Na Mwamvua Mwinyi,JamhuiMedia, Pwani

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Chalinze Islamic Modern, Bagamoyo mkoani Pwani, meiomba Serikali kuelekeza nguvu katika ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi kuanzia elimu ya msingi ili kuwapa uelewa wa masomo ya sayansi kwa vitendo .

Wameeleza, zipo shule za msingi ambazo zina wanafunzi wenye uwezo wa kufanya sayansi ya vitendo changamoto ikiwa ni ukosefu wa vifaa.

Ushauri huo umetolewa na wanafunzi wa darasa la sita katika shule Msingi Chalinze , Islamic Modern baada ya wanafunzi hao kumfanyia upasuaji mnyama Sungura na kumrejesha hai.

Wanafunzi hao wameeleza,licha ya masomo ya kawaida pia wanapatiwa mafunzo ya sayansi, na kwamba tukio la hilo ni kiumbe wa tatu kumfanyia upasuaji huo.

Wanafunzi Lattifa Bakari na Mussa Swed wa darasa la sita wameeleza, Tanzania ina uhaba wa madaktari bingwa hivyo kwa kuandaa wanafunzi wa sayansi kuanzia ngazi ya msingi itakuwa na uwekezaji mkubwa wa kizazi cha madaktari hao.

Nae Mwalimu Mkuu Seif Hashimu ameeleza ,shule yao imeamua kuwapatia masomo ya sayansi wanafunzi wao kwa lengo la kuwajengea uwezo ili waendapo sekondari wasiwe wageni kwenye somo hilo.

By Jamhuri