Chongolo aanza ziara Morogoro,agusia migogoro ya wakulima na wafugaji

………………………………………………………….

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Daniel Chongolo ameanza ziara ya kikazi leo Januari 28 mkoani Morogoro huku akitumia nafasi hiyo kueleza sababu za kufanya ziara hiyo ndani ya mkoa huo.

Aidha amesema pamoja na mambo mengine anatambua mkoa huo unakabiriwa na changamoto ya migogoro ya ardhi hasa ya wakulima na wafugaji huku akieleza wazi kwamba ukiona kuna mgogoro wa ardhi basi katikati kuna kiongozi ambaye ameshindwa kutimiza wajibu wake.

Akizungumza na wanachama wa chama hicho pamoja na wananchi wa Wilaya ya Gairo ambako ndio ameanzia ziara yake ya siku tisa akiwa ameambatana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Sophia Mjema,Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Oganaizesheni Issa Haji Gavu, Chongolo amesema anatambua wamefanya ziara hiyo kwenye kipindi cha msimu wa kilimo.

“Tumeanza ziara katika Mkoa wa Morogoro, tunafahamu watu wengi wana shughuli za kilimo na sisi tumekuja kujifunza yale yanayoendelea kutekelezwa ndani ya Mkoa huu.Kwenye eneo la elimu kwasababu hii ni Januari ndio watoto wetu wa msingi na sekondari wanaendelea kuripoti kwenye shule zetu mbalimbali na tumeanza hapa naamini tutajifunza.

“Tunajua kwenye eneo la afya lazima tuje tujiridhishe nini kinaendelea, kwenye miundombinu ni wakati mzuri wa kuja kujifunza miundombinu ndani ya Mkoa wa Morogoro ndio maana tumekuja wakati huu ili pale ambapo wananchi wanakwama na sisi tukwame ili tujue pakurekebisha na wananchi wapiti.

“Tumekuja wakati huu kuangalia kilimo, masuala ya pembejeo na mambo yanayaohusiana na kilimo ili tujifunze na changamoto tuzibebe , tumekuja wakati huu ili tuangalie vyanzo vya maji, maeneo ambayo yanaweza kutoa maji.Tunafahamu Gairo kuna changamoto ya maji na maji yanayotumika ni ya kisima na hapa kuna mlima ambao tukitega maji tunaweza kuondoa changamoto ya upatikanaji maji, hivyo ni wajibu wetu kwenda kutafuta fedha.

“Lakini tumekuja kuangalia uhai wa Chama chetu, niko na wenzangu, tutapita sehemu zote, tutaangalia, tutajifunza na baadae tutatoa maelekezo.

“Tuko kwenye Mkoa wa Morogoro wenye changangamoto ya migogoro ya ardhi na migogoro ya ardhi ni mambo mawili tu wafugaji na wakulima, tumejifunza sana na kuangalia maeneo mengi ambayo tumeshuhudia changamoto.Ukiona changamoto ya mgogoro wa wakulima na wafugaji ujue hapo katikatika kuna kiongozi katikati atimizi wajibu wake ,kwenye ungozi kuna safu nzuri ya viongozi kuanzia ngazi ya kijiji ,kata, tarafa , mkoa na mpaka ngazi ya taifa.Hivi kuna tatizo linaweza kutoa kwenye ngazi ya kijiji serikali isijue.

“Ukiona Serikali haijui maana yake kuna mtendaji katika eneo husika ameshindwa kutimiza wajibu wake, hivyo kila mmoja akae kwenye nafasi yake matatizo yanatatulika, migogoro hii inatatulika lakini haiwezekani kwenye mgogoro kila mmoja anamuingilia mwenzake , anaingia kwenye eneo la mwenzie bila ruhusa.

“Yale yanayotakiwa maelekezo tutaelekezana na yale kuchukua na kufanyia kazi tutachukua, niwahakikishie tutatekeleza wajibu wetu ili kusiwe na maswali huko mbele ya safari,”amesema Chongolo akiwa kwenye siku yake ya kwanza ya ziara ya siku tisa ndani ya Mkoa wa Morogoro.

Kwa Upande wake Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Sophia Mjema amesema Chama cha Mapinduzi kitaendelea kuzunguuka nchi nzima kwa ajili ya Kusikiliza na Kutatua kero mbalimbali za Wananchi na kuzipatia Suluhu ya kudumu kama ili kutumiza damira njema ya Mwenyekiti wa chama hicho na Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.