Na Mussa Augustine, JamhuriMedia

Chama Cha Democratic Party (DP) kimemuomba Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua kufuatia kuwepo kwa Vitendo vya kutozwa gharama kubwa kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH) hali ambayo inawafanya Wananchi kushindwa kumudu gharama za matibabu.

Rai hiyo imetolewa leo Juni 28,2023 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Chama hicho Abdul Mluya wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amebainisha kuwa Waziri wa Afya ameshindwa kuchukua hatua ya kuondoa changamoto hiyo na kuendelea kuwaumiza wananchi.

Amesema kuwa imefika hatua baadhi ya wananchi wamekuwa wakishindwa kuchukua miili ya wapendwa wao wanapofariki kutokana na kutozwa gharama kubwa ambapo ameiomba Serikali kuangalia kwa jicho la tatu gharama za Matibabu zisizo rafiki kwa Wagonjwa.

“Suala la kifo hua nila ghafla ,maisha ya Watanzania yanatofautiana ,unapomtoza mamilioni ya fedha mtu ambaye kafiwa na mpendwa wake na hana uwezo wa kulipa inamfanya asusie maiti ,hivyo naiomba serikali iliangalie gharama hizi”amesema Mluya.

Nakuongeza kwamba imefikia hatua pale Muhimbili imetengwa wodi maalumu kwa ajili yakuwafungia wagonjwa ambao wameshindwa kulipa gharama za matibabu ili wasitoroke ,yaani imetenga wodi hiyo kama Sero ni jambo la kusikitisha sana.

Katibu Mkuu huyo wa DP ameongeza kuwa serikali isifanye afya ya Wananchi kua chanzo cha kipato nabadala yake Waongeze tozo za kodi kwenye mambo ya Anasa kama vile Pombe ,Kumbi za starehe(Nigth Clubs) na zinginezo.

“Ukilala kwenye kitanda wodini kwa siku moja ni elfu thelathini(30,000) hapo bado gharama zingine za huduma ,siku unatoka hospitalini ukipewa ile bili ina gharama kubwa sana,ambapo kwa watanzania wa Maisha ya Kawaida inawaumiza sana ,sisi kama DP tunaomba Waziri wa Afya ajitathmini na kama ameshindwa kazi Rais amsaidie kupumzika”amesema

By Jamhuri