu wa Yanga, Dk. Juma Sufian, anasema mchezaji huyo anaendelea vizuri na anatarajiwa hadi kufikia mechi dhidi ya Du Sahel atakuwa fiti.
“Hadi sasa hali ya Cannavaro ni nzuri, nadhani mechi dhidi ya Polisi Morogoro Jumatatu (jana) hatacheza, lakini atakuwa tayari kwa mechi dhidi ya Etoile,” anasema Dk. Sufian.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha, anasema kwamba maandalizi ya safari ya Tunisia yanaendelea vizuri, kikosi kina morali wa ushindi na kutengeneza historia mpya kwenye ardhi ya Waarabu.

By Jamhuri