Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Chalinze

Kituo cha Kupoozea Umeme cha Chalinze kimefikia asilimia 84.3 ambapo ifikapo Desemba mitambo itawashwa.

Aidha, ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme kutoka kituo hicho hadi Bwawa la Mwalimu Nyerere ujenzi wake umefikia asilimia 99.

Akiwa kwenye ziara ya kutembelea kituo hicho ,Naibu Waziri Mkuu Dk Dotto Biteko ameeleza, Serikali itahakikisha inatatua changamoto ya umeme nchini hatua kwa hatua ili kupunguza tatizo lililopo kwenye maeneo ambayo bado yana changamoto.

Biteko amepongeza hatua ya ujenzi ulipofikia na kupongeza vijana walioajiriwa katika ujenzi wa kituo hicho.

Ameeleza kuwa Serikali Inathamini mchango wa ujenzi wao.

Awali Abubakar Kunenge Mkuu wa Mkoa wa Pwani akimpokea, Naibu Waziri Mkuu katika ziara yake ameeleza ,uongozi wa Mkoa umekuwa karibu na kituo hicho kuangalia maendeleo ya mradi.

Amefafanua kuwa ni mradi mkubwa na ametoa maelekezo kwa Halmashauri wapange eneo linalozunguka mradi ili liwe na tija zaidi.

Kunenge ameeleza vijana walioajiriwa wamepata ujuzi na ujira.

“Kituo hiki ni Mlmahususi kwa ajili ya kupoozea umeme kutoka kwenye Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere kutoka Kv 400 Kuja Kv220 na kuunganisha kwenye Gridi ya Taifa.

“Umeme utapoozwa kutoka Kv 220 Kuja 132 na kuunganisha kwenye gridi ya Taifa.” amebainisha Kunenge.

Akitoa taarifa ya mradi huo Mhandisi wa Mradi Newton Livingstone ameeleza kituo hicho kwa awamu ya lwanza kitakuwa na uwezo wa kuzalisha Mw 850.

Amengeza kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa mradi wa nyumba za watumishi 9 na barabara ya lami ya Km 1.3.

By Jamhuri