Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Pwani

Mjumbe wa Kamati ya Sensa kitaifa na Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amewataka wananchi kutowabughudhi makarani wa sensa na badala yake kuwapa ushirikiano wafanikishe shughuli hiyo

Aidha Jafo amesema kamati imeridhika na maandalizi ambayo yamefanyika kwa makarani na vifaa vinavyohitaji.

Dk Jafo aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza kwenye Tamasha la Sensa lililoandaliwa na mkoa wa Pwani kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kuhesabiwa ambalo limefanyika Kisarawe.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge akizungumza na wananchi juu ya umuhimu wa kuhesabiwa katika sensa.

Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisarawe alisema makarani wa sensa wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa kuwapa taarifa zinazotakiwa makarani wa sensa badala ya kuwabughughi.

” Tuwape ushirikiano kwa kila wanachohitaji tusipowqpa ushirikiano itakuwa haina maana kutokana na maandalizi yaliyofanyika katika shughuli hii ya sensa, na tutambue kujua idadi itarahisisha serikali katika kwenye utekelezaji wa miradi” alisema

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge ametoa onyo kwa wanaotaka kutumia sensa kuhalifu kwamba watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Kunenge alisema hali ya usalama imeimarishwa hivyo wananchi waondoe hofu kwani yeyote atakayejaribu kuharibu shughuli ya sensa hatua zitachukuliwa.

Kwa mujibu wa Kunenge maandalizi ya mkoa huo yamefikia asilimia 96, na uhamasishaji umefanyika kwa njia tofauti ikiwemo ya michezo na matamasha mbalimbali kwenye wilaya za mkoa huo.