Na Cresensia Kapinga , JamhuriMedia, Tunduru
 
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamhanga amesema kuwa tayari wamemaliza kufunga  mitambo ya kupooza umeme  kama sehemu ya kuboresha umeme katika maeneo ya mikoa ya Mtwara na Lindi ambayo umeme wake ulikuwa unapatika kwa njia mbili ambao unatokana na gesi na  umeme wa gridi ya Taifa.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye eneo la Pachani katika Kijiji cha Matemanga Wilayani Tunduru mkoani Ruvuma ambapo mtambo wa kuboresha umeme kutoka Songea kwenda mikoa ya Mtwara na Lindi umejengwa.
 
Amesema kuwa Mikoa ya Mtwara na Lindi umeme unapatika kwa njia mbili kuna umeme unapatikana kutoka katika kituo kidogo cha kuzalisha umeme kilichopo Mtwara kinachozalisha kwa kutumia gesi ambacho mitambo iliyokuwa pale sasa ina uwezo wa kuzalisha megawatt 31 .5 lakini hapa Tunduru tupo kwenye laini ya vorutege kilovolt 33 inayotoka Songea inatembea mpaka Tunduru na inasaidia pia kulisha baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Masasi  na Wilaya ya Nanyumbu .

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamhanga akizungumza na wahandisi wa shirika hilo mara tu baada ya ukamilishwaji wa ujenzi wa mashine za kupoza umeme wa msongo katika kijiji cha Matemanga wilayani Tunduru.


“Kimsingi kwa sababu ya hii laini ya grid ya Taifa ilikuwa haina ubora wa kutosha wa kupeleka umeme katika maeneo yale ya Masasi na Nanyumbu, na kama sehemu ya kukabiliana na changamoto hiyo ikiwa pia ni sehemu ya kutekeleza maagizo ya viongozi wetu.” amesema mhandisi Nyamhanga.
 
Amesema kufungwa kwa mashine hizo za kuboresha msongo wa umeme wataweza sasa kuboresha upatikanaji wa umeme katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Mtwara kwa maana ya Wilaya ya Masasi na Wilaya ya Nanyumbu na kwa kufanya hivyo watakuwa wamekipunguzia kituo chao cha kuzalisha umeme cha Mtwara mzigo wa megawatt 5.
 
Mikakati wanayoichukuwa TANESCO inalenga kuhakikisha kuwa upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Mtwara na Lindi inakuwa ni historia na si vinginevyo.



Baadhi ya wakazi wa vijiji vya Milonje, Kiuma, na Matemanga wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari kuhusiana na tatizo lililokuwepo la umeme walisema kuwa hatua zilizochukuliwa na shirika la umeme (TANESCO) za kuufunga mtambo wa kupooza umeme ni kitendo ambacho kitasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa kabisa matatizo yaliyokuwepo ya upatikanaji wa umeme kwa shida jambo ambalo lilikuwa tatizo kubwa kwa watumiaji wakiwemo wateja wa mashine za kuchakata nafaka pamoja na mashine za kuchakata alizeti. 
Wakazi hao Kinanda Athumani mkazi wa kijiji cha Milonje, Selemani Abdalla mkazi wa kijiji cha kiuma na Fadhili Ponera mkazi wa jiji cha Matemanga wameipongeza serikali ya jamuhuli ya muungano wa Tanzania kupitia shirika la umeme Tanzania (TANESCO) kwa kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa watanzania wote wanapata huduma bora ya umeme toka mijini hadi vijijini.
 

Mashine za kupoza umeme zilizojengwa katika kijiji cha matemanga wilayani Tunduru
Mashine za kupoza umeme kutoka Songea kwenda mikoa ya mtwara na lindo ikiwa imekamilika

By Jamhuri