Na Dotto Kwilasa,Jamhuri jamhuriMedia, Dodoma

Spika wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson amewasili Jijini hapa leo Oktoba 30,2023 akitokea jijini Dar es Salaam na kulakiwa na vingozi mbalimbali wa chama na Serikali pamoja na wananchi wa mkoa wa Dodoma.

Hii ni baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa IPU katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27, 2023 jijini Luanda nchini Angola.

Akizungumza mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege Dodoma Dk Tulia Axson amesema nafasi hiyo itasaidia kuing’arisha Tanzania kimataifa huku akitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi na wabunge kwa ujumla kwa maandalizi ya ujio wake .

Licha hayo amezungumzia hali ya uchaguzi uliopelekea yeye kushinda ambapo amesema ,”Haikuwa kazi rahisi kwa sababu kulikuwa na wagombea wengi,kazi hii ni ngumu lakini pamoja na ugumu huo Rais wetu aliweza kuongeza nguvu kuomba kura, “ameeleza

Amesema,” Kikanuni huwezi kugombea kama Serikal yako haikuungi mkono,Rais Samia anahitaji heshima zaidi kwa kufanya kampeni kwenye nchi mbalimbali na kuipa ushindi Tanzania,

Wananchi wenzangu sote kwa pamoja tumshukuru Rais kwa kufanya kampeni,lakini pia nawashukuru wananchi kwa kunitia moyo na maombi yenu mpaka nimepewa heshima hii, lakini ili mambo yaende sawa tuzidi kumuombea Rais wetu awe na amani ya kufanya kazi kubwa aliyo nayo, “amesisitiza

Dkt. Tulia ameshinda urais huo baada ya kupata kura 172 kati ya kura 303 zilizopigwa na anarithi mikoba ya Rais aliyemaliza muda wake, Duarte Pacheco kutoka Ureno.