Dk. Mpango alikoroga

*Atoa maagizo nje ya mipaka ya Makamu wa Rais kikatiba

*Wataalamu wasema kisheria hapaswi kusimamisha kazi watendaji

*Warejea tamko la trilioni 2, wataka amheshimu Rais Samia

*Wamtahadharisha asitoe matamko ya kiserikali akiwa kanisani

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, anatajwa kuzua mgogoro wa chini chini serikalini kutokana na tabia yake ya kujiona ana mamlaka ya kutoa maagizo, ikiwamo kuwasimamisha kazi watendaji, suala ambalo anavunja Katiba ya nchi, JAMHURI limeambiwa.

Uamuzi wa Dk. Mpango kumwagiza Naibu Waziri wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk. Festo Dugange, kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, Hamis Dambaya, kwa alichodai ni matumizi mabaya ya Sh bilioni 2.2 kujenga Stendi ya Wilaya ya Nanyumbu, umeibua hisia kuwa huenda Dk. Mpango hajui mipaka ya madaraka yake.

“Kwanza tunafahamu kwa nini ametoa maagizo haya ya Nanyumbu kumsimamisha kazi mkurugenzi. Tunaufahamu mgogoro wa kimasilahi uliokuwapo muda mrefu kati ya Mkuu wa Wilaya (DC) na Mkurugenzi Mtendaji (DED) kwa miaka zaidi ya minne.

“DC alikuwa anaagiza vitu vilivyo nje ya matakwa ya kisheria, na DED akawa anavikataa. Ikawa anaandika barua kwa Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais, kwa Makamu wa Rais, kwa Mkuu wa Mkoa, lakini kila wakichunguza wanakuta ni uzushi.

“Kilichotokea zamu hii, aliyekuwa DC na Makamu wa Rais wanatokea mkoa mmoja, hivyo wametumia dhana ya ‘wa nyumbani – home boy’. Wamepeana barua, ambazo zipo sehemu nyingi tu, Makamu akaenda pale bila kufanya uchunguzi japo kidogo, akamlipua DED.

“Najua anaweza kuibuka akasema Mama (Rais Samia) alimwomba amsaidie katika eneo la ukusanyaji mapato, hivyo anaweza kujitetea kuwa alikuwa anasimamia matumizi. Huu si utetezi. Kwanza, DED yuko TAMISEMI, Katiba haimpi mamlaka ya kusimamia watumishi wa TAMISEMI, ingawa anaonekana ana hamu sana ya kusimamia watumishi. Pengine ana malengo marefu ya siku zijazo, ila hii haikubaliki.

“Lakini pia, suala kama DED ameiba fedha au la, hilo ni suala jingine. Makamu wa Rais Dk. Mpango hajui mipaka yake kimamlaka. Yeye ni sawa na tairi ya spea kwenye gari. Anafanya kazi pale tu Rais anapokuwa hayupo au kwa maelekezo ya Rais. Katiba iko wazi, anapaswa kusimamia masuala ya Muungano na si kutoa maagizo katika maeneo nje ya hapo.

“Anachofanya sasa ni kuonyesha kuwa yeye anadhani ndiye Rais wa Tanzania, hapana. Aache hizo. Hii haikubaliki. Mama Samia ndiye Rais. Ndiye anateua na ndiye mwenye mamlaka ya kutoa maagizo. Mama amekuwa Makamu wa Rais kwa miaka zaidi ya mitano, lakini hakupata kutoa maagizo ya aina hii.

“Tulimsikia mara kadhaa, alipokuwa mikoani, kila alipokutana na yaliyopinda, alisema ‘nimeyasikia, nimeyapokea ninayapeleka kwenye mamlaka ya uteuzi.’ Kwa miaka yote zaidi ya mitano aliyokuwa Makamu wa Rais, hakupata kutoa maagizo,” amesema waziri mwandamizi mstaafu, ambaye aliomba kwa sasa asitajwe gazetini.

Ameongeza kuwa watu wenye tabia za aina hii wanaweza kufikia hatua ya kwenda hata kwa mabosi wao wakadai hawapewi kazi muhimu za kufanya, hivyo wakashinikiza kufanya kazi za mabosi wao.

Waziri huyo amesema yeye ameshuhudia Makamu wa Rais akina Mzee Ali Hassan Mwinyi, Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba, Dk. Omary Ali Juma, Dk. Ali Mohamed Shein, Mama Samia Suluhu Hassan (ambaye sasa ni Rais wa Tanzania), “lakini hawa wote walikuwa watiifu na wanyenyekevu kwa marais wao. Hawakuwa wakitoa maelekezo na maagizo hadharani. Ikiwa Dk. Mpango hajifunzi, basi afundishwe aina ya nafasi aliyonayo.

“Aache mara moja kutoa matamko na kuwasimamisha kazi watumishi wa umma, ataitia hasara serikali watu wakienda mahakamani, si eneo lake hili. Ajifunze utawala bora na utawala wa sheria.”

Wakati anamsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Nanyumbu, Makamu wa Rais Dk. Mpango alisema: “Unajua vitu vingine mkurugenzi… ukiona huwezi kazi, Awamu hii ya Sita, jiondoe mwenyewe.” Dk. Mpango alitoa kauli hiyo kisha akamwagiza naibu waziri amsimamishe kazi.

Kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 47 (1), Makamu wa Rais ana majukumu yafuatayo kisheria: “47.-(1) Kutakuwa na Makamu wa Rais ambaye atakuwa ndiye Msaidizi Mkuu wa Rais kuhusu mambo yote ya Jamhuri ya Muungano kwa jumla, na hususan – (a) atamsaidia Rais katika kufuatilia utekelezaji wa siku hata siku za Mambo ya Muungano; (b) atafanya kazi zote atakazoagizwa na Rais; (c) atafanya kazi zote za Rais kama Rais hayuko kazini au yuko nje ya nchi.”

Mwanasheria aliyeomba asitajwe gazetini kwa maelezo kuwa ana mgongano wa kimasilahi, amesema: “Si unaiona Katiba? Kuanzia pale neno hususan, kisheria ina maana inamuondoa katika maeneo mengine. Ndiyo maana Watangulizi wa Dk. Mpango wote kama Makamu wa Rais ulikuwa unawasikia kwenye masuala ya Muungano tu, si matamko wala kutumbua watu.

“Hii ilifanywa makusudi kuepusha mgongano. Mtu ambaye hukumteua, hata ile kuagiza tu, kwamba wamchunguze ni kwenda kinyume cha sheria. Alipaswa kusema amepata malalamiko, atayafikisha kwa mamlaka ya utezi kama alivyokuwa anafanya Mama Samia kwa Rais [hayati John] Magufuli.”

Mbunge mmoja ambaye amefanya kazi na Dk. Mpango kwa muda mrefu, amesema ukimya wa Dk. Mpango una siri kubwa ndani yake. “Unajua watu wanamwona ni mpole, ila yule Dk. Mpango ni mgumu kufanya naye kazi. Huwa hapokei simu, hata ukituma meseji hajibu. Huwa anaamini yeye yuko sahihi muda wote. Kwa hiyo mimi simshangai kwa haya anayofanya.

“Na usishangae hata hii habari mkiiandika kuwa anavunja Katiba atashupaza shingo, ataleta ubishi wa asili ya kwao, akisisitiza yuko sahihi. Inabidi Rais Samia amwambie kuwa anavuka mipaka ya mamlaka yake, vinginevyo ataleta shida kubwa serikalini.

“Mfano ile siku anaapishwa alipoagiza Wizara ya Fedha ikusanye Sh trilioni 2 kwa mwezi, kama Rais Samia asingekataa kodi za damu palepale, leo biashara zote zingekuwa zimefungwa. Kumbuka huyu ndiye alikuwa anamwambia Rais Magufuli kuwa wanaofunga biashara ni wapiga dili. Anapaswa kusoma alama za nyakati, amheshimu Rais Samia, asitoe matamko, akiona kero aiwasilishe kwa Rais Samia, basi.”

Wakati anaagiza Dambaya asimamishwe kazi kupisha uchunguzi, Dk. Mpango alisema stendi ya Nanyumbu mpya iliyojengwa haina thamani ya Sh bilioni 2.2, hivyo akataka ufanyike uchunguzi wa kina dhidi ya Dambaya na waliohusika katika ujenzi huo.

“Hiyo si kazi ya Makamu wa Rais. Makamu hana mamlaka ya kuteua wala kutengua. Anachopaswa kufanya akiona kuna upungufu, ni kurudi na kumshauri Rais,” anasema Peter Madeleka, Wakili wa Mahakama Kuu.

Wakili Madeleka anasema Makamu wa Rais kama mshauri mkuu wa Rais, ushauri wake unapaswa kusikilizwa na Rais na kufanyiwa kazi (japo Rais halazimiki kuufuata kisheria), lakini si kutamka moja kwa moja hatua dhidi ya ofisa ambaye hakumteua.

“Yeye ni tofauti na Waziri Mkuu. Si msimamizi wa shughuli za siku hadi siku za Serikali. Hiyo ni kazi ya Waziri Mkuu na kauli ya Waziri Mkuu ndiyo kauli ya Serikali,” anasema Madeleka.

Madeleka anasema hata Waziri Mkuu kuna wakati hulazimika kuahirisha kutoa maagizo akisema wazi kwamba kwanza awasiliane na mamlaka za uteuzi.

Dk. Mpango alianza kitambo kuonyesha nia ya kutaka madaraka makubwa, kwani siku anaapishwa, Machi 31, 2021 alisema: “Dk. Mwigulu upande ule wa kodi, lakini pia mapato kutoka kwenye taasisi zetu, bado, bado, bado sana. Tunataka kuona mapato yakiongezeka.

“Na zamu hii Mheshimiwa Rais, sijaomba ridhaa kwako, lakini ningependa, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kabla ya mwisho wa mwaka huu, tuwe tumefikia angalau wastani wa shilingi trilioni mbili kwa mwezi. Inawezekana, inawezekana, mkajipange vizuri.

“Na kwa upande wa TAMISEMI vivyo hivyo, Mheshimiwa Ummy [Mwalimu], huko kuna kazi kubwa. Kuna kazi ya mapato, lakini kuna kazi ya kudhibiti matumizi. Haya mkayafanye katika wizara zote. Mkusanye maduhuli vizuri, lakini mkasimamie matumizi katika wizara zenu, bila kupepesa macho.”

Siku hiyo, inawezekana naye Dk. Mpango alibaini kuwa amevuka mipaka ya madaraka yake kwa kutoa maagizo hayo kwa Wizara ya Fedha na TAMISEMI mbele ya Rais Samia, ndipo akajirudi na kusema: “Tutakapoyaona yana shida, basi mjue nitarudi kwa mama ni mwambie ‘mama huyu hatoshi kukimbia na sisi.’”

Mwanahabari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Pascal Mayalla, anasema:

“Waziri Mkuu, sawa, huyu ni mtendaji, lakini Makamu wa Rais, si mtendaji, yuko pale tu. Ili kumfanya asikae bure, Rais ndiye humtuma kumwakilisha ‘ceremonials’ tu na si ‘executive’.

“Si wengi wanajua, hata wakati Rais hayupo nchini, na nchi inakuwa chini ya Makamu wa Rais, huyo Makamu hawezi kusaini chochote kinachohitaji saini ya Rais!

“Wakati wa Mwalimu Julius Nyerere, tulikuwa na sheria ya ‘Presidential Preventive Detention Order’ (sheria ya kuwaweka watu kizuizini), kukatokea suala, Mzee Ali Hassan Mwinyi akiwa Makamu wa Rais, akasaini hiyo ‘order’ kwa niaba ya Rais.

“Mtu akatiwa ndani! Maprofesa watatu wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wakafungua shauri, ‘a writ of habeas corpus’.

“Mahakama ikaitengua hiyo amri. Makamu wa Rais ‘has no executive powers’ za aina yoyote zaidi ya kumsaidia Rais, kwa jinsi ile ile Rais wa Zanzibar ni Waziri asiye na Wizara Maalumu kwenye Baraza la Mawaziri wa Muungano, lakini hana anachoweza kukifanya ndani ya Serikali ya Muungano. Kinachotakiwa hapa ni kuziainisha kazi anazopaswa kufanya Makamu wa Rais.”

Hata hivyo, Dk. Mpango hakuanza kutoa kauli zenye utata majuzi, kwa kuwa hata wakati akiapishwa kushika nafasi hiyo ya juu nchini, aliwashangaza watu aliposema:

“Nitahakikisha ninasimamia matumizi ya ukusanyaji wa kodi. Kama ni kuniona mbaya, wataniona katika hili.”

Akizungumzia majukumu ya Makamu wa Rais, Wakili wa Kujitegemea, Everest Mnyele, anasema Dk. Mpango anafahamu ni nini anachokifanya.

Anasema katika suala la Dambaya, Dk. Mpango hajamfukuza kazi, bali amemsimamisha kazi kupisha uchunguzi.

“Hawezi kumfukuza kazi kwa kuwa DED si mwanasiasa. Nafasi yake si ya kisiasa bali ni ya kiutendaji na hawajibiki kwa Makamu wa Rais.

“Akikutwa na makosa anaweza kupunguzwa cheo na kurejea kwenye nafasi ya awali katika utumishi wa umma. Hii ni tofauti na ma-DC,” anasema Mnyele.

Anakiri kuwa nafasi ya Makamu wa Rais kwa Tanzania ni sawa na ilivyo nchini Marekani; kwamba hawezi kufanya chochote ila tu kwa ridhaa ya Rais, na kwamba akiwa katika ziara ya Mtwara, huenda alikuwa na ridhaa ya Rais.

“Kwa Kenya nafasi kama aliyonayo Dk. Mpango inaitwa Deputy President (Naibu Rais). Huyu majukumu yake yapo na yameainishwa vizuri kabisa tofauti na hapa kwetu,” anasema Mnyele.

Ofisa mwingine amelalamikia tabia ya Dk. Mpango kutumia makanisa kutoa kauli zinazohusu masuala ya serikali au kuingilia migogoro ya dini. “Nchi yetu haina dini. Sisi tusigeuze siasa zetu kuwa kama za Wakenya wanaofanya siasa makanisani, misikitini na misibani. Dk. Mpango akienda kusali, asali na kurejea nyumbani, akipewa fursa ya kutoa neno, asalimie waumini na pengine akusanye sadaka tu, lakini asiingize kazi za serikali makanisani.”

Juhudi za kumpata Dk. Mpango hazikuzaa matunda, kwani simu yake muda wote ilikuwa inaita bila kupokewa. Hata Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, hakuwa tayari kulizungumzia hili. JAMHURI litaendelea kumtafuta Makamu wa Rais Dk. Mpango kupata ufafanuzi juu ya utaratibu wake wa kutoa matamko na sasa kusimamisha watumishi wa umma kinyume cha Katiba au mamlaka yake kisheria.