Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana amepongeza uamuzi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan Hassan wa kuunda wizara inayohusika na mipango.

Pia, amepongeza hatua ya kuifanya Tume ya Mipango kuwa chini ya ofisi ya Rais ambapo amesema itaongeza kasi na uhakika wa mipango ya maendeleo nchini.

Kinana ameyasema hayo jana wilayani Kibiti mkoani Pwani kupitia mkutano wa hadhara uliondaliwa na Mbunge wa Jimbo la Kibiti Ally Mpembenwe kueleza kazi kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM iliyofanyika katika jimbo hilo.

“Hivi karibuni Rais ameunda wizara mpya inayoshughulika na mipango, kwa lugha nyingine ni Tume ya Mipango ambayo ipo ofisini kwake, lengo lake moja tu, tumekuwa tukifanya mambo mengi nchi hii lakini bila mipango mizuri, Rais akaona wizara ile inapoitwa Wizara ya Fedha na Mipango inafanya kazi zaidi ya kukusanya na kutumia kuliko kupanga akaona hapana, nadhani ni vizuri sasa tutengengeze wizara ya mipango,” amesema.

Amesema Tanzania tangu Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere akiwa hai, wizara hiyo ilikuwepo, ndiyo iliyokuwa ikipanga maendeleo ya nchi hata hivyo baadae iliondolewa.

“Rais katika uzoefu wake akaona hapana, hakuna maendeleo bila ya mpango, hakuna mapato bila mpango, hakuna matumizi bila mpango, kwa hiyo wizara hii na tume hii itakapoanza kazi ninawahakikishia Watanzania maendeleo yatakuwa ya uharaka zaidi kuliko ya sasa na kuliko mlivyowahi kuyaona.

“Kwa hiyo tunampongeza sana Rais (Dk. Samia), tunakipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa sera nzuri kwa sababu na Rais wetu ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na yeye serikali ya inasimamia utekelezaji wa sera na Ilani (ya uchaguzi) ya Chama Cha Mapinduzi,” amesema.

By Jamhuri