Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kigoma

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, amesema juhudi za kulinda mazingira zinazofanywa na taasisi mbalimbali kuhamasisha nishati safi ya kupikia zinastahili kuungwa mkono.

Pia, ameipongeza Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited (OGTL) kwa kazi nzuri inayoifanya kuiwezesha jamii kupata gesi safi ya kupikia kwa kugawa mitungi ya gesi na majiko yake kwa wananchi, hivyo kutekeleza mkakati wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Dk. Mpango alisema hayo kwa wananchi wa Wilaya ya Buhigwe, mkoani Kigoma katika hafla ya kukabidhiwa kwa vifaa mbalimbali kwa wanawake wajawazito ikiwemo mitungi ya gesi 300 iliyokabidhiwa kwa wajawazito 214 na watumishi wa afya ngazi ya jamii 86 kutoka wilaya hiyo.

Mitungi hiyo imetolewa na OGTL kwa kushirikiana na Taasisi ya Doris Molleli Foundation kwa lengo la kuwajengea wanufaika mazingira salama ya kupikia na kunusuru uharibifu wa mazingira unatokana na ukataji miti inayotumika kutengeneza mkaa na kuni kama nishati ya kupikia.

Akizungumza zaidi wakati akikabidhi vifaa hivyo pamoja na mitungi ya gesi ya Oryx , Dk.Mpango pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kuipongeza Oryx Gas kwa uamuzi wa kugawa mitungi hiyo bura kwa wananchi wa Buhigwe.

“Niipongeze kampuni ya Oryx Gas kwa kazi nzuri inayoifanya kwa kuiwezesha jamii kupata gesi safi ya kupikia na hatua hii inastahili kuungwa mkono kwani inalenga kuendeleza harakati za kutunza mazingira, ” amesema Dk.Mpango.

Aidha Dk.Mpango amewahimiza wanachi wa Buhigwe kutumia gesi ya Oryx kwa kuwa kampuni hiyo inasaidia jamii kwa kutoa bure mitungi na majiko.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Oryx Gas Kanda ya Kaskazini, Alex John, amesema kampuni hiyo ikiwa kinara wa soko katika usambazaji wa gesi ya kupikia nyumbani (LPG) nchini, inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa kwa wananchi kuunga mkono juhudi za serikali za kuhimiza matumizi ya nishati hiyo.

Ameongeza gesi safi ya LPG ni suluhisho la kutokomeza matumizi ya kuni na mkaa, hivyo kuboresha afya ya jamii, ustawi na utunzaji wa mazingira, pia ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan la kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kama mkakati wa kulinda mazingira.

Amefafanua kwamba kabla ya ugawaji wa majiko na mitungi hiyo, yalitolewa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya gesi yaliyowezeshwa na meneja mkuu huyo wa kanda ya kaskazini.

“Tunaamini wahudumu wa afya wa wilayani Buhigwe wanawakilisha watu wengi na wanapaswa kuwa mfano wa mabadiliko ya nishati safi.Sote tunajua kuwa kundi hili lina ushawishi mkubwa kwa watu wanaowahudumia, hivyo Oryx tumeamua kutoa mitungi hiyo na majiko ya gesi ya LPG kuwahimiza na kuwashawishi wengine kuhusu umuhimu wa mabadiliko ya nishati ya LPG,” amesema.

Pamoja na hayo amesema kampuni ya Oryx Gas Tanzania inaendelea kuwekeza katika uingizaji, uhifadhi, ujazaji wa gesi kwenye mitungi na usambazaji wa LPG Tanzania nzima, vikiwemo Visiwa vya Unguja na Pemba huku akisisitiza kila mwaka kampuni hiyo inatumia mamilioni kadhaa ya dola katika mitungi mipya inayoletwa sokoni kila siku.

Amesema kampuni pia inatoa mitungi hii kwa punguzo kubwa, kutoa ruzuku ya gharama nyingi za LPG kwa vifaa vya kuanzia (Mitungi, Gesi na majiko) ili kuwawezesha watu kubadili nishati ya kuni na mkaa kwa kutumia gesi safi na kufanya gesi ipatikane nchi nzima.

By Jamhuri