Na Magrethy Katengu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kamati ya Kupitia Kitita cha Mafao cha NHIF cha mwaka 2023 imesema hakuna Mtanzania atakayekosa matibabu kwa kuwa mkataba baina ya mfuko na watoa huduma za afya wa sekta binafsi (APHTA) haujavunjwa.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Februari 29 Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt.Baghayo Saqware amesema maboresho ya kitita cha mafao cha mwaka 2023 yalianza tangu mwaka 2018 kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Afya iliyoelekeza mfuko kufanya mapitio ya kitita na bei zake kwa kuzingatia mwongozo wa matibabu nchini toleo la mwaka 2017.

Kitita hicho kimepangwa kuanza kutumika Machi Mosi, 2024 lakini APHTA walikaririwa na vyombo vya habari wakisema watashindwa kutoa huduma kwa kuwa mazungumzo yao na kamati hayakufikia muafaka lakini ilikuwa huru kumsikiliza kila mtu na kwamba walikubaliana kwa pamoja na kuamua kitita kianze kutumika kwa faida ya pande zote.

“Tulitumia vigezo vyote kushughulikia malalamiko ya watoa huduma hao na hatujamwonea mtu yeyote, bei zetu sasa zina vigezo ambavyo vilikubaliwa kwa pamoja tuliwashirikisha. Huduma zitaendelea kutolewa kwa sababu mkataba na APHTA haujavunjwa.

“Nawahakikishieni hakuna mtoa huduma atavunja mkataba na NHIF, tunahitaji mfuko uwe endelevu na wenzetu waliowekeza wawe endelevu, sisi tuko tayari kusikiliza kwa hoja kwanini wanasema wanapata hasara…wasitie watu hofu kama mtu anahisi hiki kitita hakitaki asilete taharuki haya ni mambo ya mkataba,” amesema Dk. Saqware.

Hata hivyo Kamati hiyo imeitaka Wizara kupitia NHIF iendelee na utekelezaji wa kitita cha mafao kilichoboreshwa cha NHIF cha mwaka 2023 kama walivyoshauri na kusisitiza kama itatokea mwanachama akakosa huduma atoe taarifa katika mamlaka husika

By Jamhuri