Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA Dar es Salaam.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila leo Novemba 1,2023 amekutana na timu ya wataalam kutoka Wizara ya Nishati ambao waliambatana na Wataalam wa gesi Asilia kutoka JICA ambapo wamefanya majadiliano ya kujenga uwezo kuhusiana na matumizi ya gesi Asilia.

RC Chalamila amesema Mkoa wa Dar es Salaam umepata bahati ya kuwa moja ya mikoa kati ya mitatu ambayo mradi huo kabambe utatekelezwa na sababu kubwa ya zilizoangaliwa ni pamoja na idadi kubwa ya watu, viwanda vingi, Taasisi nyingi ambazo zina mahitaji makubwa ya Nishati.

Aidha RC Chalamila amesema Dunia kwa sasa inakabiliwa na mabadiliko ya tabia ya nchi yenye kuleta athari mbalimbali ikiwemo mvua za El-Nino, kwa mantiki hiyo jambo ambalo linafanyika ni kuzuia ukataji wa miti na uoto mwingine wa asili ili kuruhusu matumizi ya gesi Asilia kutumika kama chanzo cha Nishati katika mapishi na mambo mengine.

Vilevile Dar es Salaam pekee hasa kipindi hiki cha ukame hutumia hadi megawati 516 katika mitambo ikiwemo AC, tatizo la kukatika kwa umeme limekuwa likiathiri Shughuli nyingi za maendeleo hivyo Nishati ya gesi Asilia ni mbadala kwa Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa mradi Mhandisi Joyce kisamo alisema kwa kutumia wataalam kutoka Tanzania,wizara ya Nishati, TPDC na EWURA kwa msaada wa JICA (Japan) wamesanifu, kujenga uwezo na kutumia gesi Asilia katika miji ambayo ni Dar es Salaam, Pwani na Dodoma hiyo mikoa ambayo mradi utaanza kutekelezwa na Mikoa mingine itafuata.

Ifahamike kuwa mradi huu ni wa miaka miwili lakini awamu ya kwanza kutakuwa na mpango kabambe wa matumizi ya gesi Asilia nchini Tanzania ambapo mpango huu hutegemewa kuanza mwezi Juni 2024.