Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Katavi

Ernest Lyoba (61), mkazi wa Kijiji cha Namanyere Kata ya Majimoto Wilaya ya Mlele amejeruhiwa vibaya katika na sehemu yake ya uso na mgongoni baada ya kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana wakati akiwa njiani anaelekea nyumbani kwake .

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani amewaeleza waandishi wa habari kuwa tukio hilo la kikatili limetokea Juni 25,2023 katika cha Kijiji cha Namanyere.

Amesema kuwa siku ya tukio majeruhi akiwa anaelekea nyumbani kwake majira ya saa 9 alasiri mara baada ya kuwa amemaliza shughuli zake za kujitafutia riziki ndipo watu wasiojulikana walimmwagia tindikali sehemu za usoni na mgongoni na kutokomea kusikojulikana.

Kamanda amesema baada ya tukio hilo alipiga kelele za kuomba msaada na baada ya muda mfupi wasamaria qema walifika kwenye eneo la tukio.

Amesema walimchukua na kumkimbiza Hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe kwa ajili ya matibabu hata hivyo kutokana na kuwa amejeruhiwa vibaya mhanga alipewa rufaa ya kwenda kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi.

Hata hivyo baada ya kuwa kufikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi alipewa tena rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa KCMC ya mkoani Kilimanjaro ambako amelazwa hadi sasa.

Kamanda Ngonyani amesema juhudi za kuwasaka watuhumiwa hao zinaendelea ili kuhakikisha wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.

By Jamhuri