Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Ikiwa ni Mkutano wa mwaka wa vyombo vya Utangazaji nchini,Wadau wa vyombo vyombo hivyo wametumia dakika tano kumuenzi aliyewahi kuwa Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania Edward Lowassa ambaye alifariki dunia February 10,2024 akiwa anapatiwa matibabu jijini Dar es Salaam.

Hayo yamejiri leo February 13,2024 jijini hapa kwenye tukio la kipekee linaloandaliwa kila mwaka na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania la vyombo vya Utangazaji ambapo wadau walisimama kwa dakika tano kama ishara ya kukumbuka mchango wa kiongozi huyo anayetarajiwa kuzikwa jumamosi Wilayani Monduli.

Pamoja na mambo mengine Mkutano huu wa kila mwaka ulizinduliwa mwaka 2007 na umekuwa jukwaa muhimu linalowakutanisha watoa huduma za Utangazaji nchini, ikiwemo sekta ndogo ya Utangazaji wa redio, televisheni, watoa maudhui ya televisheni kwa njia ya waya ,Wakusanyaji na Wasambazaji wa Maudhui ya Utangazaji, Watoa huduma za maudhui mtandaoni, Waandaji Binafsi wa maudhui, pamoja na wadau wengine wote wa sekta ya utangazaji.

Mkutano huo pia unajumuisha uwasilishaji wa mada mbalimbali zinazohusu sekta ndogo ya Utangazaji kutoka kwa wadau wa sekta ikiwa ni pamoja na mijadala inayogusa masuala mbalimbali, fursa za kuuliza maswali na kupata majibu, pamoja na upatikanaji wa miongozo na uelewa wa kina kuhusu Sheria na Kanuni zinazosimamia sekta hiyo.

Lengo kuu ni kuwezesha mazungumzo yenye tija na kujenga uelewa wa pamoja kati ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, ambayo ni Msimamizi wa sekta ya Utangazaji, na watoa huduma za Utangazaji, ambao wana leseni za kutoa huduma za Utangazaji kwa jamii nchini.

Mkutano huu pia hutoa jukwaa la kipekee kwa ajili ya kuweka mikakati ya pamoja, inayolenga kuboresha na kukuza maendeleo ya sekta ya Utangazaji.

ABC inachukua jukumu la kuwa daraja la kuunganisha pande zote za sekta ndogo ya Utangazaji, ikifungua mlango wa ushirikiano wa kina na ufanisi wa sekta ya utangazaji nchini.

Ikumbukwe kuwa Tangazo la kifo cha Lowassa lilitangazwa na Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt Philip Mpango kupitia televisheni ya taifa, ambapo alieleza kuwa Lowassa amefikwa na umauti katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

”Amefariki leo akipatiwa matibabu kwa ugonjwa wa kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu. Hayati Ngoiyai Lowassa ameugua kwa muda mrefu na amekuwa akipatiwa matibabu tangu tarehe 14 mwezi Januari mwaka 2022”. Alisema Dkt. Mpango

By Jamhuri