Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar ea Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila  leo Novemba 20,2023 amefanya Mkutano mkubwa wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Singiziwa-Chanika jijini Dar es Salaam ambapo amesikiliza kero na kuzipatia majawabu hadi usiku.

RC Chalamila akisikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi hao amekemea tabia ovu za vijana maarufu kwa jina la Panya Road, ambazo zinahatarisha maisha ya watu na kuwafanya kuishi kwa wasiwasi.

hivyo wakati akizungumza kwenye mkutano huo  amesema hao vijana wamekuwa tishio kwa usalama wa wananchi na mali zao hivyo kutakuwa na oparesheni maalum itakayofanyika baadhi ya maeneo ambayo vijana hao hatari hutumia kama “maskani” yao lengo likiwa ni kujenga Dar es salaam na Tanzania yenye amani.

“Kutakuwa na oparesheni maalum ambayo itapita kwenye baadhi ya maeneo ambayo tunajua ndio maskani ya panyaroad iliwahi kutokea vingunguti alikuwa kibaka mmoja ambaye tulikuwa tunamuita panyaroad mwandamizi alipouliwa wenzake wakatoka huku Chanika wakaenda kufanya fujo Vingunguti kwanini mwandamizi wetu ameuliwa lakini nashukuru sana Mungu kama mapambio waliyaimba vizuri,” alisema Mhe Chalamila.

Akiendelea kusikiliza kero mbalimbali za wananchi hao Mhe. Chalamila alibaini matatizo makubwa yanayowakabili wananchi hao zikiwemo barabara, shule, huduma mbaya vituo vya afya, maji, umeme, migogoro ya ardhi, mwongozo wa soko la wamachinga, matatizo kijamii na familia huku RC Chalamila akibaini uwepo wa vitendo vya kikatili wanavyokumbana navyo watoto, ushoga na madanguro.

Aidha wananchi hao walimuomba Mkuu wa Mkoa huyo kuwasaidia kutatua kero zao sababu ni muda mrefu wanahangaika, ambapo baada ya kusikiliza kero hizo aliwataka viongozi wenye mamlaka na idara husika kujibu kero hizo sababu lengo ni kupata ufumbuzi wa kila kero.

Wakiongozwa na mkuu wa wilaya ya Ilala Mhe Edward J Mpogolo viongozi hao walitoa majibu ya baadhi kero na kuahidi kushughulikia na kutatua kero zilizohitaji ufuatiliaji zaidi.

Kwa kumalizia Chalamila alisema matatizo  na alitoa rai kwa viongozi kutembelea maeneo yao mara kwa kuepuka matatizo kuwa sugu, na aliwaasa wazazi wawe makini na makuzi ya watoto kuepuka taifa lenye vijana na viongozi wasiojielewa hapo badae ikiwa watajiingiza kwenye makundi ya panya road au ushoga.

By Jamhuri