Serikali ya Ethiopia imetia saini muafaka wa amani na kundi moja kuu la waasi nchini humo Oromo Liberation Front- OLF, ili kukomesha uhasama nchini humo.

Awali utawala huko Addis Ababa ulitangaza kuwa sasa kundi hilo halitaitwa la kigaidi kama ilivyokuwa ikijulikana hapo awali.

Hayo yametangazwa muda mfupi uliopita na Runinga ya taifa nchini Ethiopia ambapo mkataba huo umesainiwa katika mji mkuu wa Eritrea ambapo ndio makao makuu ya OLF.

Waziri wa habari wa Eritrea Yemane Gebremeskel amesema kwa sasa OLF itatumia njia za amani kujishughulisha na masuala ya siasa nchini Ethiopia.

Makubaliano hayo ya hivi punde yanaonyesha hatua nyingine anayopiga Waziri mkuu Abiy Ahmed, ya kufanyia mabadiliko taasisi mbali mbali za taifa hilo, kupanua uchumi, pamoja na kuboresha usalama na uhusiano wa kidiplomasia na mataifa mengine duniani.

Hatua hii inatajwa kama jitihada za waziri mkuu mpya wa nchi hiyo Abiy Ahmed kutatua migogoro iliyodumu kwa muda mrefu ndani ya taifa hilo la pili Afrika kwa idadi kubwa ya watu.

Please follow and like us:
Pin Share