Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dodoma

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa kushirikiana na Kampuni ya Tukutech Company Ltd kutoka Tanzania, Zanifi Enterprise Ltd kutoka Zambia na Radai OY kutoka Finland zinakusudia kurusha ndege nyuki (drone) angani kwa ajili ya kufanya majaribio ya utafiti wa miamba na madini katika eneo la Mirerani kwa kutumia teknolojia ya High Resolution Airborne Geophysical Survey.

Akizunguza katika semina ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyofanyika Dodoma mwishoni mwa wiki jijini, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema dhamira ya serikali ni kuona Tanzania inafanyiwa utafiti wa kina kwa asilimia kubwa huku wizara hiyo ikiwa imekuja na Ajenda ya Vision 2030 (Madini ni Maisha na Utajiri) kwa kufanya tafiti kwa njia ya jiofizikia kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 na kwa sasa ni asilimia 16 pekee iliyofanyiwa utafiti huo.

“GST ni moyo wa Sekta ya Madini, uwepo wa taarifa sahihi za kijiolojia ya miamba na madini ndiyo imebeba dhana ya utajiri wa Tanzania, hivyo niwaombe wajumbe wa kamati hii tuisaidie GST iwezeshwe kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu,” amesema Mavunde.

Awamu ya kwanza ya majaribio ya tafiti za miamba na madini ilifanyika mwaka jana (2023) katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga na Geita na awamu ya pili inafanyika eneo la Mirerani, Simanjiro mkoani Manyara, Mkoa wa Lindi na Mtwara.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dk. Suleiman Serera, ameipongeza Wizara ya Madini kupitia GST kwa kutekeleza kwa vitendo dhana ya Vision 2030 ikiwa ni pamoja na kuratibu mpango wa utafiti ndani na nje ya ukuta wa Magufuli Mirerani.

“Utafiti wa madini nchini Tanzania unatoa mazingira mazuri ya uwekezaji na mazingira mazuri ya uendeshaji katika Sekta ya Madini, na kuna uwezekano mkubwa wa kugundua maeneo mapya kwa sababu maeneo mengi bado hayajafanyiwa utafiti wa kutosha,” amesema Dk. Serera.

Akizungumza katika eneo la Utafiti, Kaimu Mkurugenzi wa Kanzidata ya Taifa ya Rasilimali Madini, Hafsa Maulid, amesema GST imejipanga kikamilifu kutekeleza kwa vitendo dhana ya Vision 2030 kwa kufanya tafiti za kina kwa njia ya jiofizikia angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 kama ajenda ya wizara inavyosema.

Amesema GST itaendekea kushirikiana na taasisi nyingine za utafiti ili kutengenezea kanzidata ya taarifa sahihi za kijiolojia kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

By Jamhuri