Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA Dar es Salaam

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema kuwa kichwa kipya cha treni ya umeme chenye namba ya usajili E6800-01 kilichoundwa na kampuni ya ‘Hyundai Rotem Company’ (HRC) kimewasili nchini Tanzania kutoka nchini Korea Kusini.

TRC iliagiza vichwa vipya 17 vya umeme kutoka “Hyundai Rotem Company’ (HRC) ya nchini Korea Kusini vyenye namba ya usajili E6800-01 hadi E6800-17 kwa ajili ya reli ya kiwango cha
kimataifa- SGR.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa kitengo cha Uhudiano TRC Jamila Mbarouk leo Novemba 02, 2023 Dar es Salaam

“Mfumo wa uendeshaji unaotumika katika kichwa ni nishati ya umeme wenye
msongo wa kilovoti 25 na l na nguvu ya kilowati 5,000 sawa na nguvu ya 6,800 kwa kipimo cha ‘Horse Power.” Amesema Jamila

“Kichwa kitakuwa na uwezo wa mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa (160km/h), kuvuta na kulisha umeme kwenye mabehewa yasiyozidi 14 ya abiria kwa wakati mmoja.”

” TRC inatarajia kufanya majaribio ya kichwa cha treni kitakachotumika katika reli ya kiwango cha kimataifa kati ya Dar es Salaam na Morogoro na baadaye Dar es Salaam hadi Dodoma, baada ya kukamilisha ukaguzi wa kichwa na mafunzo ya uendeshaji kwa madereva mapema mwezi Disemba 2023.”

Mwezi Disemba 2023 TRC inatarajia kupokea vichwa vingine vitatu (3), mpango wa uletaji vitendea kazi utakuwa ukitekelezwa kwa awamu pindi uundwaji wa vitendea kazi unapokamilika. TRC imeshapokea mabehewa 35 kwa ajili ya uendeshaji wa huduma katika reli ya kiwango cha kimataifa.

Aidha TRC imesema , kufikia Septemba 2023 mradi wa SGR Dar es Salaam -Morogoro umefikia 98.6%, Morogoro Makutupora umefikia 95.41%, Makutupora-Tabora umefikia 12.32%, Tabora-Isaka umefikia 5.02% na Mwanza-Isaka umefikia 41.95%, Mkandarasi kampuni ya CCECC yuko eneo la mradi kwa ajili ya maandalizi ya kuanza utekelezaji wa mradi wa SGR awamu ya pili Tabora- Kigoma.

By Jamhuri