Na WAF Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuboresha Huduma za afya nchini imejenga wodi maalum za uangalizi wa watoto njiti 128 na kwa mwaka huu imepanga imepanga kujenga wodi nyingine 100 ili kuhakikisha vifo vya watoto wachanga vinapungua na kuisha kabisa.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakati akifungua Kongamano la kwanza la Afya ya Mtoto Tanzania na mkutano wa 24 wa Madaktari Bingwa wa Watoto Tanzania unaoendelea jijini Dodoma kwa lengo la kuangalia ustawi wa mtoto kuanzia anapozaliwa mpaka kukua kwake.

Dkt. Mollel amesema kuwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika uangalizi wa watoto njiti lengo likiwa ni kuwapatia huduma bora na uangalizi maalum mpaka watakapofikia uzito unaostahili.

“Uwekezaji huu ni pamoja na kuwa na madaktari Bingwa wa watoto (Madaktari wa Mama Samia), kuboresha miundombinu katika Hospitali zote zenye wodi ya uangalizi maalum kwa watoto njiti ( NICU)”. Ameeleza Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel amesema serikali imeamua kuwekeza katika eneo hilo kwani mtoto kuanzia anapozaliwa mpaka kutimiza miaka 18 anahitaji uangalizi wa karibu ili kupata ustawi mzuri na kuwa na taifa la kesho imara.

Aidha, ametoa wito kwa Madaktari Bingwa wa Watoto nchini kuendelea kufanya kazi nzuri ya kuwahudumia watoto wanaozaliwa kabla ya siku na wale wanaozaliwa kawaida kwani wote wanahitaji uangalizi wa karibu katika ukuaji.

“Kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu tunawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuhakikisha mnapunguza vifo vya watoto wachanga nchini, na kwa mantiki hiyo niwahakikishie kuwa tutakuwa bega kwa bega na nyie ili kuhakikisha mnatekeleza majukumu yenu kwa ufasaha” amesema Dkt. Mollel.

Kwa upande wake Mshauri Mkuu Mwandamizi wa Sera na mipango kutoka USAID Tanzania, Jema Bisimba amesema kuwa hivi karibu watazindua programu ya USAID Tuwajali watoto yenye lengo la kusaidia watoto wanaoishi na virusu vya UKIMWI kuanzia miaka sifuri hadi miaka 17 kwa kuwawezesha Huduma zote zinazohusu mambo ya watoto.

Bisimba amesema kwa kupitia programu hiyo watasaidia Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Afya kufikia lengo la kumaliza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa watoto fufikia 2030