Na Mwandishi wetu JAMHURI MEDIA, Dar es Salaam.

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imehudumia zaidi ya wagonjwa 480 waliokuwa na changamoto ya mawe kwenye kwenye figo kwa kutumia mashine maalumu ya kuvunja mawe kwenye figo kwa kutumia mawimbi mtetemo ((Extracorporeal Shock Wave Lithotripsy-ESWL) tangu huduma hiyo ilipoanza Juni, 2020.

Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa wa Upasuaji Mfumo wa Mkojo, Dkt. Hamis Isaka alipokuwa akielezea mafanikio ya huduma hiyo ambayo kwa Hospitali za Umma hapa nchini inatolewa na MNH-Mloganzila pekee.

Dkt. Isaka amesema kupitia matibabu hayo mawe kwenye figo yanasagwa kwa njia ya mawimbi mtetemo na kuwa chembe ndogo ndogo mithili ya mchanga ambao zinatoka kwa njia ya haja ndogo.

“Kwa huduma hii mgonjwa anapata matibabu siku hiyo hiyo na kurudi nyumbani na pia hahitaji kulazwa kabla ya kufanyiwa huduma, anafika kliniki na kufanyiwa na anarudi nyumbani siku hiyo hiyo” amebainisha Dkt. Isaka

Huduma ya matibabu ya kuvunja mawe kwenye figo kwa kutumia mawimbi mtetemo inatolewa katika Kliniki ya Magonjwa ya Mfumo wa Mkojo iliyopo ghorofa ya kwanza katika jengo la Mloganzila kila siku ya Jumatatu, Jumanne, Jumatano na Alhamisi kuanzia saa 2:00 Asubuhi hadi 11:00 Jioni.