Na Mathias Canal, JamhuriMedia,Simiyu

Mbunge wa Jimbo la Bariadi mkoani Simiyu Mhandisi Kundo Mathew amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa wakati.

Amesema kuwa Rais Samia amekuwa kinara kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo ambapo ametaja mafanikio ya miradi mbalimbali ikiwemo kampeni ya kumtua ndoo mama kichani ambapo upatikanaji wa maji safi na salama katika jimbo la Bariadi umeongezeka.

ENG Kundo ametoa pongezi hizo mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa baraza kuu la jumuiya ya umoja wa wanawake wa Chama Cha Mapinduzi-CCM Wilaya ya Bariadi lilifanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Alliance leo tarehe 15 Julai 2023.

Amesema kuwa kwa mafanikio ya miradi mbalimbali Rais Samia anaenda kuandika historia kubwa katika jimbo la Bariadi na nchi kwa ujumla wake.

Kuhusu sekta ya Umeme, Mbunge Kundo amesema kuwa juhudi za wabunge wa mkoa wa Simiyu wamepeleka ombi kwa Rais Samia na tayari Bilioni 76.4 zimetolewa kwa ajili ya kujenga kituo cha kupozea umeme.

“Ndugu zangu haya mambo hayaji hivi hivi ni lazima yaje na kiongozi mwenye maono lakini Rais hawezi kuota ndoto kwamba Simiyu kuna tatizo la umeme ndio maana mna watoto na mtoto wenu katika jimbo la Bariadi ni Eng Kundo Mathew akishirikiana na dada yake Ester Midimu, pamoja na mdogo wake Mhe Lucy Sabu” Amekaririwa Mhe Kundo.

By Jamhuri