Na Mwamvua Mwinyi , JamhuriMedia, Pwani

Uwepo wa vifaa mbalimbali vya michezo katika shule mbalimbali utasaidia kuchagiza kuendelea kwa somo la michezo sanjali na kuibua vipaji vichanga mashuleni.

Akipokea vifaa vya michezo-mipira 1,000 iliyokabidhiwa na Chama Cha Soka mkoani Pwani, (COREFA) kwa ajili ya matumizi kwenye shule za mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani alhaj Abubakar Kunenge ameeleza, uhitaji ni mkubwa wa vifaa hivyo vimekuja wakati muafaka.

Alieleza ,michezo ni ajira na wanamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwekeza kwenye michezo ambapo matunda yanaonekana kwani soka limekuwa na hamasa kubwa nchini.

“Nimeelezwa kwamba Serikali iliteua jumla ya shule 56 za michezo Tanzania ambapo kila Mkoa unawakilishwa na shule mbili na kwa mkoa wa Pwani shule zilizoteuliwa ni Zogowale Sekondari iliyopo Kibaha na Utete Sekondari Wilayani Rufiji” amesema.

Kunenge alieleza, Mkoa uliteua shule nyingine 20 kwa uwiano wa shule zisizopungua 2 katika kila Halmashauri ambazo zitakuwa na vitalu vya michezo vya Mkoa.

“Hivyo hadi sasa Mkoa una jumla ya shule 22 zilizoteuliwa kwa ajili ya kufundisha michezo yote na kuendeleza vipaji vya wanamichezo”.

“Leo napokea vifaa vya michezo ikiwemo mipira ya mguu 1,000 na tutaigawa katika shule zilizopo ndani ya mkoa wa Pwani na tunaishukuru COREFA kwa kutupatia mipira hii ambayo itasaidia katika utekelezaji wa michezo kwenye mkoa wetu” alifafanua Kunenge.

Hata hivyo,aliwataka maofisa elimu wa Wilaya za Mkoa huo kuhakikisha vipindi vya michezo vinazingatiwa kama yalivyo masomo mengine

Vilevile alielezea, Serikali ya Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inasimamia uendelezaji na uboreshaji wa miundombinu ya michezo iliyopo ndani ya mkoa sanjali na maeneo yaliyotengwa kwa ajili michezo ili kuhakikisha hayavamiwi kubadilishwa matumizi.

Akikabidhi mipira hiyo Mwenyekiti wa COREFA Robert Munis alisema kuwa mipira imetolewa na Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kwa lengo la kuendeleza soka la vijana .

Munis alielezea kwamba, iwe chachu kwa wachezaji wachanga ili waje kuwa wachezaji bora watakaoiletea nchi sifa.

Anasema ili vipaji viweze kuonekana lazima kuwe na msingi wa wachezaji kuanzia chini ili wakue kwenye mazingira ya uchezaji kwa kuwa na vifaa vya michezo.

Katibu Tawala wa Mkoa huo, Rashid Mchatta akiwakabidhi mipira maofisa elimu wa Wilaya alisema , itasaidia kwa ajili ya wachezaji wanafunzi wakati wakishiriki michezo kwa shule za msingi (UMITASHUMTA) na sekondari (UMISSETA).

By Jamhuri