TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa vibali 157 kwa asasi za kiraia kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu kwa Wapiga kura.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa), Jacobs Mwambegele wakati akifungua mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu kwa wapiga kura mkoa wa Tanga.

Mafunzo hayo yamewahusisha Mratibu wa Uandikishaji Mkoa, maofisa uandikishaji, maofisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya Jimbo, maofisa uchaguzi, maofisa ugavi na maofisa Tehama wa Halmashauri.

Alisema wametoa kibali kwa taasisi na asasi za kiraia 42 kuwa waangalizi watakaoshiriki katika uboreshaji wa daftari ambapo kati ya hizo taasisi tisa ni za kimataifa na 33 ni za ndani ya nchi.

“Nisisitize kwa maofisa waandikishaji mnapofika kwenye maeneo yenu muwape ushirikiano kwa kuwa ni wadau muhimu na vitambulisho watakavyokuwa navyo wamepatiwa na tume ni utambulisho tosha,” alisema.

Aidha, alisema kwamba ni muhimu wakahakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa umakini katika eneo husika ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji kutokana na kununuliwa kwa gharama kubwa na vinatarajiwa kutumika kwenye maeneo mengine ya uandikishaji nchini.

“Kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa kutapelekea athari kubwa katika kukamilisha uboreshaji huo muhimu lakini pia hakikisheni mnazingatia maelekezo yote yatakayotolewa na tume ili muweze kuyafanyia kazi wakati mtakapoanza,” alisema.

Aliongeza kuwa matokeo bora ya uboreshaji huo yanategemea uwepo wa ushiriki mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji, Serikali, Vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi.

Hata hivyo alisema wakati wa uboreshaji wa daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura.

“Jambo hili ni muhimu kwani litasaidia kuleta uwazi wakati wa kazi ya uboreshaji lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea vurugu zisizokuwa za lazima,” alisema.

Mwenyekiti huyo wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi alisisitiza kwamba mawakala hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni.

“Maelekezo zaidi kuhusu mawakala wa vyama vya siasa yatatolewa na wakufunzi na ni muhimu kuyazingatia,” alisema.