Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameyataka mabaraza ya madiwani nchini kufanya kazi za kujadili maslahi ya wananchi na sio kulumbana kwa maslahi yao binafsi.

Chongolo amesema hayo jana wakati akizungumza na wanachama wa CCM katika Kijiji cha Kinole, jJmbo la Morogoro Kusini Mashariki ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku tisa mkoani Morogoro yenye lengo la kuimarisha chama na kukagua miradi ya maendeleo.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa – Itikadi na Uenezi, Ndugu Sophia Mjema,Akizungumza  na wananchi wa Kinole wakati msafara wa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo , ukiwa njiani kwenda Kata ya Tegetelo, kukagua mradi wa maji wa Morong’anya.

“Madiwani kazi yenu ni kujadili hoja zenye tija na sio kuvutana bila sababu za msingi” amesema.

Amesema amepata taarifa kutoka kwa mbunge wa jimbo hilo Hamis Tale kuwa Serikali ilipeleka fedha za Kituo cha Afya cha Kinole lakini fedha hizo ziliondolewa baada ya kutokea malumbano wapi kituo hicho kijengwe.

“Naenda kuziwekea msisitizo fedha hizo zirudishwe ndani ya miezi miwili fedha zitakuwa zimefika “amesema..

Akizungumzia elimu Chongolo amewataka wazazi katika Wilaya ya Morogoro vijijini kuacha tabia za kuwafundisha watoto mambo ya wakubwa kabla ya umri wao.

“Zamani mtoto wa kike akimaliza darasa la saba anachezwa ngoma kisha anaolewa, acheni kuwafanya watoto wa kike kama kitega uchumi kwa kutaka kupata mahari”amesema

Pia amewataka wazazi hao kuacha kuwageuza watoto kike kuwa wafanyakazi wa ndani na badala yake wawapeleke shule ili waweze kuhudumia familia zao kwa tija.

Kwa upande wa afya, katibu huyo amewataka kuacha kujitibu kwa waganga wa jadi na badala yake watumie huduma za vituo vya afya.

“Serikali imewekeza fedha nyingi katika vituo vya afya na hospitali hakuna sababu ya kwenda kutibiwa kwa waganga wa jadi”amesema.

Awali katibu wa shina namba 2 Shomari Mkude amesema katika vikao vyao vya shina hujadili kuhusu masuala ya kilimo na kumuhakikishia Chongolo wanatarajia kuvuna mazao ya kutosha ifikapo mwezi Aprili na hivyo hawatakuwa na njaa.

Pia katibu huyo wa tawi amesema wanamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea madarasa mapya ya kutosha hali itakayowafanya wanafunzi kusoma vizuri .

By Jamhuri