Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amepongeza Menejimenti na watumishi wote katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila kwa kuboresha ubora wa huduma za matibabu kwa wateja katika Hospitali hiyo.

Waziri Ummy amesema hayo leo mara baada ya kufanya ziara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila kujionea hali ya utoaji huduma ikiwa ni pamoja na kuzungumza na Menejimenti na watumishi katika Hospitali hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam.

“Ninaridhishwa na hali ya huduma katika Hospitali yetu ya Mloganzila na pia nimeongea na wagonjwa na wenyewe wamekiri kabisa kuwa huduma za hapa Mloganzila ni nzuri, hongereni sana ”amepongeza Waziri Ummy Mwalimu

Waziri Ummy amewataka wananchi kuondoa hofu iliyokuwepo hapo awali juu ya ubora wa huduma zinazotolewa katika Hospitali hiyo kuwa huduma zinazotolewa hivi sasa ni bora zaidi huku Hospitali hiyo ikiwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa wa aina zote hadi watu mashuhuri.

Waziri Ummy ameongezea kuwa Hospitali hiyo ya kisasa ipo kwenye mazingira rafiki zaidi na tulivu kwa mgonjwa kuweza kupata huduma za matibabu huku kwa sasa ikiwa na madaktari wa kutosha kutoa huduma za matibabu pamoja na vifaatiba.

Amesema kuwa kutokana na kuboreshwa kwa huduma Hospitali hiyo imeweza kuongeza idadi ya wateja waliopata huduma kutoka wagonjwa 9,595 Mwezi Julai 2022 hadi kufikia wagonjwa 13,227 Mwezi Desemba 2022 (Huduma kwa wagonjwa wa nje) huku kwa wagonjwa wa kulazwa kutoka wagonjwa 857 Mwezi Julai 2022 hadi kufikia wagonjwa 1,246 Mwezi Desemba 2022.

Aidha Waziri Ummy amepongeza uamuzi wa menejimenti kuhamishia huduma za kliniki ya wagonjwa wa Kisukari, Moyo na mishipa ya fahamu kuhamishiwa katika Hospitali ya Mloganzila hivyo kupunguza foleni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga).

Amesema kuwa uamuzi wa kuhamishia kliniki hizo katika Hospitali ya Mloganzila una manufaa kwa kuwa Hospitali hiyo ina nafasi ya kutosha na vitanda zaidi ya 500 ambavyo viko wazi hivyo kunapunguza foleni ya wagonjwa kuweza kupata huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na wagonjwa kuweza kupata huduma bora za matibabu.

Waziri Ummy Mwalimu hakisita kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohammad Janabi kwa maono na utendaji kazi wenye ufanisi katika kuboresha ubora wa huduma za afya na maendeleo ya Sekta ya Afya nchini.

Waziri Ummy amewataka watumishi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kumuunga mkono na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Prof.Janabi ili kwa pamoja tuweze kuboresha huduma za matibabu katika Hospitali hiyo.

By Jamhuri