Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

MAMALAKA ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya (DCEA) kupitia oparesheni zake mbalimbali imebaini watoto wengi waliocha shule na waliotelekezwa mitaani ndiyo wengi wanaotumika kwenye magendo ya kusafirisha dawa za kulevya kwenye maeneo mbalimbali jambo linalotajwa kuwaweka kwenye hatari ya uraibu.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo,Aretas Lyimo ameeleza hayo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wao katika wiki ya sheria nchini na kuongeza kuwa wiki hiyo ina lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu dawa za kulevya.

Amesema kuna oparesheni mbalimbali zinazofanywa na mamlaka hiyo ambapo wamebaini pia watoto wengi hasa wale walioacha shule wanaotelekezwa mitaani ndiyo wengi wanaotumika katika usafirishaji wa dawa za kulevya nchini na maeneo mbalimbali.

“Wafanya biashara hiyo haramu huwatumia watoto kwa kuwalaghai na zawadi na hatimaye kuwapa dawa za kulevya na kwenye mabegi ya shule na wakati mwingine wanameza na wengine wanawatumia kuwabebesha dawa za kulevya kupeleka maeneno mbalimbali kutokana na kwamba wakiamini wale watoto hawawezi wakagundulika mapema”amesema.

Amesema, “Nitoe wito kwa watoto na jamii inayowahusisha wamba tukiwakamata unajihusisha na dawa za kulevya unazalisha, unasafirisha,unauza,unatumia sheria yao inaweza ikakufunga hadi kifungo cha maisha gerezani hivyo ndiyo maana wapo katika wiki ya sheria kwasababu mahakama ni mdau wao mkubwa katika mnyororo mzima wa haki jinai.

Amesema kwa kushirikiana na mahakama na taasisi zote za haki jinai watahakikisha wanatoa elimu kwa wananchi juu ya sheria za udhibiti wa dawa za kulevya ili waweze kujiepusha na biashara ya dawa za kulevya.

“Baada ya kubaini suala hilo sasa hivi tupo tunashirikiana na jeshi la polisi katika kuhakikisha kwamba tunatoa elimu vijijini,mitaani kupitia kwa familia ili kuhakikisha kwamba wazazi walee watoto wao na watambue tabia za watoto wao mapema ili wasishiriki katika biashara ya dawa za kulevya lakini pia wahakikishe kwamba wanalinda watoto wao wasije wakatumika katika kushiriki dawa za kulevya, “amesema.

Ameeleza kuwa katika hizo dawa za kulevya ambazo mtu hutakiwa kumeza wakati mwingine ukishameza lazima uonje kidogo ili uweze kumudu kubeba zile dawa muda mrefu ambapo mwisho wake yule mtoto ambaye anatumika katika kubeba dawa za kulevya na yeye anakuja kuwa mtumiaji wa dawa za kulevya anakuja kuwa mraibu wa dawa za kulevya kwahiyo tatizo la dawa za kulevya linaendelea kuongezeka.

Amesema wazazi,viongozi wa dini na jamii kwa ujumla wanapaswa kushirikiana kubaini mitandao ya dawa za kulevya za heroine,kokeini pamoja na methamphetamine na wale wakulima wakubwa wa mashambani wenye bangi pamoja na mirungi.

“Orodha tuliyonayo sasa hivi kuacha na hii mitandao ambayo tushaikamata,tumebaini wengi wao pia wanafanya hii biashara kwa rimoti wao wenyewe hawafanyi hiyo biashara wanawatumia watu wengine na wote tumeshawatambua tunayo orodha yao na wale wanaotumiwa pia tunayo orodha yao, “amesema na kuongeza;

“Tutaendelea kufanya oparesheni kuwakamata kuanzia sasa hivi tutawaunganisha pia na hao wanaofanya biashara kwa rimoti tunawajua na wengine wanabiashara zao kubwa tutahakikisha kwamba tuwaonye waache hiyo biashara mwisho wq siku tutawakamata na mwisho wa siku watadhalilika kwahiyo wahakikishe wanatafuta biashara halali,”amesema.

Naye Mkaguzi msaidizi wa polisi Verediana Mlimba kutoka jeshi la polisi Tanzania amesema kuwa Jeshi la polisi limeweka mikakati mbalimbali ambayo kwa kiwango kikubwa kinawasaidia kuwafikia jamii kwa ujumla mkakati wa kwanza ambao wanashirikiana na DCEA kupitia Mradi wa usalama wetu kwanza ambao unalenga zaidi watoto ambao wapo mashuleni,kuanzia shule ya masingi sekondari na Vyuo .

Amesema pia wanashiriki kuthibiti utoro kwa sababu wamegundua kwamba utoro ni zao la uharifu wanajificha kwenye makorongo wanatekwa na kuvutishwa bangi,kubebeshwa ama wao kulawitiwa.

“Tulianza kwanza kukemea tulitengeneza kwanza pembe tatu kati ya polisi,mwalimu na mzazi ili kuthibiti utoro halafu tunawapa elimu wao kukataa kuwa wasambazaji kwa nanma yoyote ile kwamaana abebe mzigo kama mtu anampatia ajue amebeba nini na asipojua leo amebeba nini kupeleka wapi basi atoe taarifa kwa mwalimu rafiki ambao ni programu za shule za msingi ama sekondari atoe taarifa leo nilibeba kitu fulani kupeleka sehemu fulani na sikijui ili tuweze kufanya ufuatiliaji alibeba nini na zaidi tunawambia hata kwakutokujua hakikisha unatoa taarifa zote,”amesema.

Amesema wanashirikiana na DCEA katika kutambua biashara na kazi zinazofanyika katika maeneo ya shule kwasababu shule zimezungukwa na wajasiriamali wengi hasa zile ambazo hazina uzio .