NGARA

NA MUSHENGEZI NYAMBELE

Kwenye Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumteua mgombea urais mwaka 1995, Mwalimu Julius Nyerere alisimulia kilichomtokea New York, Marekani mwaka 1994.

Alikaribishwa na Getrude Mongela (wakati huo Katibu wa Mkutano wa kina mama wa Beijing) kushiriki chakula cha jioni. 

Mwalikwa mwingine, mama wa Kiganda, alimchokoza Mwalimu kwa kumweleza kuwa alipokuwa anafanya kazi Arusha kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wafanyakazi wenzake kutoka Uganda na Kenya walijulikana kwa makabila yao, lakini wa Tanzania haikuwa hivyo.

Katika kujibu, Mwalimu alisema Tanzania ilikuwa hivyo huko nyuma, lakini hali ilishabadilika. Alimjulisha kwamba Watanzania walikuwa wakiulizana makabila, wakidhani kuwa ni jambo la maana sana. 

Mwalimu akahoji iwapo kwa kuulizana makabila walitaka kutambika? Kwani faida ya makabila iliyokuwa imebaki ni kutambika tu.

Baada ya kueleza jinsi mataifa makubwa yalivyotawala dunia, akaendelea: “Nyinyi Waswahili, vi-nchi vidogo vidogo hivi, vya watu milioni 27 mnazungumza makabila! Mtuingize katika karne ya 21 mkiwa mnapanda basi la makabila?” 

Alihitimisha hotuba yake kwa Mkutano Mkuu huo kwa kusema: “Tunataka mtuchagulie mtu ambaye anajua kushabikia ukabila ni upumbavu na ni hatari.” 

Hatimaye akateuliwa Benjamin Mkapa kuwa mgombea na baadaye akawa Rais wa Tanzania. Sasa je, aliyazingatia maneno ya Mwalimu katika utawala wake? Marais waliofuata nao vipi?

Ubaguzi wa watu Ngara

Novemba 1999 aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngara, hayati Stephen Bitwale, alikabidhi kwa Rais Mkapa barua iliyokuwa na kichwa cha habari; ‘WASIWASI WA WANANCHI WANAOTOKA WILAYA YA NGARA WAISHIO DAR ES SALAAM’. 

Miongoni mwa aliyoyaeleza katika barua ile ni kwamba wananchi wa Ngara wanashangaa na kusikitika kwa nini ni wao tu wanabaguliwa kwa kutuhumiwa kuwa si Watanzania, bali ni Warundi au Wanyarwanda huku wanaoishi wilaya nyingine za mipakani hawatuhumiwi kuwa raia wa nchi jirani kama Msumbiji, Malawi, Zambia, Zaire (DRC) au Kenya na Uganda?

Aliandika: “Kama hatuoni tofauti ya Mjaluo au Mmasai wa Kenya na yule wa Tanzania huko Kaskazini; Mnyamwanga wa Tunduma na yule wa Nankonde, Zambia; Mmakonde wa Tanzania na wa Msumbiji kusini mwa nchi; inakuwaje tuwaone wa Wilaya ya Ngara kuwa ni Warundi na Wanyarwanda?” 

Sikuwahi kupata ushahidi iwapo Rais Mkapa aliyafanyia kazi malalamiko yale.

Mimi binafsi nimekuwa mwathirika wa ubaguzi huo tangu nikiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Mwaka 1974 niligombea urais wa Serikali ya Wanafunzi (DUSO). 

Miongoni mwa wapinzani wangu wakubwa alikuwamo Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, aliyegombea umakamu wa Rais Kampasi ya Mlimani, huku akiwa nyuma ya mmoja wa wagombea urais. 

Usiku wa kuamkia siku ya uchaguzi, wapinzani wangu waligawa vipeperushi vyumbani kwa wanafunzi, si wa Mlimani pekee, bali pia Kampasi za Muhimbili (MUHAS) na Morogoro (SUA).

Pamoja na madai mengine, waandishi wa kipeperushi kile waliwaonya wapigakura kutonichagua kwa kuwa mimi nilikuwa nusu-mkimbizi kutoka Rwanda (Semi-Rwandese Refugee). 

Nilishindwa urais kwa kura 14 tu. Hata nilipolalamikia uhalali wa ushindi wa mpinzani wangu, uongozi wa chuo wakati ule uliziba masikio. Mzee Pius Msekwa analikumbuka hilo. Ubaguzi huo wa awali uliniandama maisha yangu yote hadi leo.

Kunyimwa leseni ya kumiliki silaha tangu 2005 

Mwaka 2002 nilizawadiwa silaha aina ya ‘Rifle’. Aliyenipa zawadi hiyo aliikabidhi Bohari ya Silaha ya Polisi (armory) Ngara takriban miaka 20 iliyopita, yaani Januari 24, 2002. 

Kwa mujibu wa sheria, nilitakiwa kwanza kukamilisha taratibu za kupata leseni ya kuimiliki kabla ya kukabidhiwa na polisi. 

Kutokana na majukumu ya kazi nje ya wilaya na mkoa, sikuweza kuwasilisha maombi rasmi ya kumilikishwa silaha hiyo hadi Machi 2005. 

Tangu mwanzo sikuwa na haraka wala wasiwasi wowote juu ya kukidhi vigezo vya kupewa leseni kwa kuwa wakati huo nilikuwa ninamiliki kihalali silaha nyingine tangu mwaka 1988. Jambo la kushangaza na kusikitisha ni kwamba, tangu wakati huo hadi leo maombi yangu hayajapitishwa, hivyo silaha hiyo bado imo mikononi mwa polisi.

 Kutokana na kumbukumbu mbalimbali, ni dhahiri kuwa maombi yangu ya kumilikishwa silaha hayakupitishwa kutokana na hisia potofu miongoni mwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, kwamba mimi si Mtanzania halali. 

Katika mojawapo ya mawasiliano baina ya mjumbe wa Idara ya Uhamiaji kwenda mkoani ilidaiwa kwamba mimi niliwahi kuwa mtumishi wa serikali wa cheo cha juu katika Mamlaka ya Mapato (TRA) lakini niliondolewa kwenye utumishi huo kwa sababu si Mtanzania.

Ni kweli kwamba mwishoni mwa Juni 2002, ajira yangu TRA ilisitishwa katika mazingira ambayo hadi leo sijapata maelezo yake. 

Kabla ya hapo, Gazeti la Majirala Jumapili, Februari 24, 2002, lilikuwa limeandika yafuatayo chini ya kichwa cha habari; ‘WATUTSI, WASOMALI, WACONGO WAITEKA DAR’

“JIJI la Dar es Salaam limetekwa na raia kutoka nchi jirani za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Somalia wanaoishi nchini kinyume cha sheria za uhamiaji, jambo linalohatarisha usalama …”

Gazeti hilo lilimnukuu ‘kiongozi mmoja wa CCM‘ akisema: “Kuna vigogo wengi kwenye sekta mbalimbali muhimu hata zile nyeti ambako wanaoziongoza si Watanzania, wanachofanya ni kuhakikisha wanawavuta wenzao wanaojifanya ni Watanzania na kuwapatia kazi. Sasa hivi kuna Watutsi kibao katika sekta zote hususan maofisini …

“Sehemu zilizotajwa kuenea kwa watu hao ni Wizara ya Mambo ya Ndani na Idara ya Mahakama na taasisi zilizotajwa kuvamiwa zaidi na wageni ni TRA na UDSM.”

Baada ya makala hiyo kuchapishwa gazetini, mwananchi aliyejipa jina la Remmy Mbonde, lakini aliyeomba jina lake lisichapishwe, aliandika barua kwa Mhariri wa Majira Jumapili akimpongeza kwa kuchapisha makala ile.  

Alidai kwamba waandishi wake (mhariri) mahiri walikuwa wamefumbua macho ya Watanzania juu ya tatizo lililokuwa likiota mizizi ‘huku serikali ikionekana kulifumbia macho’.

Alieleza kwamba ilikuwa haitoshi kumnyang’anya uraia Jenerali Ulimwengu peke yake, kwa kuwa walikuwapo akina ‘Jenerali’ zaidi ya milioni nchini. 

Aliendelea kudai kwamba wakati TRA inaanzishwa, kuna baadhi ya Watusi walioshiriki: “moja kwa moja na ni hao hao waliohusika na kufukuza wazalendo wengi waliokuwa katika idara za Customs na VAT.

“Wakati fulani Serikali ilimshitukia kigogo mmoja ndani ya TRA, Bwana Nyambele Mushengezina na kumnyang’anya pasi ya Tanzania. Alisikika akilalamika kwamba pasipoti yake ilikuwa imeshikiliwa na Serikali kwa zaidi ya mwaka mmoja. Hiyo ilikuwa mwaka 2000. Cha ajabu ni kwamba hadi leo kigogo yupo na anaendelea na kazi na kutumbua huku Watanzania halali wengi wakisota bila kazi, wengine akiwa ndiye aliyewaachisha au kuwafukuza.

“Wakati wa likizo zake, Bwana Nyambele huenda Burundi na Rwanda kufanya kazi na baada ya hapo hurejea na kuendelea na kazi kama kawaida. Tunashangaa ni serikali ya namna gani inayoweza kumruhusu mtu kuichezea namna hiyo. Mara ya mwisho ni mwaka jana mwanzoni alipokwenda kufanya kazi katika Burundi Revenue Authority. Hata hivyo, ni lazima tujiulize; kama alinyang’anywa pasi ya Tanzania, anatumia ya nchi gani?” 

Kama nilivyoeleza hapo juu, miezi minne baada ya chapisho lile la Februari 24, 2002, Bodi ya Wakurugenzi ya TRA ilikutana kujadili, pamoja na ajenda nyingine, maombi ya mikataba mipya ya ajira kwa wakuu wa idara na wasaidizi wa wakuu wa idara ambao mikataba yao ya kazi ilikuwa inamalizika mwisho wa Juni mwaka huo.

Kama mtendaji wa kwanza kuteuliwa kushiriki kuanzisha chombo hicho, nilikuwa nimeshiriki katika kupitisha uamuzi wa kuajiri viongozi wa ngazi hizo mbili kwa mikataba ya miaka mitatu mitatu; madhumuni yakiwa ni kuhakikisha kwamba watendaji hao wanafanya kazi kwa ufanisi na uadilifu wa hali ya juu huku Bodi ya Wakurugenzi ikiwa na madaraka ya kuwaondoa wakati wowote au kutowaongezea muda wa kuendelea kufanya kazi baada ya mikataba yao kufikia ukomo. 

Hata hivyo, Bodi ilikuwa imekubaliana kwamba kwa wale ambao wangeendelea kumudu masharti yote ya kazi, wangekuwa wanaongezewa mikataba yao kila baada ya miaka mitatu hadi umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma. 

Kwa taarifa za uhakika nilizopata baadaye, bodi ilipofika kwenye ajenda ya kupitisha mapendekezo ya Kamishna Mkuu ya kuidhinisha mikataba mipya, ukiwamo wa kwangu, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dk. Ennos Bukuku, aliitaarifu bodi kwamba serikali ilikuwa imeagiza kwamba mimi nisipewe mkataba mpya wa ajira. 

Kamishna Mkuu na wajumbe wengine wa bodi walishitushwa na taarifa hiyo, lakini mwenyekiti hakuwa tayari kutoa maelezo zaidi. 

Baada ya kuachishwa kazi katika mazingira hayo yenye utata, nilifanya jitihada kujua sababu zilizoifanya ‘serikali’ kutoa uamuzi huo kama hilo lilikuwa kweli. Niliandika barua kwa Katibu Mkuu Kiongozi.  

Baada ya kutopata majibu ya hoja yangu, niliandika kwa Rais Kikwete, lakini naye hakujibu barua yangu. Wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 52. Niliamua ‘kupotezea’ na kusonga mbele. 

Kama nilivyogusia hapo juu, hoja ya uraia wangu imedumu miaka mingi, tangu nikiwa chuo kikuu. Lakini naomba msomaji atafakari yafuatayo: 

1.  Nilisomeshwa na serikali tangu ngazi ya awali hadi chuo kikuu.

2.  Niliajiriwa na EAC mwaka 1976 katika Idara ya Forodha na Ushuru.

3.  Mwaka 1979 nikiwa Mkuu wa Idara hiyo kwenye mikoa ya Iringa, Mbeya na Rukwa, nilipewa pasi ya kusafiria ya Tanzania kwa mara ya kwanza. Baada ya hapo nilikuwa ninapewa hati mpya kila niliyokuwa nayo ilipokwisha hadi leo.

4.  Kabla ya hapo, mwaka 1978 niliitwa Ikulu, Dar es Salaam na kutakiwa kujiunga na Ofisi ya Rais; kazi ambayo niliikataa kwa sababu binafsi. Niliwahi kuwa na hisia kwamba hii ilikuwa sababu ya huo unyanyasaji wa baadaye, lakini kazi nilizopewa zinapingana na hisia hizo.

5.  Kati ya mwaka 1979 hadi 1987 nilikuwa Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Uhusiano wa Kimataifa katika idara hiyo hiyo Makao Makuu. Kwa wadhifa huo nilikuwa mwakilishi (Balozi) wa Tanzania kwenye Shirikisho la Dunia la Forodha (World Customs Organisation). Pia nilikuwa mjumbe kwenye timu ya wataalamu wa Tanzania walioshiriki mazungumzo ya kuanzisha PTA (baadaye COMESA).

6.  Mwaka 1987 hadi 1989 nilikuwa Mkuu wa Idara ya Forodha na Kodi ya Mauzo Mkoa wa Tanga. Nikiwa huko nilifanikiwa kumng’oa kazini mkuu wa mkoa baada ya kuingilia majukumu yangu ya kuzuia upotevu wa mapato ya serikali kutokana na biashara za magendo. Aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa na Ofisa Usalama wa Mkoa wote walihamishwa, kwa kuwa walikuwa wanamtetea mkuu huyo wa mkoa wakati akiniingilia katika utendaji wangu wa kazi.

7.  Mwaka 1989 niliteuliwa kuwa Katibu Msaidizi kwenye Tume ya Rais ya kuchunguza na kushauri namna ya kuongeza mapato ya serikali na kupunguza matumizi (Tume ya Mtei). Ni tume hiyo ambayo ilipendekeza, pamoja na mambo mengine, uanzishaji wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato muhimu unaojitegemea ili serikali iweze kuwapatia watumishi wa mfumo huo mafunzo ya kutosha, mishahara mizuri na vitendea kazi vya kutosha ili waweze kupaisha mapato kwa maendeleo ya nchi.

8.  Mwaka 1991 baada ya Tume ya Mtei kumaliza kazi yake nilipangiwa kazi makao makuu ya idara kama mkuu wa kitengo cha kuzuia na kupambana na dawa za kulevya. Katika wadhifa huo nilishiriki katika kuandaa muswada uliokabidhi kazi hiyo kwa Jeshi la Polisi.

9.  Mwaka 1993 niliteuliwa kuwa Kaimu Kamishna Msaidizi kwenye kitengo cha upelelezi, uzuiaji magendo na uendesha mashitaka. Nakumbuka kadhia kubwa mbili nilizokumbana nazo katika wadhifa huo. Moja, kulikuwa na upotevu mkubwa wa mapato kutokana na udanganyifu uliofanywa na waliodai kuingiza mafuta ghafi na kuyasafisha (refine) kabla ya kuingizwa sokoni. Nilitembelea ‘kiwanda’ kimojawapo kuchunguza iwapo kilikuwa na uwezo huo.

Nikiwa bado sehemu ya mapokezi ya kiwanda hicho, mhusika alimpigia simu mwenye kiwanda kumjulisha juu ya uwepo wangu kwa ajili ya ukaguzi. Niliambiwa kusubiri pale mapokezi. Baada ya muda nilipewa simu kuongea nikakuta aliyekuwa amepiga ni mkuu wangu wa kazi ambaye alisema alikuwa ameagizwa na kiongozi mmoja mkuu serikalini (siyo Rais) kuwa niachane na kazi hiyo mara moja.

Kadhia ya pili kubwa ilihusu upotevu wa mapato kwenye uingizaji wa bia aina ya Stella Artois. Mwingizaji wa bia hiyo alikuwa akipewa kibali na mamlaka husika cha kuondoa bidhaa bandarini kwa masharti kuwa angelipa kodi husika kidogo kidogo kwa mafungu (installments). 

Baada ya muda mrefu bila idara kupata malipo yoyote nilifuatilia, lakini mkuu mmoja wizarani aliniita na kunionya kuacha ufuatiliaji ule. Baada ya siku chache nilipokea barua ya uhamisho kwenda Mkoa wa Mwanza!

10.  Mwaka 1995 baada ya sheria ya kuanzisha TRA kupitishwa niliteuliwa na serikali kuwa Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi ya kwanza. Baada ya Bodi na serikali kupitisha muundo rasmi wa TRA nilithibitishwa kuwa Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi na Mwanasheria Mkuu wa Mamlaka. 

Ni vema kusisitiza hapa kwamba uanzishwaji wa mamlaka maalumu ya kusimamia ukusanyaji mapato ulikuwa umependekezwa kwenye ripoti ya Tume ya Mtei iliyowasilishwa kwa Rais Ali Hassan Mwinyi mwaka 1991. Ni Rais Mwinyi aliyesaini muswada wa sheria ya kuanzisha TRA Agosti, 1995 lakini uzinduzi wa TRA kuanza kazi rasmi ulifanywa na Mkapa, Juni 30, 1996.

 Hitimisho

Baada ya jitihada za takriban miaka 10 ya kupigania haki yangu ya kumilikishwa silaha hiyo kushindikana, Oktoba 2011 nilimwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi nikilalamikia uonevu ule. 

Aidha ‘nilijisalimisha’ kwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji na kuomba kuchunguzwa uraia wangu kama miaka yote hiyo ya nyuma walikuwa hawajafanya hivyo. Ndipo, baada ya zaidi ya miaka mitatu na nusu niliandikiwa barua na Kamishna Mkuu huyo akinitaarifu ifuatavyo:

“Kwa barua hii, nimeelekezwa nikujulishe kuwa baada ya kukamilisha uchunguzi wetu, imethibitika pasipo shaka kuwa wewe ni raia wa Tanzania kwa mujibu wa kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Uraia ya Tanzania Sura ya 357 (Rejeo la 2002) na kanuni zake za mwaka 1997.”

Barua hiyo ilinakiliwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ofisi ya Uhamiaji ya Mkoa wa Kagera na ile ya Wilaya ya Ngara. Barua hiyo ilikuwa ya Machi 10, 2015, miaka zaidi ya sita iliyopita na bado silaha imeshikiliwa na serikali. 

Ni kwa sababu hiyo nimeona ni vema niikabidhi serikali silaha hiyo na nyingine niliyomilikishwa mwaka 1988. Iwapo pamoja na maelezo yote hapo juu na nyadhifa nilizoshika serikalini bado serikali haina imani na mimi kama Mtanzania wa kweli, basi sistahili kumiliki hata hiyo silaha ingawa nina hakika kuwa wako watu wengi nchini ambao si raia, lakini wako nchini kihalali na wanamiliki silaha zao kihalali.

By Jamhuri