Chongolo, Shaka wakemea uzembe

SUMBAWANGA

Na Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, ameacha maagizo mazito kwa uongozi wa Mkoa wa Rukwa baada ya kumaliza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani hapa.

Miongoni mwa maagizo hayo ni kumtaka Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti, kuunda mara moja kikosi kazi maalumu kukagua na kutathmini miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani hapa.

“Hatukuridhishwa na miradi tuliyoitembelea, hasa katika sekta ya afya inayokabiliwa na upungufu mkubwa wa dawa, wataalamu na huduma duni kwa wazee,” anasema Chongolo.

Katibu Mkuu huyo aliyekuwa ameambatana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka na sekretarieti nzima, amesema kikosi kazi hicho pia kinapaswa kukagua miradi isiyoendana na thamani ya fedha iliyotumika.

“CCM haiko tayari kuwalea viongozi na watendaji wazembe wanaoshindwa kutatua kero za wananchi na kuimarisha ustawi wao,” anasema.

Chongolo ametoa siku 14 kwa Mkirikiti kuwasilisha ofisini kwake taarifa ya utekelezaji wa maelekezo hayo kabla ya hatua kali kuchukuliwa.

Akikazia kauli hiyo, Shaka anasema kamwe CCM haitaacha kutetea masilahi ya umma au kutofuatilia ahadi zilizotolewa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mikutano mkoani hapa, Shaka anasema kamwe viongozi wazembe hawawezi kuvumiliwa.

“Iwapo Rais Samia Suluhu Hassan mwenyewe anathamini ziara hizi na anatoa maelekezo kutatua kero za wananchi, mtendaji wa kijiji ni nani hata ushindwe kuhudhuria mikutano hii?

“Ni nani atajibu hoja za wananchi kama mtendaji hayupo? Mtendaji ndiye anastahili kujibu hoja, si mwenyekiti wa halmashauri. Hili hatuwezi kulivumilia na hawa watendaji wazembe tutawatolea mfano kwa nchi nzima,” anasema. 

Shaka anasema katika mambo ambayo hayatarudi nyuma ndani ya utawala wa Rais Samia ni juu ya suala la kuguswa na changamoto za Watanzania.

“Katika hili hatuwezi kurudi nyuma kabisa kabisa. Tutahakikisha changamoto za wananchi zinatatuliwa,” anasema.

Anasema kazi ya CCM tangu enzi za TANU na ASP ni kushughulika na maisha ya watu, shida na kero zao, lakini pia kutazama kwa kina iwapo mikakati ya kimaendeleo iliyobuniwa kisera katika maeneo husika inafanyiwa utekelezaji na hatimaye utekelezaji huo utoe matokeo chanya.

“Hadi sasa havijatokea vyama vya siasa makini na mbadala wa CCM vyenye uwezo na misuli ya kushika madaraka ya utawala. Kazi ya kuendesha nchi ni nzito na ngumu mno. Kazi ya utawala si mchezo au mahali pa kufanyia majaribio kama mpo maabara. Kwa sasa kazi hii CCM inaimudu vyema chini ya Rais Samia, hivyo Watanzania waendelee kutuamini,” anasema Shaka.

Katika hatua nyingine, Chongolo amesema Sekritarieti ya CCM itawaita mawaziri wanaohusika na sekta za afya, maji, ardhi, kilimo, TAMISEMI na maliasili ili kujiridhisha juu ya mipango yao ya kutatua kero za wananchi.