Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma.

Serikali imesema inatambua na kuthamini mchango wa Chuo Kikuu huria nchini katika kuendeleza elimu kwa walala hoi, wafanyakazi ambao hawana elimu ya juu kutokana na kukosa muda wa ziada na kuahidi kushughulikia changamoto zote zinazokikabili Chuo hicho kuongeza ushawishishi.

Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma George Simbachawene ameeleza hayo Jijini hapa wakati akizungumza na jumuiya ya wahitimu wa chuo kikuu huria jijini Dodoma huku akitumia nafasi hiyo kuwashauri wafanyakazi wanaokosa muda wa kujiendeleza kielimu kujiunga na Chuo Kikuu huria nchini .

Amesema Serikali ilianzisha Chuo hicho kwa lengo la kuhakikisha kila mtanzania anapata haki ya elimu na kuweza kujiendeleza bila kikwazo chochote kile ili kutimiza ndoto za kila mmoja kufikia malengo yake.

Mbali na hayo ameeleza kuwa kuna watu wanaodharau uwepo elimu inayotolewa na Chuo Kikuu huria nchini kwa kudhani hakina hadhi na kutilia mkazo kuwa Chuo hicho ni muhimu kwani kinatengeneza wasomi wengi wenye nyadhifa za juu na ubobevu wa masuala mbalimbali unaowezesha kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii.

Akijitolea mfano Simbachawene amesema,”Wakati nataka kuwa mwanasiasa niliona elimu niliyokuwa nayo pekee haitoshi hivyo nikawa natafuta namna ya kuweza kujiendeleza na dhamira yangu ilikuwa kuwa mwanasheria ndipo nikaambiwa kuwa open university ndio sehemu pekee ninayoweza kujiendeleza bila changamoto yoyote ile.

Niliposajiliwa kozi yangu nilifanya kwa miaka tatu,kusema ukweli chuo kikuu huria kimekuja kutusaidia viongozi na walala hoi na hii leo kupitia chuo kikuu huria mimi ni wakili na mambo mengine yakiisha naweza kurudi kwenye taaluma yangu”amesema

Akielezea uzuri wa chuo hicho Waziri huyo amesema,”Uzuri wa Chuo hiki,kila mmoja ni mwalimu wa mwenzake na aliyesoma chuo kikuu huria huwezi kumfananisha na mtu mwingine yeyote sababu huku unafundishwa kujitegemea kwa kutafuta material na mazingira hayo hayo ndio unayokutana nayo kazini hivyo inatengeneza viongozi imara zaidi” amesisitiza .

Kwa upande wake Mbunge wa Singida mjini Musa Sima ambaye pia ni mhitimu wa Chuo hicho kwenye masuala ya uongozi na utawala bora amesema taaluma inayotolewa na chuo kikuu huria ni taaluma bora kwani yeye binafsi
amenufaika .

“Chuo hiki kimekuwa msaada kwangu na watanzania wengi,faida yake ni kuwa unaendelea na kazi huku unasoma, nawashauri watanzania wenzangu mlioko makazini msome kupitia Chuo hiki kwani Maisha yanahitaji taaluma ya ziada na hutaipata sehemu nyingine zaidi ya hapa,”amesisitiza Mbunge huyo.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya chama cha wahitimu wa chuo kikuu huria Tanzania Almas Maige Mbunge wa jimbo la Tabora kaskazini Uyui amesema kuwa mkutano huo ni muendelezo wa majadiliano yenye chachu ya kuboresha Chuo hicho.

Amesema chuo kinapata namna bora ya kihakikisha kila mwanachama anachangia kwa namna yoyote ile iwe kifedha au kwenye miundombinu bora ili kuhakikisha chuo kikuu huria kinakuwa bora zaidi na kuwafikia watu wote ndani na nje ya nchi pamoja na kukidhi soko la ajira.

“Tunatambua kwamba wahitimu wengi ni wawekezaji na nilazima kujadiliana ni namna gani ya kutatua changamoto ya ajira ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na maisha mazuri, tunatambua kwamba wahitimu kutoka chuo kikuu huria wengi wanakuwa tayari wameshaajiriwa ni wachache ndio huwa bado wanakuwa wanasoma huku hawana ajira mpaka kumaliza,”Amesema.

By Jamhuri