Na Isri Mohamed

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imetoa maagizo kwa vyama vya siasa kufanya uchaguzi wa viongozi wapya katika nafasi ambazo viongozi waliopo muda wao unaelekea ukingoni.

Maagizo hayo yametolewa kwa njia ya barua leo Januari 18, 2024 kwa Makatibu Wakuu wa Vyama vya Siasa vyenye Usajili kamili, ambayo imefafanua kuwa Kifungu cha 9(2)(e) kikisomwa pamoja na Kifungu cha 8D(1) cha Sheria ‘The Political Parties Act, CAP 258’ kinaelekeza kuwa kila chama cha siasa kinapaswa kufanya Uchaguzi wa Kidemokrasia wa Viongozi wake kulingana na Vipindi ambavyo vimewekwa katika Katiba yake

Barua hiyo ambayo imesainiwa na Naibu Msajili wa Vyama vya siasa, Sisty Nyahoza kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini Jaji Francis Mutungi, imeendelea kufafanua kuwa Kanuni ya 16 ya Kanuni ‘The Political Parties (Registration and Monitoring) Regulations, 2019 (TS. 953/2019) inaeleza kuwa Uchaguzi wa viongozi wa chama cha siasa unapaswa kufanyika si zaidi ya miaka mitano (5) tangu uchaguzi uliopita kufanyika na kwamba chama husika kitaomba ruhusa ya Msajili wa Vyama vya Siasa endapo kinataka kufanya uchaguzi zaidi ya kipindi hicho.