Hapi, Waitara wanyukana

*Hapi: Hii ni vita, mimi mtoto

 wa mjini wameshindwa kunizunguka 

*Asema kelele ni nyingi kwa kuwa ameziba mirija ya wizi

*Waitara: Siogopi kifo kiwe cha risasi au sumu, Wakurya si ‘maboya’

*Asema RC hana mamlaka ya kuvunja CDC, adai amefanya ubadhirifu wa fedha za madawati 

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Vita ya maneno, mikwara, majigambo, ubabe na vitisho imeibuka kati ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi, dhidi ya Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara.

Kisa cha vita hiyo ni tuhuma za ubadhirifu wa fedha kwa ajili ya uwajibikaji (CSR) kutoka Mgodi wa Barrick North Mara na kusababisha Hapi kuivunja Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) iliyoundwa ili kupanga na kusimamia matumizi yake kwa lengo la kutekeleza miradi ya maendeleo.   

Hapi atema cheche

Akizungumza katika kikao kilichofanyika Aprili 20, 2022 na kuhudhuriwa na karibu viongozi wote wa mkoani humo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa kamati iliyoundwa na ofisi yake kwa ajili ya kuchunguza matumizi ya fedha za CSR, Hapi, amesema anajua kinachopiganwa sasa hivi ni vita ya masilahi, kwa kuwa ameziba mirija ya watu.

“Najua ni vita, hii ni vita, na ninaelewa vita hii inayopiganwa ni vita ya masilahi. Nimeziba mirija ya watu. Hivi haya niliyoyaeleza hapa kuna jambo gani nimelieleza la familia yangu au langu binafsi, kwa nini nipigwe vita? Ukishazuia mrija wa watu ni lazima vita itakuja tu,” amesema.

Pia amesema hawezi kukubali wizi wa fedha hizo ukapita katika mikono yake kwa kuwa yeye ni mkuu wa mkoa ambaye ni mtoto wa mjini na wameshindwa kumzunguka. 

Amesema ana taarifa zote kuhusiana na jambo hilo hadi watu walioahidiwa fedha katika ununuzi na yuko tayari kutetea uamuzi wake popote.

“Nisingekuwa mkuu wa mkoa, mtoto wa mjini imara wangeweza kunizunguka, ningekuwa kama sijalelewa katika chama. Rais ametoka amenipa maelekezo ya hadharani na ya ndani. Anayeuliza nani ni mkuu wa mkoa mwambieni mimi ndiye mkuu wa mkoa hapa na nimewekwa kwa mujibu wa sheria na Katiba,” amesema na kuongeza: 

“Wizi huu hauwezi kupita mikononi mwangu kamwe. Nataka niwaambie, kelele za chura hazitamzuia tembo kunywa maji. Ninazo baraka za sheria, ninazo baraka za aliyeniteua, nitasimamia utaratibu. 

“Nataka kuwapa habari za mwisho CDC. Kwa kuwa hakuna sheria yoyote na kwa ubadhirifu uliotajwa kuanzia sasa nimevunja CDC yote mkatafute kazi nyingine na mamlaka nayarejesha katika vyombo vya serikali.” 

Vilevile amesema amefanya ziara mkoani humo na kugundua kuwa jinsi fedha za CRS iliyopita zilivyotumiwa, kufanyiwa kazi na kutekelezwa ni wizi mtupu, kwa kuwa miradi yote ya maendeleo ilikuwa ya ovyo na fedha za wananchi zimeliwa.

Katika miradi hiyo amesema kuna baadhi ya vifaa vya ujenzi kama nondo zinabaki na hazitumiki na saruji inaganda na hawezi kukubali, kwa kuwa hiyo ni fedha ya umma na wananchi wanyonge na atasimama imara kwa niaba yao.

Amesema anachotaka kama wakikubaliana mradi ujengwe na ukamilike na watu wasigeuze fedha za ujenzi wa kituo cha afya posho za kulipana kwenda kuhudhuria kesi mahakamani.

“Hiyo hatuwezi kukubali na kuna kituo cha afya kinajengwa kule kwa Sh milioni 500. Kuna kituo cha afya kingine zimefika Sh milioni 800 hakijakamilika, tunachekaje na watu wa namna hiyo?” amehoji na kuongeza:

“Tunataka mipango ifuate utaratibu na serikali ina sheria na taratibu zake, tunataka tudhibiti wizi. Ukisema unalipa ada, unamlipia nani, tujue hayo majina ya wananchi wanaolipiwa ada, tukawatafute shuleni tuwakute wanasoma.

“Siyo unatuambia umepanga Sh milioni 46 unalipa ada lakini hutuambii unamlipia nani, ni mtoto wa mjomba wako, ni nani? Kwa hiyo mimi kwa niaba ya serikali nataka niwahakikishie wananchi, tunataka maisha yenu yaboreke, tunataka miradi isimame lakini fedha zisitumike.”

Amewaonya wananchi wasitumike kama kichaka cha watu kuiba fedha, kwa kuwa wana shida na yeye hawezi kuruhusu ziibwe kisha baada ya miezi sita wakute zote zimekwenda katika mikono ya watu.

Amesema hilo hawawezi kukubali na hata migodi haiwasaidii na akauliza swali kama kuna mwanamume au mwanamke anaweza kusimama amuone akiri kwamba CSR iliyopita imewasaidia, lakini hakuwapo mtu huyo. 

Ametolea mfano kwa kusema kuwa huo ni wizi kwa sababu kuna madarasa mawili yalikuwa yanajengwa na zimebaki nondo 900 na akahoji wataalamu wao wamekuwa mufilisi kiasi hicho? 

“Mimi na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa tutasimamia masilahi ya watu, tunachotaka tu fedha ipangwe kwa utaratibu na iende kutatua shida za wananchi,” amesema na kuongeza: 

“Leo hii kuna watu wana fedha za CSR za mwaka 2019 kwa ajili ya miradi ya maji, wanaandika katika jedwali fedha tuliyonayo ni Sh milioni 300, mradi bado haujaanza kutekelezwa, tunaomba tena tuongezewe sijui Sh milioni 30 na ngapi?

“Hivi wewe una miaka miwili una Sh milioni 300 haujazitumia kwa wananchi, unataka tukuongezee fedha nyingine tena, siwezi kubariki wizi wa namna hiyo kwa wananchi.” 

Amesema hakubali ujanja ujanja, michongo, wizi kwa kutumia majina ya wananchi waibiwe, kwa sababu wakiruhusu serikali ndiyo itakayotukanwa na si Mgodi wa North Mara.

Katika hatua nyingine, amesema CDC ilikuwa inatekeleza mradi mmoja kwa gharama mbili tofauti? 

“Wakaendelea tena kisima kirefu shule nyingine ya Bichune baadaye wakaja ujenzi wa maabara mbili Sh milioni 88, sehemu nyingine huku ujenzi wa maabara mbili Sh milioni 90, sehemu moja nyumba ya watumishi mbili kwa moja Sh milioni 100,” amesema na kuongeza:

“Sehemu nyingine Sh milioni 163, yaani ni kitu kimoja lakini kinajengwa kwa gharama mbili tofauti. Yaani CDC kwenye kata moja anajenga nyumba mbili kwa moja kwa Sh milioni 100 na katika kata nyingine anajenga nyumba mbili kwa moja kwa Sh milioni 163 yaani ramani ile ile, vyoo vilevile, halmashauri ile ile.

“Yaani wewe una Sh milioni 300, huo mradi haujaanza halafu unaomba unataka madiwani na mkuu wa mkoa tukupitishie milioni 27 tena, basi nitakuwa mkuu wa mkoa wa michongo.”  

Kuhusu ada za watoto kutengewa Sh milioni 46, akahoji ni watoto gani waliotengewa, kwa kuwa majina hakuna, pia katika huduma za afya kwa nini CDC wamejitengea Sh milioni 53.8 lakini hakuna ufafanuzi wa matumizi ya fedha hizo?

Pia amehoji kuhusu ujenzi wa Chuo cha VETA uliotengewa Sh milioni 400 na akamuuliza Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mara kama ana maelekezo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

“Ukitaka kujenga vitu kama VETA lazima muwasiliane na Wizara ya Elimu, lazima upate kibali kwa sababu VETA itaajiri walimu, mafundi, je, ipo katika mpango wa serikali au tunakwenda kujenga gofu, BoQ imetoka wapi?” amehoji.

Amesema CDC ina jumla ya salio la fedha lililobaki kwa mwaka 2021 la Sh bilioni 1.248 lakini wanaomba tena mkoa ubariki kuruhusu kutoa Sh bilioni 1.2.

“Kama tukipitisha hii chama kitaendelea kutukanwa, kubezwa na kunyooshewa vidole na wananchi. Usifikiri wewe mwenyekiti wa UVCCM ndiye kijana peke yako, mimi nimelelewa na chama hiki, nina uchungu, msije mkadhani kwa sababu mtu unaitwa mwenyekiti fulani ukadhani wewe ndiyo una uchungu zaidi na nchi hii, hakuna, nchi hii ni yetu sote,” amesema. 

Mbali na hayo, amesema hata CDC iliyoasisiwa hapo awali anairudisha katika halmashauri na akamtaka mwenyekiti na watalamu wake wakae na kujiridhisha, kwa kuwa wana mamlaka ya kupanga maendeleo ya wananchi kwa kufuata sheria.

“Nairudisha kwenu, kwa hiyo mwenyekiti wa CDC na katibu wa CDC kuanzia sasa biashara imeisha na mkawaambie wale wajumbe 200 wakatafute kazi ya kufanya. Hatuwezi kukubali mambo ya kihuni yafanyike,” amesema na kuongeza: 

“Vyombo vya dola, Polisi Kanda Maalumu, Takukuru na vyombo vingine ripoti mnayo na hawa ambao wamekaa na kwenda kupanga matumizi ya fedha za umma CDC nataka mpate maelezo yao. Viongozi wa CDC wote waje fungueni majalada ya uchunguzi. Na uchunguzi ule wa Takukuru nimeona mnachunguza sijui nani, uchunguzi uanzie na CDC iliyopita.

“Wamepata wapi mamlaka ya kisheria ya kupanga bajeti za serikali? Anzisheni uchunguzi wakatoe maelezo. Kikundi cha watu 200 kinakaa kupanga mabilioni ya fedha, na humo ndani kuna mirija na mianya ya watu. CDC viongozi wake, mwenyekiti, katibu, msaidizi wa katibu, Jeshi la Polisi na Takukuru fungua jalada pata maelezo yao.”

Amesema wao wana halmashauri na Tarura wanaofanya kazi kwa mujibu wa sheria lakini akahoji CDC inafanya kazi kwa sheria gani na kuweza kupanga matumizi ya fedha za umma?

Katika hatua nyingine, amesema CSR si sadaka, si kishika uchumba, bali ni sheria. Kisha akazipa kampuni za uchimbaji madini mwezi mmoja wa utekelezaji na kuwataka kuacha ujanja ujanja.

Amesema suala hilo analirudisha kwa halmashauri na akamuagiza Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) kutoa muda maalumu.

Amesema hata mwenyekiti akitaka akae na halmashauri ya kijiji ilete maoni, iende kata nayo ilete maoni na wataalamu wawachambulie BoQ na  kila kitu kisha watengeneze bajeti ya fedha halafu waone kama yeye atazuia.

Amesema hata kesho wakileta ataipitisha lakini si hiyo, kwa sababu kuna zaidi ya Sh bilioni moja wamechambua na wataalamu wake na kuna karibu Sh bilioni mbili zinakwenda kwa ujanja ujanja katika mifuko ya watu na malipo hewa.

“Mimi siwezi kupitisha hiki kitu, kule kuna North Mara Trust Fund inasaidia kusomesha hawa watoto, sasa wanachofanya wenzako wanaingiza yenyewe inaonekana mafungu mawili yanafanya kazi moja,” amesema.             

Waitara ajibu mapigo

Akizungumza katika kikao kilichofanyika Aprili 25, 2022 na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa vijiji, Waitara, amesema uongo ukisemwa sana unageuzwa kuwa ukweli na yeye kama mbunge akaamua kujibu mapigo kwa sababu madhira mengi ya Nyamongo anayafahamu kwa muda mrefu wala si leo.

Amesema ameanza kushughulika na mambo hayo kabla hajawa mbunge wa eneo hilo, kwa sababu anayafahamu tangu miaka ya nyuma, kwa kuwa alikuwa anakwenda katika eneo hilo.

Amesema changamoto za eneo hilo zinafahamika na anazijua na anashangaa kwa nini kuna mambo yanakwama bila sababu wakati fedha zipo.

“Sioni sababu zozote kwa nini mambo yakwame katika eneo ambalo fedha zipo, watu wapo na changamoto zipo lakini mambo yanakwama na nilipoona kuna mambo yanazungumzwa ya uongo, tena yanazungumzwa na viongozi nikaona ninao wajibu kama kiongozi,” amesema na kuongeza:

“Kama Mtanzania kuwaeleza watu ukweli ili kuwasaidia Watanzania wa Nyamongo na Tarime Vijijini na nitausaidia pia Mkoa wa Mara kutoendelea kupotoshwa, na viongozi wengine wa nchi hii wajue ukweli ukoje.

“Tarehe 20, 2022 kikao kiliitishwa na RC Hapi, kikao kile, mimi nimekuja hapa tangu maadhimisho ya miaka 100 ya Mwalimu Nyerere, niliondoka Dodoma tangu tarehe 12 na hadi leo sijarudi, sasa nilipokuja nikaambiwa kuna kikao kimeitwa Musoma na ajenda mojawapo ni kuzungumza habari za fedha za CSR.

“Nikasema nitakuwapo hapa wakati nasubiri kikao hicho, nitakuja Nyamongo nisikilize changamoto zote zilizoibuliwa na wenyeviti na madiwani.” 

Hata hivyo, amesema hakupata mwaliko wa kwenda katika kikao hicho licha ya kuwapo kwa barua iliyoandikwa Aprili 12, 2022 ya kuwaalika wajumbe wengine. 

Baada ya kusikia taarifa ya kikao hicho cha kujadili mambo ya CSR akahoji mbona wabunge hawajaalikwa wakati Mwenyekiti wa Halmashauri, DC na DED wamealikwa?

Amesema alifuatilia mwaliko wa kikao hadi Aprili 19, 2022 saa tatu asubuhi akatumiwa barua iliyoandikwa Aprili 12, 2022 na akagundua wakuu wote wa wilaya, wakurugenzi wote, wenyeviti wa halmashauri zote, wachimbaji wote wa madini wa Mara na viongozi wa dini wamealikwa lakini madiwani wa Tarime ambao ndio wenye miradi ya maendeleo katika halmashauri hawajaalikwa.

Pia amesema wajumbe wa CDC hawakualikwa kwa sababu aliitwa mwenyekiti tu na kulikuwa na sintofahamu ya kikao hicho na ajenda zake.

Amesema alichofanya Hapi ni kumshambulia yeye baada ya kuongea na wananchi wake wenye changamoto za malipo, fidia na shida ya maji. Amesema hayupo tayari kuona mamlaka ya halmashauri yakipokwa na Hapi.

Vilevile amesema Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye, maarufu kwa jina la ‘Namba Tatu’ alipopewa nafasi alisema wao wanaropoka na yeye anaipinga serikali ya CCM.

“Kana kwamba sijui ninachofanya ni kitu gani. Sasa katika mjadala Hapi aliposimama kuzungumza alisema mambo mengi na akatoa taarifa ya kamati ya uchunguzi iliyoundwa na mwenzake aliyekuwa RC, akazungumza peke yake mwanzo hadi mwisho,” amesema na kuongeza:

“Inaonekana alinishambulia na wakati fulani akatoa tuhuma kana kwamba mimi na madiwani tunakula fedha za mgodi na hata hii CDC ni wabadhirifu sana, wameiba sana na hiyo ndiyo ilisambaa katika jamii kuwaaminisha watu kwamba hawa ni wabaya kweli kweli. 

“Sasa mimi nimefanya uchambuzi wa namna ambavyo mambo yalivyozungumzwa katika mkutano ule. Ni vizuri Watanzania wakajua kwamba watu wa Mara na watu wa Nyamongo ni lazima washituke kwa sababu uking’atwa na nyoka hata ukiona jani unashtuka.”

Amesema mwaka 2019 alikuwa Naibu Waziri wa Tamisemi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, aliitisha mkutano Musoma akawaambia Ma-DC na Ma-DED wapeleke vipaumbele na akachukua fedha za CSR ambazo ni halali kwa watu wa Nyamongo na halmashauri zetu akazigawa kama mali yake binafsi.

Amesema Malima alizigawa Sh milioni 200 na Sh milioni 300 kama njugu na zikaisha na akatoka Musoma akaenda Dodoma akazitengenezea bajeti kwa kuzigawa bila ya kuzungumza na watu wenyewe wa eneo hilo, bila kuongea na madiwani na bila hata ya kuomba ushauri.

Amesema kwa kuwa yeye alikuwa Naibu Waziri akazizuia fedha hizo na hadi Malima ameondoka Mara hawasalimiani.

Amesema kosa lake kubwa hadi kufikia hatua hiyo ni kwa nini fedha za Nyamongo zigawanwe mkoa mzima wakati Buhemba kuna machimbo na Serengeti wanapata CSR ya hifadhi lakini wao hawapati mgawo na ukienda Musoma Vijijini kuna machimbo nako hawapati.

Pia amesema pale Musoma Mjini wana minofu ya sangara lakini nako hawapati mgawo na watu wa Tarime na Nyamongo wana haki ya kushtuka kutokana na malumbano hayo kwa sababu huko nyuma wameshazoea kudhulumiwa haki yao. 

Amesema fedha hizo zinazosemwa na Hapi zilikuwa za mwaka wa 2019/2020 kwa ajili ya kufanya miradi ya CSR na wakati huo hakuwa mbunge wa Tarime Vijijini wala madiwani wa sasa hivi hawakuchaguliwa wakati huo kuongoza halmashauri na kamati zilizoundwa hazikuwepo.

Amesema wakati huo zilikuwa ni kamati za Chadema na mbunge wa Chadema na alichokifanya katika miradi iliyoibuliwa wakati huo ni kusaidia fedha hizo zije kwa haraka na zikaja.

Aidha, amesema wenyeviti wakaibua miradi na waliosimamia ni halmashauri ya Chadema na DC na RC hawawezi kujitoa katika lawama.

“Kama kuna miradi imekwama ni vizuri tukapiga mstari kwamba madiwani wa CCM na mbunge hatukuwepo wakati huo na Oktoba, 2020 ndipo tulipata uongozi na kwa maana ya serikali tumeanza kazi mwaka 2021.

“Kama kuna fedha ya kwanza ya kujadili miradi ya maendeleo ni ile iliyotolewa na mgodi sasa hivi ya Sh bilioni 5.6 za mwaka wa fedha uliopita lakini zipo nyingine zingeweza kutolewa zaidi ya Sh bilioni tano ambazo ukijumlisha ni kama Sh bilioni 11.6 zipo kwenye mgodi.”

Amesema hadi sasa miradi yote ya CSR imesimama Tarime kwa sababu Hapi ameandika barua ya kuizuia. 

Amesema anao muhtasari wa kikao cha Januari 31, 2020 kilichoitishwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mtemi Msafiri na watu waliohudhuria ndio mahususi waliokwenda kupanga miradi iliyopo leo, mafundi walipatikanaje, vifaa, nani anasimamia miradi wakazungumza wao watu 23 na hakuna mwenyekiti wa kijiji aliyehudhuria.

Amesema hata vifaa vyote vya ujenzi kununuliwa kutoka mjini walipanga wao na wakajadili mafundi wengine watoke mjini.

“Kwa mfano roli moja la mawe hapa vijana watapasua watakuuzia kwa Sh 120,000 lakini wao walisema Sh 360,000 na wenyeviti wakakataa na waliopendekeza yote hayo ni Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.

“Lakini leo Hapi hafahamu anasema eti CDC ndiyo iliyojadili miradi na yalikuwa ni maagizo, walikuta wao DC, DAS na wakurugenzi wawili wakapitisha na miradi yote ikaanza kutekelezwa,” amesema. 

Katika hatua nyingine, amesema sheria ya uwapo wa RC na DC, kifungu kidogo cha tano (1, 2 na 3) inasema kazi yake ni kusaidia Serikali za Mitaa zitimize wajibu wake na kutoa mazingira wezeshi ya kukamilisha miradi ya maendeleo.

Amesema sheria hiyo haisemi kwamba RC ataingilia kwa ujumla miradi yote na taarifa zote za CDC za wizi na ubadhirifu ni za uongo.

“Nilisema nitasema jambo hili hadharani na nitaonyesha kwa nini Hapi ni muongo na bahati mbaya kwamba kiongozi aliyepata dhamana ya kuteuliwa kati ya wachache halafu unaita mkutano mkubwa wa mkoa unatoa taarifa za uongo kana kwamba wale watu ni wajinga hawawezi kusema,” amesema.

Vilevile amesema hawawezi kuubadili uoga ndio ukawa ni mtindo wa uongozi, kwa kuwa kuna mtindo wa viongozi wakija Mara wanadhani watu wote ni ‘maboya’.

“Yaani hapa ni kama kuna wanyama tu, wakati wao wanasomesha vijana wao wanadhani sisi hatupeleki watoto shuleni, Hapi anatengeneza mgogoro ambao hataweza kuumaliza, kwa sababu Nyamongo kuna wasomi na wakianza katika huo mgogoro hawezi kuutatua,” amesema.

Kuhusu Hapi kuzuia fedha, amesema wakati anatoa matamko mengi na majigambo alisema sheria inampa baraka pia Rais Samia Suluhu Hassan amempa baraka lakini atawaeleza madudu yake akiwa ndiye RC kisha waulizane.

Amesema baada ya kuulizana ndipo wajue kwamba je, hizo ndizo siri alizopewa kuja kuzifanya Mara?

Amesema CDC iliibua miradi katika vijiji 11 na si halmashauri nzima kama anavyodai Hapi. 

“Hawa walibua miradi katika vijiji vyao na kata zao zinazozunguka Mgodi wa North Mara na vijiji vingine madiwani waliibua miradi katika kata zao halafu taarifa zote zilikwenda katika chombo cha wataalamu kinaitwa CMT, kwamba kuna shida ya shule, kuna nini wakachakata wenyewe,” amesema na kuongeza: 

“Kwa hiyo si kweli kwamba CMT haikujadili miradi ya Tarime ambayo Hapi anaizuia, ni muongo, walijadili tena unaweza kupeleka mradi wa Sh milioni 500 wakachakata hadi wanapata Sh milioni 70 au 80. 

“Lakini kamati ya fedha ya halmashauri ilijadili nyaraka hii ya miradi na baada ya hapo ikaenda baraza la madiwani kujadili na imepitia hatua zote kutoka kuibuliwa, ngazi ya CMT, kamati ya fedha na baraza likapitisha na kukawa na mawasiliano kati ya halmashauri na Tamisemi.”

Amesema kulikuwa na mjadala mkubwa na haukuishia hapo na barua iliyokwenda Tamisemi aliyeisaini ni RAS na maana yake Hapi alikuwa na taarifa ya hii miradi.

“Hapi anaijua hii miradi kupitia RAS na anajua sheria na nikauliza pale mkoani hata wale wanasema kuna mtu wa miundombinu wa serikali za mitaa na wanasheria hawakuulizwa, alikaa na watu wa ulinzi na usalama akatoa uamuzi wake bila kushirikisha.

“Kama Hapi angemuuliza RAS wake angemsaidia vizuri na sisi tulikuwa tayari kujadiliana kumwambia namna ya kwenda mbele, sisi Mara tunataka maendeleo yaje kwa kasi,” amesema.  

Kuhusu madudu ya Hapi katika zabuni ya madawati, amesema alitoa agizo yote yatengenezwe Musoma na mzabuni anamjua yeye. 

“Mimi nimepokea malalamiko kwamba haya madawati ni ovyo, picha ninazo na baada ya muda mfupi nitaziachia katika mitandao. Baadhi ya shule hadi leo hazijapata madawati, Kemambo Sekondari ni hapo tu Nyamongo lakini leo hawajapata madawati pamoja na kwamba ni mabovu walimu wanalalamika, madiwani wanalalamika, sasa wanaogopa kwamba mbabe amekalia kiti pale mkoani na yeye ndiye anayetoa maagizo kimyakimya. 

“Hatuwezi kuacha uoga kwa mtindo wa uongozi lazima tuseme ukweli, kwa hiyo narudia madawati ya Tarime DC naomba Waziri wa Tamisemi, Waziri Mkuu na CAG huu ukaguzi unaofanywa hapa wakague tena madawati,” amesema. 

Pia amesema Hapi aliagiza mtu mmoja atengeneze kwa bei kubwa na akawataka watu waende wakapige picha waone ili isionekane anasema uongo.

Amesema Hapi ni mtu anayetaka kuwaaminisha wananchi kwamba yeye ni msafi na anatishia kwamba amekulia CCM.

“Nani ambaye haijui CCM na CCM haiwezi kuwa kichaka cha wizi, yaani watu wabovu wakivaa shati la kijani waseme wao ni malaika, hapana, anatisha watu ili atuibie, anatisha watu ili warudi nyuma atoe maelezo katika mgodi,” amesema na kuongeza: 

“Nataka niseme tu mbele ya hadhara kwamba kama mimi ndiye mbunge wa jimbo hili, hakuna mtu atachukua maelekezo kinyume cha Katiba, sheria, kanuni na taratibu tukamkubalia. Hata kama wengine wote watafyata mikia, mimi ndiye nitakuwa mtu wa mwisho. 

“Madawati yaliyotengenezwa Kelimeri C ni mabovu, yapo chini ya kiwango, hayakubaliki na fedha zimeibwa, uchunguzi ufanyike na Hapi anatakiwa awajibike kwa hilo. Alipokuwa Iringa aliwatukana wazee nasikia walimlaza makaburini.” Amesema Rais Samia alipomteua alisema kwamba anamuangalia na sasa ameanza mapema.

Pia amesema ameambiwa kwamba Hapi anasema wengine ni ng’ombe hapa Tarime na kwa kushirikiana na Namba Tatu wanapanga mgombea ubunge asiwe yeye.

Amesema hoja yake si kuwa mbunge bali watu wa Tarime watendewe haki na atakayefika huko hawaheshimu na si kuwaita ng’ombe wakati madudu yake wanayajua na watayasema mchana, usiku na kila mahali.

Amedai kuwa kwa sasa wanajipanga usalama wake utakuwa hatarini.

“So what? Mimi nilishazaliwa, nilishaoa hapa nasubiri kufa muda wowote, kwa hiyo nikifa leo, kesho, keshokutwa, nikipigwa bomu, nikipigwa risasi, nikiwekewa sumu potelea mbali. Nitasema ukweli bila kumuonea mtu na nitasema kila mahali,” amesema na kuongeza:

“Huu ni upuuzi ambao hatuwezi kuuunga mkono, mkuu wa mkoa si polisi kwetu kwamba Mara hatuna akili si kweli, halafu unawatukanaje Wakurya? Kwa hiyo nina mpango wa kuitisha wazee wote wa mila, niwaambie mimi kijana wao nimedharauliwa na RC, madiwani wangu wanadharauliwa, wenyeviti wangu wanadharauliwa.

“Wakurya wenzangu wanaitwa ng’ombe na Hapi na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa na sisi ndio tumewachagua, tuna haki sawa kama Watanzania wengine, kuwa hapa Tarime si bahati mbaya na Mgodi wa North Mara lazima utunufaishe, kama kuna jambo la kupigania ni heshima.” 

Amemuomba Rais Samia atupie jicho uongozi wa Mara kwa maana ya RC, kwa sababu huko wanakoelekea hali haitakuwa nzuri kwa kuwa watu wa Tarime na Mara hawatakuwa tayari kukashifiwa na kudharauliwa.

“Tunazo sheria, kanuni na taratibu tunazijua na wengine tumezitumia katika nafasi mbalimbali, kwa hiyo tunamuomba Rais Samia jambo hili la Mara na kama wanafikiri mimi nadanganya walete tume huru ichunguze matendo ya Hapi tangu ameingia hapa Tarime.

“Wachunguze madawati ambayo nimesema na wapitie nyaraka zote hizi halafu watangazie Watanzania kwamba Waitara ni muongo. Ni muhimu sana, tunataka wakuu wa mikoa waje Mara lakini si dizaini ya Hapi,” amesema.

Jambo jingine amesema mwenendo wa Namba Tatu wa kubadilika na kuacha kuwasemea wapiga kura wa CCM na anaelekeza tamaa zake kwa wenye fedha haukubaliki kwa kuwa wananchi wamelalamika na viongozi wao wanawasemea serikali ichukue hatua lakini yeye anawaita wapingaji wa serikali na wanapiga porojo.

Amemtaka Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Daniel Chongolo, aende Tarime na Mara akawasikilize na amemuomba mara kadhaa na akaonya kuwa ngoma ikilia sana mwisho wake inapasuka.

Jumanne ya wiki iliyopita Gazeti la JAMHURI lilimtafuta Hapi pamoja na mambo mengine kutaka ufafanuzi wa kuhusika kwake katika tuhuma za madudu zilizosemwa na Waitara lakini kwa kifupi akajibu kwamba amempuuza.

Viongozi wengine wafunguka

Mwenyekiti wa kamati za vijiji vinavyozunguka Mgodi wa North Mara, Paul Bageni, amesema miradi yote iliyoibuliwa imefuata taratibu zote kwa mujibu wa sheria na kanuni na ameshangaa wao viongozi wa CDC kuambiwa ni wezi.

Amesema wamechafuliwa ila kwa kuwa yeye ni kiongozi kuchafuliwa ni kawaida na ana tamani kwamba tume iliyoundwa kuchunguza sakata hilo anaona inachelewa na anataka iende haraka kwake ikamhoji wakati wowote.

Amesema yeye ni kiongozi hawezi kukimbia kwenda sehemu yoyote na anataka kutoa ushirikiano ili awaonyeshe kwamba yale yaliyokuwa yanasemwa na Hapi ni uongo na labda alidanganywa au hakusikiliza upande wa pili.

“Nataka hiyo tume ije ili aone je, hii tume imeniambia hivi lakini nimeshuka kule chini na hao viongozi nimeongea nao lakini hawakufaya hivyo. Nimuombe tu Hapi akiwa anafanya vitu awe anasikiliza pande zote.

“Asikilize ili na yeye apime, hata Kikwete anasema ukiambiwa changanya na zako, sasa sijajua aliambiwa halafu hakuchanganya na zake ndiyo maana akatuhukumu kwa hilo. Nimuombe awe anaangalia kuanzia kule chini kwa wadogo, awe anachukua mawaidha halafu afananishe je, kuna ukweli?” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongwe, Daudi Tembe, amesema siku za nyuma hajawahi kuona haya yanayofanyika japo Malima aliwahi kuzuia fedha za CSR.

Amesema kama alivyosema Waitara kwamba sheria ilitafsriwa wakati huo na fedha zikafanya kazi na usimamizi wa Halmashauri ya Tarime na DC akishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama walisimamia miradi ya maendeleo. 

Amesema wakati wanatekeleza hiyo miradi walikuta imepitishwa katika vijiji na wamekwenda kuisimamia.

“Kwa mfano wakati wanaleta matofali ya ujenzi wa sekondari katika kijiji changu walileta kwa bei ya Sh 2,500, niligoma kuyapokea na DC alinikamata na kuniweka ndani.

“Nikasema ni afadhali nikamatwe niwekwe ndani kuliko kununua matofali kwa Sh 2,500 wakati Nyamongo tunayanunua matofali kwa Sh 1,500,” amesema.