Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KATIKA kuunga mkono juhudi za Serikali kusimamia upatikanaji wa elimu bora na mazingira rafili ya utoaji huduma hiyo mijini na vijijini, Benki ya NMB imetoa msaada wa madawati, viti na meza kwa shule tano za msingi wilayani Kibaha mkoani Pwani, vyenye thamani ya Sh. Mil. 25.

Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Dismas Prosper amekabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, aliyepokea kwa niaba ya Wakuu wa shule za Kambarage, Lumumba, Kongowe, Bungo na Viziwaziwa, hafla iliyofanyika viwanja vya shule ya Kambarage

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Prosper alisema changamoto za elimu Tanzania ni miongoni mwa vipaumbele vya taasisi yake hiyo, ambayo inaamini kuwa elimu ni ufunguo wa maendeleo ya taifa lolote duniani.

“Tunatambua jitihada za dhati na za makusudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha miundombinu na mazingira ya elimu mijini na vijijini, ndio maana hatuna budi kuipongeza na kuiunga mkono.

Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Dismas Prosper (wa pili kulia) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya KIbaha, Mhe. Nickson Simon John (kushoto) msaada wa madawati, viti na meza kwa shule tano za msingi wilayani Kibaha mkoani Pwani, vyote vikiwa na thamani ya Sh. Mil. 25. jana mjini hapa. Shule zilizonufaika na msaada huo ni pamoja na Shule za Msingi Kambarage, Lumumba, Kongowe, Bungo na Viziwaziwa.

“Pamoja na makubwa yanayofanywa na Serikali hiyo, sisi kama wadau vinara wa maendeleo tunao wajibu wa kuisapoti kustawisja jamii yetu, ambayo imeifanya NMB kuwa hapa ilipo – ikiwa ni benki kubwa na bora zaidi Tanzania, yenye mtandao mpana unaojumuisha matawi 230.

“Mheshimiwa mgeni mgeni rasmi, leo tunakabidhi msaada kwa ajili ya shule tano unaojumuisha madawati 200 kwa ajili ya wanafunzi wa Shule za Msingi Kambarage, Lumumba, Bungo na Kongowe – zinazopata madawati 50 kila moja, huku Viziwaziwa ikipata viti 16 na meza nane za walimu.

“Ni vifaa vyenye thamani ya Sh. Mil. 25, ambayo ni sehemu ya Sh. Bilioni 6.2 tulizotenga kwa ajili ya Programu ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI), ambayo imekuwa na utaratibu endelevu wa kutoa asilimia moja ya faida yake kwa jamii, tukifanya hivyo kwa miaka saba mfululizo,” alisema.

Akipokea msaada huo, DC Nickson aliishukuru NMB kwa msaada huo unaoenda kuwatoa sakafuni wanafunzi 600 na kuwaketisha madawatini, huku akibainisha kuwa Serikali pekee haiwezi kumaliza kwa uharaka na wepesi changamoto zinazokwaza sekta hiyo, hivyo inahitaji nguvu za wadau.

“Nianze kwa kuishukuru NMB, ambayo yenyewe na Serikali tumekuwa mapacha, katika muda mfupi wa takribani miezi mitatu, nimeshiriki matukio mengi ambayo yamepewa nguvu na benki hii.

“Tulikuwepo kwenye mazingira ambako mlitoa mchango mkubwa wa upandaji miti, katika siku ya walimu mkaja na huduma maalum ya NMB Mwalimu Spesho na leo tuko nanyi mkikabidhi madawati ambayo yatawasaidia wanafuzi 600, watatu katika kila dawati moja.

Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Dismas Prosper (awa pili kulia) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya KIbaha, Mhe. Nickson Simon John msaada wa moja ya viti na meza kwa shule tano za msingi wilayani Kibaha mkoani Pwani, vyote vikiwa na thamani ya Sh. Mil. 25. jana mjini hapa. Shule zilizonufaika na msaada huo ni pamoja na Shule za Msingi Kambarage, Lumumba, Kongowe, Bungo na Viziwaziwa.

“Mnachokifanya mnaunga mkono juhudi za Dokta Samia Suluhu Hassan, ambaye amefanya makubwa katika elimu Tanzania, na hapa Kibaha pekee kwa mfano mwaka huu ametuwezesha kujenga sekondari mpya mbili, shule za msingi mpya mbili na tumeajiri walimu wapya 900.

“Kwa hiyo juhudi zinazofanywa na Serikali, ukaja kupata mdau kama NMB, unarahisisha na kuboresha mazingira ya ufundishaji kwa walimu na kujifunzia kwa wanafunzi. Serikali pekee haitoshi, hivyo yenyewe ‘inapo-play part’ yake, na wadau ‘waka-play part’ yao, tunafanikisha elimu bora.

“Tumesikia changamoto ya madawati hapa Kambarage kama yalivyoainishwa na Mwalimu Mkuu (Happiness Msaki), ina maana yaliyotolewa na NMB yamevuka nusu ya uliokuwa upungufu. Tungetarajia kuona mdau akitoa asilimia 20 au 25, lakini NMB imetoa zaidi ya asilimia 50,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya KIbaha, Mhe. Nickson Simon John pamoja na Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Dismas Prosper wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi na walimu mara msaada wa madawati, viti na meza kwa shule tano za msingi wilayani Kibaha mkoani Pwani, vyote vikiwa na thamani ya Sh. Mil.25.

By Jamhuri