Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kimesema mpango wa kuwasaidia wanafunzi wajasiriamali kuendeleza biashara zao au kuatamia mawazo ya biashara zao utakuwa wa manufaa makubwa.

Chuo kimesema lengo la kufanya hivyo ni kutatua tatizo kubwa la ajira lililopo nchini kwa kuwafanya wahitimu wa chuo hicho waendane na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia katika nyanja za biashara na uchumi

Hayo yamesemwa jana na Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Edda Tandi Lwoga, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kozi ambazo zitaanza kufundishwa mwezi tisa.

Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Edda Tandi Lwoga, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kozi ambazo zitaanza kufundishwa mwezi  tisa

Ametaja baadhi ya kozi hizo kuwa ni Astashahada ya Msingi ya Uchumi na Fedha, Astashahada ya Msingi ya Usimamizi wa Usafirishaji, Astashahada ya Msingi ya Ujasiriamali na Ubunifu, Astashahada ya Msingi ya Uongozi wa Biashara, Usimamizi wa Kumbukumbu na Makavazi, Astashahada ya msingi ya Digital Marketing na Astashahada ya Msingi ya Masoko na Utalii .

“Katika ngazi hii tunampokea mwanafunzi ambaye amemaliza kidato cha nne na kufaulu walau masomo manne. Hapa tunaanza kumpa elimu ya Msingi katika fani husika,” amesema.

Amesema kasi inayoongezeka kila mara ya mabadiliko ya kiteknolojia katika nyanja za biashara na uchumi yamekuwa chachu kwa Chuo kuwaandaa wahitimu wanaoendana na mabadiliko hayo.

“CBE imejielekeza zaidi kusaidia katika kutoa mafunzo kwa wahitimu wenye ujuzi wa biashara kwa uchumi wa Tanzania. Chuo kinatambua kuwa maendeleo ya rasilimali watu wenye ujuzi kwa uwezeshaji wavijana, tija, na ufanisi katika jamii unategemea wakufunzi wenye ujuzi na uzoefu, na ubora wa taasisi za mafunzo,” amesema.

Profesa Tandi amesema Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kwa miaka 58 sasa kimekuwa kikitoa huduma bora katika jamii kwa kutoa elimu ya biashara kwa wajasiriamali, kutoa wahitimu wenye ujuzi kulingana na uhitaji wa soko na kutoa mafunzo na kutoa ushauri wa kitaalamu.

Amesema mambo hayo yamejikita kwenye majukumu ya msingi ya Chuo ambayo ni Kutoa Taaluma, Kufanya tafiti na Kutoa Ushauri wa Kitaalamu. Ili kuwafikia wananchi wengi Chuo kimeweka huduma hizi katika Kampasi zetu za Dar es salaam, Dodoma, Mwanza na Mbeya,” amesema .

Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Edda Tandi Lwoga, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kozi ambazo zitaanza kufundishwa mwezi  tisa Kushoto ni Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Dk. Nasibu Mramba na kulia ni Mkuu wa Uhusiano wa chuo hicho, Leonidas Tibanga

Profesa Tandi alisema ili kutoa mchango kwenye Maendeleo ya Viwanda na Biashara Katika Ukuaji wa Uchumi Endelevu Tanzania, Chuo kimekuwa kinabadili mitaala yake na kuongeza kozi mpya zinazoendana na kuendeleza Uchumi, Biashara na Maendeleo ya viwanda.

Amesema katika kukabiliana na Mfumo wa Elimu ya Juu na Kutoa Wahitimu Wasio na Ajira

Tanzania, Chuo cha Elimu ya Biashara kimekuwa kikizidi kuongeza matarajio mengi kwa wahitimu kwa kuwapatia ujuzi unaohitajika na soko la ajira ikiwa ni pamoja na wahitimu wengi kuweza kujitegemea kwa kujiajiri.

Chuo kimekuwa kikijitahidi kubadili mitaala, kubuni kozi mpya ikiwa ni pamoja na kutumia mbinu za kisasa za kufundishia.

Pia,chuo kimeanzisha mafunzo ya Uanagenzi vilevile baadhi ya wanachuo kuwa kwenye Atamizi za biashara.Mafunzo ya uanagenzi yana msingi wa mafunzo kwa vitendo kwa kushirikiana na mahali halisi pa kazi. Hapa mwanachuo hutumia nusu ya muda wake Chuoni na nusu kwa mwajiri ambapo hupata fursa ya kujifunza kwa vitendo mambo ambayo tayari amekwisha jifunza kwa nadhalia,” alisema.

By Jamhuri