Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro

BOHARI ya Dawa (MSD), imeanza usambazaji majimboni vifaa tiba vilivyonunuliwa na Serikali vyenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 14.7 kwa ajili ya hospitali, vituo vya afya na zahanati lengo ni kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Meneja wa MSD, Kanda ya Mashariki yenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ,Morogoro na Visiwani Zanzibar, Betia Kaema amesema hayo wakati wa makabidhiano wa vifaa hivyo na mkuu wa mkoa wa Morogoro , Adam Malima kwa ajili ya majimbo 11 ya mkoa huo.

Kaema amesema ,Mkoa wa Morogoro umepatiwa vifaa aina tisa vyenye thamani ya sh milioni 759 na kuanza kusambazwa katika majimbo yote 11 na kila jimbo litapokea vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 69.

“ Kama tunavyofahamu Serikali yetu inayoongozwa na Rais mama Samia Suluhu Hassan , imenunua vifaa kwa ajili ya kupunguza vifo vya mama na mtoto vyenye thamani ya sah bilioni 14.7 na vifaa hivyo vilizinduliwa na Waziri wetu wa Afya kwa ajili ya majimbo ya Tanzania nzima” amesema Kaema.

Kaema amevitaja vifaa vilivyokabidhiwa kwa kila jimbo la mkoa huo na idadi yake kwenye mabano ni Drip stand (330), vitanda vya kawaida vya wagonjwa (330), vitanda vya kujifungulia mama wanajawazito (220) na seti (220) za kujifungulia mama wajawazito.

Ametaja vingine ni shuka (1,320), magodoro (330), Examination table (220), meza ndogo za wagonjwa kuwekea vifaa vyao pale wanapokuwa wamelazwa (165) na Bed side Locker (330).

Kaema amesema hizo zote ni juhudi za serikali katika kuondoa kabisa ama kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua .

“ Kwa sasa serikali imetoa kipaumbele kuimarisha na kuwezesha hospitali zote mikoani ambazo zimeanishwa katika majimbo mbalimbali kuwa na vifaa hivi ili kuweza kuondokana kabisa na vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua” amesema Kaema .

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombonu ya sekta ya afya na kwa sasa imejielekeza katika uboreshaji wa viwango vya utoaji wa huduma za afya nchini.

“ Malengo yetu sisi mkoa baada ya kupokea kwa vifaa tiba hivi ni kwenda kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na hili tumekuwa tukilihimiza nyakati zote “ Malima .

Mkuu wa mkoa huyo alisema licha ya kupokea vifaa tiba hivyo, mkakati wa mkoa ni kuendelea kutoa elimu kuhusiana na kujikunga na magonjwa mbalimbali na namna ya utumiaji wa vifaa hivyo kwa wagonjwa.

Hivi karibuni Waziri wa Afya ,Ummy Mwalimu alizindua usambazaji wa vifaa vya kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto vyenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 14.9 ambavyo vitasambazwa katika majimbo 214 na halmashauri nchi nzima.

Ummy alisema usambazaji wa vifaa vya hivyo umelenga kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto na kuimarisha uzazi salama nchini.