Na Allan Vicent, JamhuriMedia, Tabora

Jamii imetakiwa kuwa mstari wa mbele kulinda usalama wa miundombinu ya reli inayoendelea kujengwa na serikali kwa mabilioni ya fedha ili kuepusha uharibifu unaofanywa na watu wasio na nia njema.

Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Uyui Zakaria Mwansasu alipokuwa akifungua Maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli Kitaifa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo katika uwanja wa Chuo cha Teknolojia ya Reli mjini hapa.

Amesema kuwa usalama wa reli ni suala mtambuka linalohitaji ushirikiano wa wananchi wote ili kuhakikisha miundombinu inayoendelea kujengwa na serikali ikiwemo reli mpya ya kisasa ya SGR inaleta tija kwa uchumi wa taifa.  

Amesisitiza kuwa ili usafiri wa reli uendelee kuwa salama na kuleta tija kubwa, serikali ilitunga sheria namba 10 ya mwaka 2017 ili kulinda miundombinu hiyo na kudhibiti vitendo vyovyote vya hujuma kwenye reli.

Aidha sheria ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ya mwaka 1995 imeainisha jukumu la serikali kuchukua hatua stahiki na udhibiti dhidi ya vitendo vya uhalifu na uhujumu wa miundombinu hiyo.

‘Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika miundombinu hii, naomba kila mmoja akawe raia mwema wa kulinda miundombinu hii na kutoa taarifa punde anapoona mtu yeyote anafanya hujuma inayohatarisha usalama wa reli’, amesema.

Mwansasu amebainisha kuwa serikali iliamua kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA) ili kuhakikisha kanuni na taratibu za usafiri zinazingatiwa ili wananchi wapate huduma bora za usafiri na miundombinu mizuri.

‘Nawapongeza LATRA kwa hatua wanazochukua dhidi ya vyombo vya usafiri vinavyokiuka taratibu, kufuatilia mienendo ya vyombo hivyo na kuweka utaratibu mzuri wa usafiri ili kulinda usalama wa abiria na kudhibiti ajali’, amesema.

Ameelekeza Shirika la Reli nchini (TRC) kuendelea kuboresha utaratibu wa ukataji tiketi za mtandao ili kuwaondolea usumbufu wananchi, aidha alishauri mifereji iliyopo pembezoni mwa barabara kuzibuliwa ili kuepusha uharibifu wa reli.

Mwenyekiti wa Bodi ya LATRA Profesa Ahmed Mohamed alipongeza Wizara ya Uchukuzi kuandaa maadhimisho hayo ya wiki ya usalama wa reli na kubainisha kuwa ni fursa muhimu sana kwa wananchi kutambua umuhimu wa reli hiyo.

Ametoa wito kwa jamii kulinda miundombinu hiyo na kukemea wanaotaka kuiharibifu ili kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inayosema ‘Usalama Unaanza na Wewe, Chukua hatua’.

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuimarisha usalama wa reli ili uwe bora na salama kwa watumiaji wote ili kuchochea kasi ya uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla na kuongeza kuwa elimu ya usalama wa reli itaendelea kutolewa.

Kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kuwa Oktoba 13, 2023katika uwanja huo.

By Jamhuri