Wauguzi watuhumiwa kuomba rushwa wajawazito

Na Allan Vicent, JamhuriMedia,Tabora

Baadhi ya Watumishi wa Idara ya Afya Mkoani Tabora wametuhumiwa kuomba rushwa kwa akinamama wajawazito na kuwatolea lugha zisizo na staha wanapokwenda kujifungua katika vituo vya afya na zahanati.

Hayo yameelezwa na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani humo Mussa Chaulo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake na kubainisha hatua zilizochukuliwa dhidi yao.

Amesema kitendo hicho ni kinyume cha maadili ya taaluma yao na ni kinyume cha taratibu za utumishi kwani badala ya kuwahudumia wamekuwa wakitanguliza tamaa mbele kwa kuomba rushwa kinyume na taratibu za Wizara hiyo.

Mbali na kuomba rushwa amesema pia wamekuwa wakitoa lugha chafu kwa wagonjwa wanaokwenda kupata huduma za matibabu kwenye hospitali hizo wakiwemo wajawazito.

Amebainisha kuwa wilaya mbili katika mkoa huo ndio zimebainika kuwa kinara wa matukio hayo kwani zaidi ya akinamama 20 walitoa malalamiko juu ya kadhia hiyo ya kuombwa rushwa na kutolewa lugha mbaya.

Kamanda Chaulo amefafanua kuwa taasisi hiyo imeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya kijamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaojihusisha na mapambano dhidi ya rushwa ikiwemo Jeshi la Polisi.

Aidha ameongeza kuwa taasisi hiyo imeendelea kutembelea maeneo mbalimbali ili kubaini wahusika wa vitendo hivyo na hatua zimeanza kuchukulia kwa baadhi ya watumishi hao.

Amebainisha kuwa taasisi hiyo imeendelea kufuatilia utekelezaji miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ili kujiridhisha kama fedha zilizotolewa na serikali zinatumika ipasavyo kwa kazi iliyokusudiwa.