Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewakabidhi wabunge wa majimbo 10 ya Mkoa wa Dar es Salaam vifaa tiba vya gharama ya shilingi Milioni 691 vilivyotolewa na serikali kwa ajili ya majimbo hayo.

Vifaa hivyo ni miongoni mwa vifaa vilivyozinduliwa wiki iliyopita na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu vilivyogharimu zaidi ya sh.bilioni 14.9 kwa ajili ya majimbo na halmashauri 214 nchi nzima.

Chalamila amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amedhamiria kumaliza vifo vinavyosababishwa na uzazi hivyo uwekezaji mkubwa unaendelea katika sekta hiyo.

Amesema mkoa umepewa zaidi ya shilingi bilioni 52 katika sekta ya afya na wanafanya maboresha ya ujenzi wa vituo vipya na kuiwezesha MSD kusambaza vifaa tiba vya kisasa katika vituo vya umma vilivyo tayari kutoa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 14.9 kununua vifaa hivi kwa ajili ya nchi nzima na MSD ndiyo imenunua na itavisambaza kwa majimbo hayo 214 nchi nzima.

By Jamhuri