DAR ES SALAAM

Na Christopher Msekena

Miongoni mwa waimbaji wa Injili wenye mafanikio nchini ni Madam Flora ambaye kwa kupitia nyimbo zake amefanikiwa kubadilisha maisha ya wengi kupitia muziki.

Baada ya kugusa mamilioni ya watu kupitia muziki sasa amekuja kivingine na taasisi yake ili kuendelea kuigusa jamii kwa namna nyingine.

Madam Flora ameweka wazi kuwa taasisi yake ya Fariji Initiatives ni shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na kusaidia jamii ya watu wanaoishi kwenye mazingira hatarishi hasa watoto, wanawake na wazee ili wajikwamue kielimu, kiafya na uchumi.

“Shirika lilianzishwa  rasmi mwaka 2022 kwa namba ya usajili; 00NGO/R/2840 likiwa na malengo ya kupambana na kuenea kwa magonjwa ya ukimwi na malaria.

“Malengo mengine ni kutoa msaada wa kimaadili, maarifa na kiuchumi kwa wanawake, watoto yatima na makundi mengine yaliyomo kwenye mazingira magumu.

“Hali kadhalika kuhamasisha wanajamii juu ya utunzaji wa mazingira,” amesema Madam Flora.

Katika kile kinachoonekana kujikita zaidi katika kugusa maisha ya watu kupitia taasisi hiyo, Madam Flora amesema: “Dira kubwa ya shirika hili ni kuimarishwa kwa maisha na usawa kwa wanawake, watoto, yatima, wazee na makundi yaliyotengwa na jamii Tanzania na hilo tumeanza kulifanikisha.”

Madam Flora amesema ndani ya mwaka huu tayari shirika hilo limewafikia watu wengi, ikiwa ni robo pekee ya 2022: “Hadi Machi 30, mwaka huu, Shirika la Fariji limefanikiwa kuwasaidia watoto takriban 590 wa darasa la nne na 310 wa chekechea katika Halmashauri ya Chalinze kupitia kampeni ya ‘Wezesha Mtoto Asome’.”

Aidha, anaongeza: “Fariji Initiatives inakuomba wewe mdau wa maendeleo na unayeguswa na changamoto wanazokumbana nazo watoto na wanawake waliopo kwenye mazingira hatarishi, uzidi kutuunga mkono ili tuifikie jamii kwa upana zaidi.”

Madam Flora ambaye ni mbeba maono na Mkurugenzi Mtendaji wa Fariji Initiatives anasema: “Nimekuwa nikifanya huduma hii ya kusaidia watu wenye mahitaji zaidi ya miaka 13 sasa, namshukuru Mungu kwa kuwa ninapata sapoti mbalimbali kutoka kwa watu wengine na ninatamani waendelee kujitokeza kuisapoti Fariji Initiatives ili tuwafikie watu wengi zaidi.

“Kwa sasa tuna ‘project’ ya wezesha mtoto asome, tunategemea kujenga vyoo kwenye baadhi ya shule za Chalinze na hii ni baada ya kutembelea Chalinze na kufanya utafiti kwa kushirikiana na halmashauri (Ofisa Elimu), kwa hiyo tunapambana kuhakikisha tunajenga vyoo ili kuwezesha mtoto asome kwenye miundombinu bora.

“Ninaishukuru serikali chini ya uongozi wa Mama Samia Suluhu Hassan, maana jitihada zinazofanyika kuweka miundombinu mizuri ya shule ni kubwa, na sisi tunamuunga mkono ili watoto wapate elimu bure na bora.”

By Jamhuri