CHALINZE

Na Mwandishi Wetu

Miundombinu inatajwa kuwa na umuhimu mkubwa katika kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa, ikifananishwa na mishipa ya damu katika mwili wa binadamu.

Barabara na madaraja ndiyo hasa vitu vinavyoyagusa moja kwa moja maisha ya mwananchi wa hali ya juu hadi wa kawaida kabisa, kwa kuwa hutumiwa na wote.

Katika kulifamu hilo, serikali imekuwa ikiimarisha madaraja na barabara na katika miaka ya karibuni kumekuwa na ujenzi wa madaraja makubwa na ya kisasa.

Miongoni mwa madaraja hayo ni Daraja la Mto Wami ambalo ni alama ya kujivunia hasa wakati huu tunaposherehekea miaka 58 ya Muungano.

Ama, taarifa kwamba daraja hili litaanza kazi Juni mwaka huu, ni za kuvutia kwelikweli hasa, kwa kuwa hiki ni kiungo cha miaka mingi ya uchumi wa upande wa kaskazini mwa Tanzania unaosifika kwa utalii na kuchangia fedha nyingi katika pato la taifa.

Kwamba daraja la awali limechakaa na kupitwa na wakati, hili kila mtu analiona na sasa daraja jipya linakuja na matumaini mapya ya ile Tanzania tunayoitamani.

Ujenzi wa Daraja la Wami

Daraja la Wami lenye urefu wa mita 88.75 lililoko Mkoa wa Pwani lilijengwa mwaka 1959. Daraja hili ni kiungo muhimu kutoka Chalinze kwenda mikoa ya kaskazini mwa nchi yetu na nchi za jirani.

Kwa sasa daraja hili halikidhi mahitaji ya magari yanayopita kwa kuwa lilijengwa kabla ya Uhuru, ni jembamba, lenye njia moja tu. 

Vilevile barabara zinazounganisha daraja hili ziko kwenye miinuko mikali na kona mbaya, hivyo kusababisha ajali za mara kwa mara na hata vifo.

Kutokana na uwezo mdogo wa daraja unaotokana na ongezeko la magari yanayopita na kwa kuzingatia umuhimu wa daraja hili katika usafirishaji na kukuza uchumi wa nchi, serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) walifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kazi hiyo ilikamilika Machi 2016.

Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 510 na upana wa mita 11.85 linajengwa umbali wa mita 670 pembeni mwa  daraja la zamani kwenye uelekeo wa Mto Wami. 

Upana wa daraja hili umezingatia sehemu ya barabara ya magari, watembea kwa miguu pamoja na vizuizi kwa ajili ya usalama. 

Ujenzi huu unajumuisha ujenzi wa barabara za maingilio ya daraja kwa pande zote mbili zenye jumla ya urefu wa kilomita 3.8 (km 2.1 kwa upande wa Chalinze na km 1.7 kwa upande wa Segera wa daraja) ili kuunganisha daraja jipya na barabara kuu ya Chalinze – Segera.

Mkandarasi Power Construction Corporation of China Ltd kutoka China alisaini mkataba wa ujenzi wa daraja jipya Juni 28, 2018 kwa gharama ya Sh 67,779,453,717.00 pasipo Kodi ya Ongezeko la Thamani. 

Mkandarasi alianza kazi Oktoba 22, 2018 na anatarajiwa kukamilisha mradi Novemba 21, 2022 (ingawa ameombwa kukamilisha Juni mwaka huu). Ujenzi huu unagharamiwa na fedha za Serikali Kuu kwa asilimia 100. 

Kazi ya ujenzi inasimamiwa na kampuni mbili; ILSHIN Engineers & Consultant Co. Ltd (ya Korea Kusini) na Advanced Engineering Solutions Limited (ya Tanzania) kwa gharama ya Sh bilioni 6.307.

Maendeleo ya kazi

Kazi ya ujenzi wa misingi ya nguzo za daraja imekamilika kwa asilimia 100; ujenzi wa kuta mbili za mwanzo na mwisho wa daraja umekamilika kwa asilimia 100.

Ujenzi wa nguzo zote nne za daraja umekamilika kwa asilimia 100; ujenzi wa muundo wa juu wa daraja (yatakapopita magari) ulianza kwa nguzo zote nne na kukamilika kwa urefu wa mita 511 kati ya mita 513.5 sawa na asilimia 99 ya urefu wote. 

Nguzo namba moja;  vipande 18, nguzo namba mbili; vipande 18, nguzo namba tatu; vipande 18 na nguzo namba nne ni vipande 18.

Ujenzi wa kingo za pembeni ya daraja umeanza kwa sehemu kati ya kuta ya daraja namba 1 na nguzo namba 1 na kuta ya daraja namba 2 na nguzo namba 4. Hadi sasa urefu wa kingo za pembeni uliokamilika ni mita 207 sawa na asilimia 20 ya urefu wote.

Ujenzi wa barabara unganishi

Barabara unganishi zimekwisha kufanyiwa usafishaji na ufukuaji kwa asilimia 100. (Kilometa 3.41 kwa ujumla).

Kazi ya kukata milima ili kupata usawa wa barabara imekamilika kwa asilimia 100 (kilomita 1.23) kwa pande zote za daraja; ujenzi wa makalavati mstatili matatu na makalavati mduara saba umekamilika kwa asilimia 100.

Kazi ya kujaza udongo kwa tabaka la kawaida (G3) na tabaka lililoboreshwa (G15) kufikia usawa wa barabara imekamilika kwa asilimia 99; ujenzi wa safu ya mchanganyiko wa udongo na saruji unaendelea kwa pande zote mbili za barabara unganishi (Chalinze na Segera) na kukamilika kwa kilomita 2.44 kati ya kilomita 3.815 sawa na asilimia 64.

Maendeleo ya kazi yaliyofikiwa

Kwa ujumla maendeleo ya mradi yaliyofikiwa mpaka sasa ni asilimia 76.7. Na muda wa mradi uliopita mpaka sasa ni takriban miezi 41 kati ya miezi 49.37 ya muda wa mradi.

Hadi sasa mkandarasi amelipwa asilimia 15 ya malipo ya awali kiasi cha Sh bilioni 10.17 kulingana na matakwa ya kimkataba. Mkandarasi amekwisha kuwasilisha hati kumi na tano za malipo yatokanayo na kazi alizokwisha kufanya za jumla ya Sh bilioni 33.048 sawa na asilimia 48.7.

Mhandisi – Mshauri amekwisha kuomba malipo ya miezi 35 yenye jumla ya Sh bilioni 4.570 sawa na asilimia 72.5 ya fedha za usimamizi.

Faida za mradi

Mradi umesaidia kutengeneza ajira kwa wenyeji na vipato kwa familia moja moja.

Malighafi za mradi, kwa mfano mchanga, kokoto, saruji pamoja na nondo zimenunuliwa nchini na kuchangia pato la taifa.

Mradi unategemewa kupunguza ajali kwa kiasi kikubwa kutokana na kwamba daraja la zamani lilikuwa na njia moja ila daraja la sasa litakuwa na njia mbili. Pia miinuko mikali haitakuwapo. Hii itasaidia kupunguza muda wa kusafiri na gharama za matibabu zitokanazo na ajali.

Mradi umesaidia wataalamu wazawa kuongeza ujuzi kutokana na teknolojia mpya ya ujenzi wa daraja hili ambayo kwa hapa nchini bado yapo machache.

Waziri Mbarawa azungumza

Akizungumza katika ziara aliyoifanya darajani hapo wiki iliyopita, pamoja na mambo mengine, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, anasema:

“Mkandarasi alianza kazi Oktoba 22, 2018. Muda wa utekelezaji wa mradi huu ni miaka minne, ambapo utakamilika Novemba mwaka huu. Hadi kufikia Machi 31, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 77.

“Baada ya maelezo yaliyotangulia, mimi niseme yafuatayo: “Kwanza, mkandarasi aongeze bidii zaidi na ahakikishe anakamilisha kazi hii ndani ya muda uliopangwa, kwa kufanya kazi usiku na mchana, kuongeza rasilimali watu na mitambo.

“Pili, TANROADS na Mhandisi-Mshauri simamieni kazi hii kwa weledi na utaalamu mlio nao ili iweze kukamilika katika viwango vya ubora unaotakiwa kulingana na mkataba.

“Tatu, serikali itaendelea kuwalipa Mkandarasi na Mhandisi-Mshauri kulingana na madai yanayowasilishwa na kuthibitishwa.”

Waziri amewaomba wahusika kukamilisha kazi ifikapo Juni mwaka huu, akiahidi kutembelea tena eneo hilo; ombi linaloelekea kukubaliwa na kuna kila dalili kwamba daraja hilo litakuwa tayari muda huo.

By Jamhuri