Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma.

Kamati ya utendaji ya Chama cha Walimu Tanzania CWT)Taifa,imeazimia kwa pamoja kuweka zuio kwa Katibu Mkuu wa Chama hicho Japhet Maganga kuendesha shughuli zozote za Chama hicho hasa katika masuala ya fedha na utawala.

Hatua hiyo ni kufuatia kuwepo kwa madai ya uongozi wa Juu kuvunja Katiba ya CWT hivyo Kamati hiyo kuelekeza shughuli zote za CWT kufanywa na Naibu Katibu Mkuu Joseph Msalaba.

Maazimio hayo yamefanywa na Wajumbe wa Kamati 18 toka mikoa 18 nchini ambapo wametoa maazimio hayo jana Jijini hapa.

Wakiongea mbele ya Waandishi wa Habari mara baada ya kukutana katika ofisi za chama hicho,wamesema wamejiridhisha kuwa uongozi uliopo madarakani unavunja Katiba na kanuni zake.

Akizungumza kwa niaba ya wengine Mwenyekiti wa muda wa kikao hicho ambaye pia ni mjumbe wa Kamati hiyo na mwakilishi wa walimu wa Mkoa wa Njombe Mwl.Tobias Sanga alisema kikao hicho kimeridhia kumzuia Katibu Mkuu wa CWT kutoendesha shughuli za Chama hicho Kutokana na uonevu anaoufanya kwa wanachama wake.

Amefafanua kuwa moja ya ajenda ya kikao hicho ni uhamisho holela wa wafanyakazi, kuhusu matumizi holela ya michango ya walimu pamoja kutaka mkutano Mkuu wa dharula bila mafanikio .

“Tumejiridhisha na tumeona utendaji kazi wa Katibu huyu hauko sawa,tumepitia miongozo yetu tumejiridhisha,tunachukizwa kuona fedha za 2% za walimu zinatumika bila utaratibu,tukihoji hatupewi Ushirikiano,”alisema Mwalimu huyo.

Pamoja na mambo mengine Sanga amesema,”Kwa Mamlaka tuliyonayo tumekubaliana kazi zetu zitafanywa na Naibu Katibu mkuu ambaye atasimamia masuala yote ya utawala na fedha,”alisisitiza.

Alifafanua kuwa,”Naomba nieleweke wazi kuwa hatuna shida na Katibu Mkuu ila tunachotaka ni mfumo wa utendaji,tunataka walimu tunao wawakilisha wapate haki zao na sio unyanyasaji unaoendelea,”amesema

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CWT-Taifa Joseph Msalaba ambaye ndiye amepewa Mamlaka ya utendaji amesema kuwa amelipokea suala hilo na kueleza kuwa kikao hicho kimefanyika kwa amani kama ilivyotarajiwa.

Alisema “nimepokea uwepo wa ujio wa Wajumbe hawa 18 wa Kamati ya utendaji Taifa japo walitakiwa kuwa 38 lakini hakuna kilicho haribika,”amesema

Naye Mwalimu Sabina Lipukila ambaye ni mwakilishi wa walimu wa Ruvuma alisema mgogoro uliopo unasababisha utendaji kazi wa walimu kushuka na kusisitiza kuwa kwa ujumla Katiba yao haiendi wanavyotaka.

Alisema uhamisho wa Makatibu unafanywa kiholela bila wao kushirikishwa na kueleza kuwa jambo hilo linashusha ari ya kufanya kazi kwa weledi Kutokana na hofu ya uhamisho.

“Hakuna asiyefahamu kuwa sisi ni chombo cha ajira,kuna vitu vingi tunavifuatilia haviendi sawa,kwa muda mrefu sasa tumekuwa tunaomba kikao lakini tumenyimwa,tungekubaliwa vikao haya yote tungezungumza na kuyamaliza kule,”amefafanua.

Hata hivyo gazeti hili limeshuhudia baadhi ya Wajumbe hao wa Kamati ya utendaji majira ya asubhi kuanzia saa mbili kwenye ofisi za CWT Taifa wakizuiwa kuingia ndani na Walinzi katika Ofisi za CWT Taifa na kuzuiwa kwa madai ni maelekezo toka uongozi wa juu.

Aidha jambo hilo limezua sintofahamu kati ya wajumbe hao na ulinzi na kupelekea kukaa nje Kwa masaa sita kabla ya kuruhusiwa kuingia ndani ya uwanja wa Ofisi za Chama hicho na kufanikiwa kufanya kikao nje ya Ofisi jambo waliloliita kuwa ni unyanyasaji na uvunjifu wa Katika ya CWT.

By Jamhuri