DODOMA.

EDITHA MAJURA.

Wakati Serikali ikiendelea kuhamia Dodoma, jiji hilo limeonekana kuwa kitovu cha wahamiaji haramu, ambapo katika kipindi cha miezi mitatu zaidi ya wahamiaji haramu 70 wamekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dodoma, Peter Kundy, amesema wanafanya misako, doria na ukaguzi kwenye shule, saluni, viwanda, nyumba za kulala wageni, madukani na kwenye vyombo vya usafiri, wakati wowote.

“Baada ya serikali kuanza kuhamishia makao makuu yake hapa na manispaa kuwa Jiji, shughuli za kiuchumi zimeongezeka hivyo wengi wanakuja wakiwemo hata wasiyofuata sharia wahamiaji haramu,” amesema Kundy.

Ametoa mfano wa wahamiaji haramu 64 raia wa Ethiopia waliokamatwa Machi mwaka huu, kwenye kizuizi cha Chenene wilayani Chamwino, wamefungwa miezi mitano jela.

Adhabu hiyo imetokana na wahamiaji hao kushindwa kulipa faini ya Sh. 500,000 kwa kila mmoja, ingawa walipokamatwa walikutwa wakiwa na Sh milioni 5.4.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Giles Muroto, amesema kuwa siku tatu kabla ya kuwakamata wahamiaji hao haramu, walipata taarifa kwamba walikuwa wanatokea Holili, Tanga mpakani mwa Tanzania na Kenya, wakipitia Dodoma hadi Mbeya, wakielekea Afrika Kusini.

Wakati wahamiaji haramu wakikumbwa na adhabu bya kifungo cha miezi mitano gerezani, gari aina ya Mitsubish Fuso lililotumika kuwasafirisha limetaifishwa.

Sheria ya uhamiaji ya mwaka 2005, inatoa adhabu ya kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh 500,000 kwa wahamiaji haramu huku
wale wanaowasafirisha wakitozwa faini ya Sh milioni 20 au kifungo cha miaka 20 jela ama vyote viwili.

Katika tukio hilo, Alois Mvungi (34) mkazi wa Pasua na msaidizi wake, Emanuel Sambara (39) mkazi wa Majengo mkoani Kilimanjaro, walitiwa nguvuni wakituhumiwa kusafirisha wahamiaji haramu 64.

Katika tukio jingine wahamiaji haramu 40 raia wa Ethiopia walikamatwa Julai 4, kwenye kijiji cha Kuhi wilayani Kondoa. Afisa Uhamiaji wa Mkoa, Kundy amesema pamoja na hao, Julius Kitoma (57) ambaye alikuwa dereva wa gari lililokuwa linawasafirisha naye alikamatwa.

Mapema wiki iliyopita, Kundy, amesema walikamatwa watu 10 wakiwemo wahamiaji haramu wanane, ambao walikuwa wanashikiliwa na idara ya uhamiaji mkoani humo kwa makosa tofauti.

Watanzania, Khalid Kimbe (40) na Shineni Mwindadi (41) walishikiliwa kwa kushindwa kutoa ushirikiano kwa askari wakati wa upekuzi, raia watano wa Ethiopia na raia watatu kutoka nchini Rwanda, Burundi na Uganda walishikiliwa kwa kuingia na kuwepo nchini kinyume cha sheria.

Majina yao, umri na nchi wanazotokea kwenye mabano yametajwa kuwa ni Amuri Harerimana 44 (Rwanda), Sada Niyonkuru 38(Burundi) na Akena Thomas 35(Uganda).

Kundy, ameomba wananchi wanapotilia shaka mtu au kundi la watu kuhusu uraia na uhalali wao wa kuwepo nchini, kutoa taarifa kwa idara hiyo ya uhamiaji.

Please follow and like us:
Pin Share