Vicheko wakazi wa manispaa kigoma-ujiji, Rais Samia kumaliza kero ya maji

Na Allan Vicent, Kigoma

Zaidi ya sh bil 9.5 sawa na Euro mil 3.2 zilizotolewa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA) zimewezesha kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wenye uwezo wa kuzalisha lita mil 42 za maji kwa siku katika Halmashauri ya Manispaa Kigoma/Ujiji.

Akiongea na JAMHURI jana Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo Mhandisi Poas Kilangi amesema kukamilika kwa mradi huo kumemaliza kero ya maji iliyodumu kwa miaka mingi kwa wakazi wa manispaa hiyo.

Amebainisha kuwa mradi huo wa chanzo cha maji cha ziwa Tanganyika (Amani Beach) uliopo katika kata ya Bangwe mjini hapa mbali na kutoa huduma ya maji safi ya kunywa kwa jamii pia ni fursa muhimu sana kwa wawekezaji.

Mhandisi Kilangi amefafanua kuwa chanzo hicho kinazalisha maji mengi sana zaidi ya mahitaji halisi ya wakazi wa manispaa hiyo ambayo ni lita za ujazo mil 23 kwa siku.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kumeongeza idadi ya watumiaji kutoka 15,000 waliokuwepo hadi 22, 440 mwaka huu, idadi ya wateja wa kuunganishiwa majumbani inaendelea kuongezeka na wakazi wa kata 19 sasa wananufaika.

‘Tunawakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza katika Mkoa wetu kwa kuwa maji sio tatizo tena kama ilivyokuwa huko nyuma, yapo ya kutosha,’ amesema.

Mkurugenzi amemshukuru sana Rais Samia Suluhu na Waziri wa Maji Jumaa Awesu kwa kuwaongezea kiasi cha sh bil 1.9 ili kupanua mtandao wa mabomba katika maeneo yote ambayo hayana huduma ya maji safi na salama katika manispaa hiyo ikiwemo kujenga matenki makubwa.

Ametaja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni Simbo, Sigunga na Kibirizi, Kalalangabo na ujenzi wa Kituo cha kuongezea nguvu (booster) maeneo ya Kibirizi.

Aidha katika kuhakikisha manispaa hiyo inaendelea kuwa safi na salama amesema wanatarajia kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa uvunaji majitaka majumbani.

Naye Afisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo Bi.Regina Kalima amefafanua kuwa mradi huo wa maji ya ziwa Tanganyika umekamilika kwa asilimia 100 na utakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi wa wakazi wa manispaa hiyo.

Amewataka kutunza vizuri miundombinu yake ili udumu kwa miaka mingi na kunufaisha wakazi wote wa manispaa hiyo na vizazi vyao.

Aidha amewaomba kutoa taarifa za watu watakaoharibu miundombinu yake ili hatua kali ziweze kuchukuliwa dhidi yao kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa.