Na Byarugaba Innocent, JamhuriMedia, Kibaha

Bodi ya Michezo ya kubahatisha Tanzania GBT imekabidhi mradi wa Maji wenye thamani ya Shilingi 64,656,520 kwa uongozi wa Shirika la Elimu Kibaha unaolenga kutatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji iliyokuwa ikiwakabili wanafunzi wa shule ya Sekondari Kibaha wavulana na kuathiri utoaji na upokeaji wa Taaluma

Hafla ya makabidhiano imefanyika Oktoba 12,2023 wakati wa mahafali ya 57 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo ambayo imezalisha wataalam wengi wanaofanyakazi ndani na nje ya Tanzania.

Akikabidhi mradi huo,Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo James Mbalwe amesema uongozi wa bodi hiyo ufikia uamuzi wa kutoa msaada huo baada ya kuona na kujiridhisha kero kubwa waliyokuwa wakipata wanafunzi na kuathirika kimasomo hivyo kuona kwao ni faraja kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto hiyo.

Aidha,ameongeza kuwa wamekuwa wakitoa misaada mingine kama vile kusaidia vifaa na kujenga majengo maeneo yenye uhitaji kama sehemu ya kurudisha kwa jamii

“Msaada huu ni mwendelezo wa GBT kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kuboresha na kuunga mkono sekta ya Elimu bila malipo ili kuwa fanya wanafunzi kutimiza ndoto zao” amesema Mbalwe

Mkuu wa shule hiyo George Kazi ameeleza kuwa eneo lao lilikuwa na changamoto kubwa ya Maji na kwamba mradi huu umekuwa mwarobaini wa utatuzi kwani GBT pamoja na kujenga miundombinu ya Kisima imejenga pia tenki la chini lenye ujazi wa Lita 100,000 na kuweka simutenki tano zenye ujazo wa Lita 10,000 zitakazotumiwa na wanafunzi 825 pamoja na watumishi.

Sambamba na hilo, Kazi amezitaja faida za mradi kuwa utaongeza ufanisi kwenye ufundishaji na ujifunzaji kwani wanafunzi walikuwa wakitumia muda wa vipindi kwenda kutafuta Maji,Usafi wa miundombinu,uhakika wa upatikanaji wa maji Safi na salama ya kunywa na kupikia pamoja na ufufuaji wa Kilimo cha bustani za shule zitakazo wahakikishia upatikaji wa mboga salama zitakazoimarisha afya zao.

Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha Robert Shilingi amewashukuru bodi ya Michezo ya kubahatisha Tanzania msaada huo na kutoa rai kwa taasisi nyingine kuwiwa kutoa kwani Shule hiyo bado ina mahitaji mengi ikiwemo matengenezo makubwa ya jiko la gesi ambalo limeanza kutumika miaka 30 iliyopita

By Jamhuri