Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango amesema ni wakati umefika kwa watunga sera barani Afrika kutambua umuhimu wa kilimo na wakulima ili kuweza kutumia vema fursa ya ardhi ya Afrika kujiletea maendeleo.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akishiriki mjadala unaohusu “kutengeneza fursa katika ardhi ya Afrika” uliyofanyika katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani unaofanyika Davos nchini Uswisi.

Amesema ni muhimu watunga sera wa Afrika kutambua umuhimu wa wakulima kwa kuwa ndiyo wanaohakikisha usalama wa chakula, kuongeza fedha za kigeni pamoja na kuongeza upatikanaji wa mapato ya serikali.

Amesema ni muhimu kuondoa sera zisizo rafiki ili kuwasaidia wakulima kufikia masoko kirahisi na kupata haki ya kile wanachozalisha. Pia amesema mikopo kwa wakulima kwa riba nafuu itasaidia ukuaji wa kilimo barani Afrika.

Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea na jitihada za kuboresha sekta ya kilimo kwa kuongeza bajeti ya kilimo mara tatu zaidi, kuongeza huduma za ugani ikiwemo kutoa vitendea kazi kwa maafisa ugani na kufanya ufuatiliaji wa wakulima wa mara kwa mara.

Aidha amesema serikali imeendelea kuweka mkazo kwa wakulima kubadilisha uzoefu wao kwa wao pamoja na kujenga miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo visima vya maji kwa wakulima wadogo.

Pia Tanzania inashirikiana na wadau katika upimaji wa afya udongo, utoaji mbolea kulingana na maeneo husika ya kilimo pamoja na kukaribisha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya uzalishaji mbolea.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema jitihada zinapaswa kufanyika barani Afrika katika kupanga matumizi ya ardhi, kupima afya ya udongo ili kuweza kutambua aina ya mazao na mbolea itakayofaa katika maeneo fulani ya kilimo na hivyo kuongeza uzalishaji.

Makamu wa Rais amewakaribisha wawekezaji, sekta binafsi na wadau kushirikiana na Tanzania katika sekta ya kilimo ikiwemo ujenzi wa maghala ya uhifadhi wa mazao.